Mawaziri wameonesha uzalendo kwa wanafunzi Ustawi wa Jamii

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

“KWA kauli hiyo, Kamati Maalumu hii ya dharura inapenda kuutangazia umma kuwa, Serikali imeyapokea vizuri maombi ya Kamati na pia, inawapongeza Mawaziri na waheshimiwa wabunge kutokana na ushirikiano na ukarimu walioionesha Kamati hii.”

Ndivyo inavyosema sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamati Maalumu ya Dharura iliyoteuliwa na Mkutano Mkuu wa Wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii uliofanyika Julai 21, 2011 baada ya Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo, Mlwande Madihi, kutangaza kuwa Taasisi (Chuo) imefungwa kwa kipindi kisichojulikana kutokana na mgomo usio halali wa wahadhiri.

Taarifa ya Kamati hiyo inayoundwa na wanakamati 13 iliyosainiwa na Kaimu Mwenyekiti wake, Chrisant Mutatina (Spika wa Bunge la Wanafunzi wa Taasisi), Makamu Mwenyekiti Mariam Saad na Katibu Kitamogwa Safari (Waziri wa Elimu-ISWOSO), imeeleza kuwa chanzo kufungwa kwa Chuo ni pamoja na mgogoro sugu baina ya wahadhiri hao na Menejimenti. Kimsingi, kufungwa kwa Chuo katika kipindi hiki, kumekuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi hao ambao ni tegemeo la taifa.

Katika ufafanuzi wa taarifa hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Mutatina anasema mjini hapa kuwa, “Wanafunzi tumeathirika sana kuona kwamba Acting Principal (Kaimu Mkuu wa Taasisi) anasema, Chuo kimefungwa kutokana na mgomo usio halali wa wahadhiri, lakini cha ajabu wanafunzi ndio wanaonekana kama wanaoadhibiwa kwa kutakiwa kuondoka chuoni mara moja. Hii ni ajabu maana tulitegemea kwa kuwa kosa sio la wanafunzi, basi labda waondolewe waliogoma lakini sisi wanafunzi tupewe msaada na hifadhi zaidi maana sisi hatuhusiki na mgomo.”

Kwa upande wake, Mariam Saad (Makamu Mwenyekiti) anasema, “Hivi kweli wanafunzi wametendewa haki? Menejimenti na walimu wanashindwa kuelewana, wanafunzi wanatimuliwa ndani ya masaa; wengine tunatoka mikoa ya mbali na wengine hata nje ya nchi; waende wapi kama sio kuwatuma kufanya ufuska na vitendo vya uhalifu? Hivi hapa haki iko wapi?”

Taarifa hiyo inayataja baadhi ya madhara wanayowakumba wanafunzi wa Taasisi hiyo kuwa ni pamoja na ugumu wa maisha kwa kuwa mkataba wao na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya juu ulikwishamalizika hivyo, hawana sehemu wala njia nyingine ya kujiingizia kipato ili kumudu maisha na kwa mantiki hiyo, kuwatimua na kuzidi kuchelewesha muda wa kuhitimu ni kuwatia hatarini wakiwa hawana kosa.

Wanasema, awali ilikuwa Chuo kifungwe kwa semister (muhula) ya pili mwezi Julai mwaka huu kama ilivyo kwa vyuo vingine na hivyo, wahitimu kumaliza mitihani yao na kurudi nyumbani na kazini, lakini kwa sababu mbalimbali za kiutawala, muda huo ukaongezwa hadi Septemba 2, 2011 hali iliyowafanya waishi katika mazingira na kipindi kigumu kwani muda wao wa ruhusa kazini umemalizika.

“Wengine walikuwa wanaishi katika hosteli za Chuo, hao wakapewa saa chache waondoke huku wakisimamiwa na polisi; waende wapi na mkataba wa pango la hosteli unasemaje na lingine kubwa zaidi, waliopanga katika hosteli za nje ya chuo (kwa watu binafsi) nao muda wa mkataba wa pango umeisha, wanatimuliwa na wenye nyumba na kutakiwa kulipia upya pango; wafanye nini huku kosa sio lao?” anasema Kitamogwa.

