HalmashauriI Kuu(NEC) ya Chama cha NCCR-Mageuzi, imempa Mwenyekiti wake, James Mbatia, siku 21 kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na baadhi ya wanachama kwamba, ni pandikizi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya chama hicho.
Agizo hilo ni miongoni mwa maazimio kadhaa ya NEC yaliyofikiwa kwa kauli moja na idadi kubwa ya wajumbe wa halmashauri hiyo, katika kikao chake kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 50, lakini kinyume cha kawaida, waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuhudhuria.
Azimio hilo dhidi ya Mbatia lilisomwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Samuel Ruhuza katika kikao hicho na limezingatia kanuni za chama zinazotoa fursa kwa mwanachama mtuhumiwa kujitetea.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zinaeleza kuwa hoja kuhusu tuhuma hizo, iliwasilishwa katika kikao hicho na Mjumbe wa NEC kutoka Tanga, Mbwana Hassan. Hoja hiyo imesainiwa na wajumbe 28 wa halmashauri hiyo, ambao kwa kauli moja wanataka Mbatia ajiuzulu uenyekiti wa chama hicho kutokana na tuhuma zinazomkabili.
Kwa mujibu wa habari hizo, kati ya wajumbe waliohudhuria kikao cha jana, ni wajumbe 10 tu ndio wanaodaiwa kumuunga mkono Mbatia kuendelea kuwa mwenyekiti wa chama hicho, huku wengine waliosalia wakiwa hawana upande. Kutokana na agizo hilo, Mbatia sasa anatakiwa kujibu tuhuma hizo na kuwasilisha majibu hayo kwa Katibu Mkuu. Katibu Mkuu baada ya kuyapokea, atawasilisha kwa Kamati ya Maadili ya Chama na kisha kupelekwa katika kikao cha NEC kitakachofanyika Februari, mwakani kwa ajili ya maamuzi. Habari hizo zinasema kuwa baada ya azimio hilo kupitishwa na NEC, Mbatia aliomba kutendewa haki kwa kupewa muda wa kutosha kujibu tuhuma zinazomkabili.
Imeelezwa kuwa awali, viongozi waliokuwa wamekaa meza kuu walijaribu kuzuia hoja inayohusu tuhuma dhidi ya Mbatia kujadiliwa katika kikao hicho. Hata hivyo, idadi kubwa ya wajumbe walipinga hatua hiyo na kushinikiza ijadiliwe.
Mvutano kuhusu suala hilo uliendelea baada ya Mbatia kugoma kujibu tuhuma zinazomkabili. Jambo lingine lililotaka kulipua kikao hicho, ni madai kwamba, kulikuwa na mabaunsa waliokuwa wamekodiwa na baadhi ya wanachama kwa lengo la kutisha wajumbe na kuleta vurugu.
Hali hiyo ilimfanya Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali, kutishia kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, ili alete askari kwa ajili ya kuwashughulikia mabaunsa hao.
Mkosamali, ambaye ni mjumbe wa NEC, alifikia hatua hiyo baada ya baadhi ya wajumbe kutaka mabaunsa hao waondolewe, huku baadhi ya viongozi wakipinga suala hilo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI