Mbowe: Siwaogopi Polisi na Siwezi kuwakimbia

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Na Mwandishi Wetu, Arusha

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo amezungumza na vyombo vya habari leo mjini Arusha na kudai hajawakimbia polisi na wala hawaogopi pale anapoungana na wanachama wake kudai haki zao.

Mbowe ametoa kauli hiyo muda mfupi uliopita mjini Arusha na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linawaongopea wananchi kwa muda mrefu dhidi ya viongozi wa CHADEMA.

“Ndugu zangu waandishi wa habari, nitazungumza kwa kifupi sana mambo machache ambayo nafikiri ni ya msingi kwa mstakabali wa taifa hili. Nimepata taarifa kwamba Jeshi la Polisi linanitafuta na taarifa imetolewa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Arusha kwamba mimi nilikimbia katika mkesha ambao tuliutangaza katika Viwanja vya National Milling (NMC),” alisema Mbowe.

Amesema kitendo cha Jeshi la Polisi kutoa taarifa za uongo si kizuri kwani hawezi kuwakimbia kama wanavyodai katika viwanja vya National Milling na wala hawezi kuwakimbia wananchi pale wanapoungana nao kudai haki na madai ya msingi.

“Ni kweli polisi walipovamia eneo la tukio, binafsi sikuwepo kwa wakati ule. Na nilikuwa sipo katika eneo hilo kwa sababu ya ratiba zetu wenyewe za ndani za namna ya kupanga mikakati mingine ya kufanya na maandalizi mengine muhimu ambayo nilistahili kufanya na nisingeweza kufanya nikiwa katika eneo la tukio.”

“Lakini niliporejea katika eneo la tukio baada ya shughuli maalum niliyokwenda kufanya, ndiyo nikakuta purukurushani lile limeshaendelea na watu wameshakamatwa. Kwa hiyo eti nimekimbia sijakimbia, na wala siwezi kukimbia, sijifichi na wala siwezi kujificha. Mimi ni kiongozi ninayejiamini, siwezi kukimbia polisi wala siwezi kuogopa magereza.”

“…ningependa Watanzania wanielewe ni kwamba, kumekuwa na mikakati ya muda mrefu ya sana ya kudhalilisha CHADEMA na hususan viongozi wake ili kupunguza imani ya wananchi kwa viongozi wa CHADEMA. Na kumekuwa na propaganda kutaka kuonesha kuwa CHADEMA ni chama cha matatizo, ni chama kinachochochea vurugu na kwa misingi hiyo, vyombo vya dola vimekuwa vikitumika kuinyima haki CHADEMA, kunyima haki wabunge wa upinzani na kwa hiyo kuwanyima Watanzania wa kawaida haki,” alisema Mbowe.

“Kwa maana yake tumekuwa tuna-deal na matokeo ya kosa la msingi, lakini kosa (lenyewe) la msingi halitatuliwi. Serikali inakuwa bubu. Inaachia uongozi wa Mkoa wa Arusha na vyombo vya dola viendelee kuibana CHADEMA, viendelee kuiumiza Chadema, ili kuharibu reputation ya CHADEMA. Tumelalamika mpaka, nimezungumza na Waziri Mkuu Pinda na Waziri Mkuu akamweleza Msjaili wa Vyama vya Siasa aunde timu ya pande zote mbili, kwa CHADEMA na Chama Cha Mapinduzi, tukae kwenye meza tuzungumze wote,” alisema Mbowe katika taarifa hiyo,” aliongeza Mbowe.

Sasa katika resistance za kisiasa kuna kitu kinaitwa Civil disobedience, civil disobedience ni pale ambapo wanaharakati wanalazimika kuchukua hatua na wakijua kuwa zina madhara yanayoweza kupatikana kutokana na hatua hizo ili kufikisha ujumbe kwa wahusika.

“…Kwa kweli tumedhalilishwa kiasi kikubwa mno, tunaendelea kudhalilishwa na tutaendelea kudhalilishwa kwa sababu wamedhamiria kufanya hivyo. Na Mkuu wa Mkoa mpya, aliyeletwa Arusha huyu bwana anaitwa Magesa, ameletwa hapa kwa minajili hiyo. Na Magesa anatoa vitisho kwa kauli za kuwatisha watu na wanaharakati wasidai haki zao za misngi.

Mkuu wa Mkoa Magesa ni mwajiri wa serikali, lakini anakuja Arusha, Magesa anajipa mamlaka ya kutaka kutisha kila mtu na kwamba yeye ni mkuu wa mkoa, who is mkuu wa mkoa katika mazingira ambayo amepewa kazi na mtu mmoja na Rais Kikwete. Kwamba yeye anaweza kuja hapa, akatoa maagizo kwamba eti ni Kamati ya Ulinzi na Usalama imekaa na kuamua hatukai mchezo na Arusha! Anaijua vipi Arusha, amechaguliwa kwa kura ngapi Arusha, Magesa huyu…anamtisha nani Magesa!

Aidha amesema bunduki na mabomu wanayotumia askari si suluhisho bali mazungumzo kwa ajili ya haki. “Sasa mimi nakwenda polisi. Nakwenda polisi mimi na ningependa kuwahikishia polisi, napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu, siogopi polisi, siogopi magereza, simwogopi mtu yeyote, naogopa kweli na ninamwogopa Mungu,” alisema Mbowe.