Katika ufafanuzi wake, Kitamogwa anaongeza kuwa hali hiyo inawadfhuru wanafunzi bila kosa kwa kuwa kama alivyosema Kaimu Mkuu wa Taasisi katika Tangazo la kufunga Chuo kwamba, Chuo (Taasisi) kimefungwa kutokana na mgomo usio halali wa wahadhiri uliosababisha ufundishaji usio na ufanisi na hivyo kusababisha tishio la uvunjifu wa amani; kama hivyo ndivyo, kwanini ugomvi wa Menejimenti na wahadhiri wanafunzi ndio waumie?”

Uchunguzi umebaini kuwa siku ya kufungwa kwa Chuo ilitanguliwa na Mkutano Mkuu wa Wanafunzi uliouomba Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi kupitia Rais wao, Gerald Julio Simbeye awaombe Menejimenti wawape nafasi wajadili kwanza yaliyojili katika kikao kama hicho kilichopita na ndipo Rais huyo akaiomba Menejimenti kuwapa nafasi hiyo.

Imebainika kuwa kutokana na hali hiyo Menejimenti hiyo ikiwakilishwa na Kaimu Mkuu wa Taasisi (Mlwande Madihi na Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo, Andrew Mchomvu) walifanya jaribio la kutaka kulaziimisha kubaki ndipo wanafunzi wakaanza kuimba, “Waondokeee waondokeee! Waondokeee!”.

Wanafunzi wanasema baada ya mjadala wao kumalizika waliutuma ujumbe wa Serikali ya Wanafunzi kuwaita Menejimenti lakini menejimenti ikagoma na badala yake, wakapata taarifa kuwa hatima ya Chuo kutokana na upungufu wa walimu unaosababishwa na takriban walimu watano kufukuzwa na wengine takriban 21 kuwa katika mgomo, wataipata siku iliyoafuata saa 4: 00 asubuhi toka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Taasisi.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, wanafunzi kadhaa waliozingumza na gazeti hili wanasema walishangaa kuona Kaimu Mkuu wa Taasisi na Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo wakiambatana na Rais wa ISWOSO pamoja na maofisa wa polisi na walipofika, Kaimu Mkuu wa Taasisi akatangaza kufungwa kwa Chuo kwa muda usiojulikana.

Hapo ndipo wanafunzi hao walipopigwa na butwaa huku wengine wakilia wasijue la kufanya na hatimaye, wakaunda Kamati Maalumu ya Dharura kwenda kupeleka kilio na mapendekezo yao kwa Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi huku wakizingatia kuwa, mawaziri na manaibu waziri wako bungeni Dodoma.

Kamati hiyo iliyoundwa na Mkutano Mkuu ilikuwa na wajumbe ambao ni pamoja na Gerald J. Simbeya (Rais wa ISWOSO), Boniphace Benezeth, Khadija Mkwama, Tatu Said, Joseph Sabinus, Godfrey Kinogo (Waziri wa Mikopo- ISWOSO), Johnson Rutechula, Julieth Muchunguzi, Machibya Mayala na Kenan Edwin. Hata hivyo, Simbeye (Rais), Tatu Said na Kenan Edwin walishindwa kufika Dodoma kwa sababu mbalimbali zikiwamo za kifamilia.

Baada ya kufika Dodoma Julai 24, 2011 inasema sehemu ya taarifa ya Kamati hiyo kwa vyombo vya habari, ilionana na viongozi mbalimbali wa Chama (CCM) na Serikali ngazi ya kitaifa wakiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Hussein Mponda na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Lucy Nkya.

Taarifa inasema Kamati hiyo ilitoa mapendekezo yake kwa viongozi hao ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali iwaonee huruma kwa kuwa wanaathirika kutokana na mgogoro usiowahusu hivyo, wakaiomba ifanye kila iwezekanalo kuwarudisha mapema masomoni ili wasizidi kuathirika ikiwa ni pamoja na kuzidi kupoteza fursa mbalimbali za ajira walizo nazo hasa wahitimu watarajiwa.

