MBUNGE wa Viti Maalumu Mwanakhamisi Kassim Said (CCM) ameanguka ghafla na kuzirai Bungeni wakati vikao vya Bunge vinaendelea na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kupata msaada zaidi.
Tukio hilo lilitokea jana mchana mjini hapa wakati wabunge wakiendelea kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2011/2012. Hali hiyo ilishtua idadi kubwa wa watu waliokuwa wakifuatilia bunge kwa kiasi kikubwa kutokana natukio hilo la kuanguka ghafla.
Kuanguka kwa mbunge huyo kulisababisha Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kuanza kuhangaika kutafuta gari ya kusafirisha wagonjwa ili aweze kukimbizwa hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Akitoa taarifa ya kuanguka kwa mbunge huyo, Mwenyekiti wa Bunge Sylivester Mabumba aambaye alikuwa akiongoza mjadala wa bajeti muda huo aliwaeleza wabunge kuwa kuna mbunge ameanguka na kwamba amekimbizwa hospitali na kadri hali yake itakavyokuwa ikiendelee watapewa taarifa.
Hata hivyo mwenyekiti huyo wakati anawatangazia wabunge kuhusu kuanguka na kuzirai kwa mbunge huyo hakusema anasumbuliwa na ugonjwa gani ingawa taarifa za awali zilieleza kuwa anasumbuliwa na presha.
Wakati akianguka alikuwa amekaa karibu na Mbunge wa Jimbo la Chwaka, Yahya Kassim Issa ambaye muda mfupi alikuwa ametoka kuchangia bajeti hiyo. Hivyo baada ya kurudi katika kiti chake muda mfupi tu ndipo Mwanakhamis alipoanguka na kuzirai.
Kitendo hicho cha kuzirai kwa mbunge huyo kilisababisha baadhi ya wabunge kukimbilia katika eneo ambalo alikuwa amekaa mbunge huyo kwa lengo la kumsaidia. Kutokana na wabunge wengi kuzunguka kiti chake ilikuwa ngumu kufahamu kinachoendelea.
Baadaye ilikuja gari ya wagonjwa yenye namba STK 8346 eneo hilo la Bunge kwa ajili ya kumchukua. Hata hivyo kutokana na taratibu za kuingia katika eneo hilo gari ilisimama kwa dakika chache ili dereva akaguliwe kabla ya kuingia kumchukua.