Mazoezi ya Pamoja ya Kijeshi ya EAC Yaanza Burundi

Mazoezi ya Pamoja ya Kijeshi ya EAC Yaanza Burundi

Na James Gashumba, EANA-Arusha

MAZOEZI ya pamoja ya kijeshi kwa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yamefunguliwa rasmi nchini Burundi mwishoni mwa waiki. Zoezi hilo la kijeshi lililopewa jina la Ushirikiano Imara 2013 linafanyika katika kambi ya jeshi ya Muzinda, iliyoko km 19 kutoka jijini Bujumbura, Burundi.

Wanajeshi wapatao 269 kutoka majeshi ya EAC na wadau muhimu katika ulizni wakiwemo polisi na raia wanashiriki katika zoezi hilo linahusu opereheni za kiusalama na kupambana na ugaidi, uharamia na majanga.

Makamu ya Pili wa Rais wa Burundi, Gervais Rufyikiri alizindua rasmi zoezi hilo. Rufykiri alisema uwepo wa vikosi vitano vya EAC kutoka nchi wananchama kushiriki zoezi hilo ni ishara ya wazi yakuonyesha mshikamano miongoni mwa nchi hizo.

Aliyapongeza majeshi hayo pamoja na wadau katika kazi hiyo muhimu ya kujenga uzoefu na uwezo wa kushughulikia changamoto za kiusalama kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi,unyang’anyi na usafirishaji haramu wa binadamu.

“Nchi za EAC zina mambo mengi wanayofanana. Chochote kinachoikumba nchi moja inaathiri nchi nyingine,” alisema.

Naye Katibu Mkiuu wa EAC, Dk Richard Sezibera alisema mshikamano miongoni serikali za EAC, hususan masuala ya mafunzo ya ulinzi na ushirikiano wa kijeshi yanapeleka ujumbe mzito kwa maadui wa amani na kwamba EAC iko tayari kupambana na kuwashinda.