MABINGWA Watetezi wa Kombe la Klabu Bingwa Barani Afrika, TP Mazembe, kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema inatarajia kuwasilisha rufaa yake Shirikisho la Mchezo wa Soka Duniani (FIFA), badala ya mahakama ya Upatanishi ya Michezo (CAS).
Shirikisho la mchezo wa soka barani Afrika CAF, iliipiga marufuku TP Mazembe kutetea taji lake baada ya Klabu ya Simba ya Tanzania, kulalamikia uamuzi wa klabu hiyo wa kumshirikisha Janvier Besala Bokungu kama mchezaji wake.
Awali klabu ya TP Mazembe, ilisema itawasilisha rufaa yake kwa mahama ya upatanishi ya micheszo CAS. Lakini baada ya muda wa mwisho kuwadia, bila ya Mazembe kuwasilisha rufaa yake, Klabu hiyo imesema itawasilisha malalamishi yake kwa FIFA.
Klabu hiyo kutoka DRC, iliishinda Simba kwa jumla ya mabao 6-3 katika raundi ya pili ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Afrika, lakini Simba ikahoji uhalali wa Bokungu kuichezea Mazembe.
TP Mazembe, imeteuwa mawakili kutoka Ubelgiji Luc Mission na Gregory Ernes kuwasilisha rufaa yao kwa FIFA.
Wachezaji wa TP Mazembe kabla ya mechi yao dhidi ya Simba ya Tanzania
Bokungu, mwenye umri wa miaka 22 mzaliwa wa Congo, alihamia klabu ya Esperance ya Tunisia kutoka Mazembe mwaka wa 2007 na kujiunga tena na klabu Mazembe mapema mwaka huu.
Ripoti zinasema Bokungu, alikiuka mkataba wake na Esperance ambao ungemalizika mwezi june mwaka huu, lakini mawakili wa Mazembe wanasema uhamisho wa mchezaji huyo ni halali.
Mazembe imeshinda kombe la klabu bingwa barani Afrika kwa miaka miwili iliyopita na pia ilifuzu kwa fainali za kombe la klabu bingwa ulimwenguni, ambapo ilishindwa 3-0 na klabu ya Inter Millan, kutoka Italia.