Na Mwandishi Wetu, Arusha
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeshutumu hatua ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (TAMISEMI), George Mkuchika, kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuwatambua madiwani watano waliofukuzwa na kuwalipa stahili zao pamoja na posho za vikao. waliokwua madiwani wa chama hicho watano akiwemo aliyekuwa Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Estomih Mallah.
Akizungumza na waandishi wa Habari nje ya mahakama ya Hakimu Mkazi
Mkoa wa Arusha, Freeman Mbowe ameshangazwa na hatua ya Mkuchika, kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuwatambua madiwani waliofukuzwa na kuwalipa posho za vikao.
Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema jana kuwa kitendo cha Waziri Mkuchika ni matumizi mabaya ya ofisi na fedha za walipa kodi. Alisema Waziri Mkuchika hana mamlaka ya kuwarudisha madiwani waliofukuzwa, kwani uamuzi huo ulifikiwa na chama na wakakata rufaa mbele ya Baraza Kuu la chama.
Hata hivyo, alisema madiwani hao wamefungua kesi ya kuzuia uamuzi wa chama wa kuwafukuza, ambayo bado ipo katika hatua ya awali ya kutajwa mahakamani. Alisema mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kutengeua maamuzi ya CHADEMA juu ya madiwani hao na sio Waziri Mkuchika.
Alisema uamuzi wa Mkuchika kuwarejesha madiwani hao unasukumwa na hoja ya ukada wa CCM zaidi badala ya kuiachia sheria ifuate mkondo wake. “Mkuchika kuamuru madiwani warudi na walipwe stahili zao ni kosa, Waziri anafanyakazi kwa niaba ya CCM na sio ya Serikali,” alisema.
Alisema hali hiyo inaonesha upendeleo unaofanywa na serikali na wamekuwa wakichochewa na CCM kuipasua CHADEMA. “TAMISEMI haina mamlaka ya kuwarejesha, na kufanya hivyo ni matumizi mabaya ya fedha…madiwani wanadhaminiwa na chama wakati wa uchaguzi hivyo, Mkuchika hawezi kuingilia hapo. Hii ni mbinu ya CCM kutaka kuvuruga Chadema,” alisema.
Alisema Mkuchika sio msemaji wa wizara isipokuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye naye amekwisha mwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kumwelekeza aitishe vikao kati ya makatibu wakuu wa vyama vya Chadema na CCM kuzungumzi kuhusu namna ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro kati ya vyama hivyo viwili.
Alisema anashangaa kuona Waziri Mkuchika amejitumbukiza katika suala hilo wakati sio msemaji wa wizara.