VYAMA vya siasa vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, leo vitafanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani kuhamasisha wananchi wapinge kile wanachodai ni hujuma dhidi ya Mchakato wa Katiba Mpya.
Hatua ya kufanya mkutano huo, ilifikiwa jana baada ya wenyeviti wa vyama hivyo kumvamia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema ofisini kwake wakipinga kitendo cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kupiga marufuku maandamano waliyokuwa wayafanye leo jijini humo.
Katika mkutano wao na IGP Mwema, viongozi hao walikubaliana maandamano hayo yasitishwe kwa sababu za kiusalama, lakini wafanye mkutano huo wa hadhara.
Wenyeviti hao wa vyama vya Upinzani, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), ambao walikutana na Mwema jana mchana.
Hatua ya viongozi hao ilitokana na tamko lililotolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova kusitisha maandamano ya vyama hivyo yasifanyike.
Kova alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kuhofia yatasababisha kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi pamoja na kuwepo taarifa za kiintelijensia kwamba yatakuwa na vurugu.
Tamko hilo liliwakera viongozi wa vyama hivyo vitatu vilivyotangaza kushirikiana katika kupinga kile wanachodai ni uporaji wa haki ya wananchi kutunga Katiba yao.
Mazungumzo wenyeviti hao na IGP yalianza saa 6 mchana na kumalizika saa 11 jioni, ambapo walitoa taarifa ya pamoja kuhusu waliyokubaliana.
Akitangulia kutoa taarifa hiyo, kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema: “Tumekubaliana kesho tutafanya mkutano Viwanja vya Jangwani. Tumekubaliana kusitisha maandamano hadi Oktoba 5, (mwaka huu).”
Aliongeza kuwa wamekubaliana pia kwamba watafanya mkutano mwingine wa hadhara Visiwani Zanzibar, Jumatano ijayo.
Hata hivyo, katika taarifa ya pamoja, ulitokea kuhitilafiana kwa kauli, pale IGP Mwema alipokuwa akitoa ya upande wake.
Hali hiyo ilitokana na kauli ya Profesa Lipumba kusisitiza kuwa mikutano na maandamano ni haki ya msingi kwa vyama vya siasa na kwamba wanachopaswa ni kutoa taarifa kwa polisi na wala siyo kuomba kibali.
Awali, wakati Mwema akihitimisha taarifa hiyo ya pamoja alisema kuwa wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali cha maandamano hayo ya Oktoba 5.
Alisisitiza kuwa kazi ya polisi ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, hivyo wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali na baada ya polisi kuchunguza watakuwa na mamlaka ya kuridhia au kukataa ombi lao.
Mwema alisema haoni haja ya kuwepo malumbano na wanasiasa hao katika suala hilo kwa sababu lengo lao ni moja nalo ni kudumisha ustawi wa jamii.
“Wote tunajenga nyumba moja, sioni sababu ya kugombania fito,” alisema Mwema.
Mzozo wa Katiba
Mzozo wa vyama vya siasa vya upinzani ulianzia kwenye Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, lakini sasa umehamia nje ya Bunge na vyama hivyo vimetangaza azma ya kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Viongozi hao wa upinzani wanadai kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho.
Wanadai kuwa hali hiyo inatoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na CCM kupitia kwa rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Vyama hivyo viliazimia kuanza rasmi leo harakati za kuhamasisha umma kupitia maandamano na mikutano ya hadhara.
Ndoa hiyo ya wapinzani waliifunga, Septemba 15, kwa kuandika historia nyingine mpya kwenye tasnia ya siasa za Tanzania wakipinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
Wanadai mapendekezo mengi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yalipendekezwa na vyama hivyo, hivyo havitakuwa tayari kuona maoni hayo pamoja na ya Watanzania wengi yakichakachuliwa.
Wanasema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi.
Vyama hivyo vinadai kuwa vinaungwa mkono na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.
Misimamo ya wenyeviti
Profesa Lipumba anasema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, anaongeza kuwa suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Tunamshauri Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona, ila aurejeshe bungeni,” anasema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mbatia anasema historia ya nchi inaonyesha kuwa waasisi wa kutaka sauti, kauli na mawazo ya umma isikike katika kudai Katiba Mpya ni vyama vya upinzani.
“CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo. CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubakia” anasema na kuongeza;
“CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu wanakosea, hatuwezi kuangamiza wazo letu la kutaka Katiba Mpya, katika taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao.”
Mbowe anasema wameamua kuweka pembeni tofauti zao kwa ajili ya kudai Katiba Mpya ya Watanzania wote, kwamba hata wanahabari wanatakiwa kuweka pembeni itikadi za vyombo vyao vya habari vinavyomilikiwa na vyama vya siasa, kuwa wakweli katika kudai Katiba Mpya.
“Waandishi wa habari msiwe vipaza sauti vya watawala bila kutafakari kwa kina Tanzania ya miaka 100 ijayo itakuwaje, wanahabari mnaweza kutunyima Katiba Mpya au mkatunyima kama ikitumika vibaya,” anasema.
Anaongeza kuwa amani ya nchi inaweza kuvurugwa kama mchakato wa katiba utahodhiwa na chama kimoja cha siasa (CCM), “Ikiwa hivyo, sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani hiyo, amani inapatikana kunapokuwepo na haki.”
Huku akinukuu kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere cha ‘Freedom and Unity’, anasema, “Ni rahisi mno kuliwasha taifa la watu ambao wamekwazika, taifa hili watu wamekwazika sana. Mchakato wa katiba unaweza kutibu majeraha makubwa ambayo yanalikabili taifa.”
Anasema fursa adimu ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na bunge na CCM na anasisitiza kwamba wapinzani watatumia kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea ili washiriki katika kuidai katiba iliyotokana na mawazo yao.
“Wapinzani hatutarudi nyuma na hatutakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa katiba ya sasa. Hilo wenzangu (wenyeviti wenzangu) naomba mnielewe, Chadema hatukubali na naomba na nyinyi msikubali, maana ndani ya CCM kuna kundi linataka kurudi katika katiba hii tunayoilalamikia,” alisema.
Anasema katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere alisema, ‘Kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa makini’, kwamba hoja ya kutaka Amani itaharibiwa na wale wenye dola, siyo vyama vya upinzani.
Chanzo: Mwananchi