Uchunguzi umebaini kuwa, katika mazungumzo yao na DK. Kawambwa (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) aliahidi kukutana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii (Dk. Mponda) kujadili na kutafuta suluhisho la haraka na la kudumu la kwa mgogoro usioisha wa Taasisi hiyo na kuahidi kushughulikia ombi la wanafunzi. Waziri Kawambwa aliwasihi wanafunzi kuwa wavumilivu na waendelee kujisomea wakati Serikali ikishughulikia matatizo yao.

Kwa mujibu wa mazungumzo na viongozi wa Kamati hiyo, Waziri Kawambwa alisema atamshauri Waziri Mponda kufanya mazungumzo mengine ya pamoja yatakayowahusisha wadau wa Taasisi hiyo wakiwamo watendaji wa NACTE, Menejimenti, wahadhiri, wanafunzi na Serikali.

Dk. Nkya aliwaambia wanafunzi (Kamati) kuwa watulivu kwa kuwa Serikali inashughulikia suala hilo na kwa nyakati tofauti, Dk. Mponda alisema kiini cha migogoro ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii bado kinachunguzwa na kutafutiwa suluhisho la kudumu haraka. Aliwataka wanakamati kupeleka kile alichokiita “habari njema” kwa wanafunzi wenzao.

Katika mazungumzo hayo na Dk. Mponda yaliyofanyika katika Ofisi za Bunge, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) alimwambia Waziri Mponda kuwa, kwa kuwa inafahamika wazi kuwa mgomo haukuwa wa wanafunzi na pia wanafunzi hawakuwa sehemu ya mgogoro, Chuo kitakapofunguliwa ni vyema wanafunzi wote warudishwe chuoni bila masharti wakiwamo wanakamati wote.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyothibitishwa Mbunge huyo, Waziri Mponda alisema kuhusu hoja hiyo kuwa, wanafunzi hao kwa vyovyote siyo sehemu ya mgogoro, bali ni waathirika na hivyo, Serikali iko makini kuhusu usalama wao ukiwamo wa kimasomo.

Mbunge wa Kinondoni (CCM) ilipo Taasisi ya Ustawi wa Jamii Iddi Azzan aliyeshiriki mazungumzo hayo, alimwambia Waziri Mponda kuwa Serikali haina budi kushughulikia haraka kero zilizopo katika Taasisi hiyo kwa wakati ili wanafunzi wamalize muhula wa masomo kwa wakati kwani wao sio sehemu ya mgogoro na hivyo, kuiepushia gharama mbalimbali zisizo za lazima.

Waziri Mponda alisema, Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi kwa muda ambao unaweza kuongezeka kutokana na mgogoro huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamati hiyo ilipendekeza kwa viongozi hao mbalimbali ikiomba Serikali iingilie kati tatizo lilopo katika taasisi hiyo ili iweze kuendelea na utoaji wa huduma zake kwa wakati mwafaka.

Niliwahi kumsikia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama akisema, “The society needs solutions and not answers.” Kwamba, jamii inahitaji majawabu na sio majibu maana kama ni majibu, hata hapana pia ni jibu na kwa msingi huo, ndiyo maana ninasema, umefika wakati vyombo na taasisi za serikali kufanyia kazi vyanzo vya migogoro, badala ya kushughulikia matokeo.

Hii ni kusema kuwa, kiini hasa cha mgogoro katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii kitafutwe na kipatiwe ufumbuzi kwa kuwa kipo na pengine labda tatizo ni nani wa kumfunga paka kengere. Bila hilo kufanyika kwa umakini, wimbo wa migogoro katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii hautaisha na badala yake, kama sio kufungwa kabisa, Chuo kitalazimika kuishia kutoa cheti (certificate) au Stashahada (Diploma) pekee ili kulinda maslahi binafsi ili mradi tu, ukweli unabaki paleplae kwamba bila kumpata na kumtoa malkia wa mchwa, kichuguu cha matatizo hakitaisha na badala yake, fahari watapambana, lakini nyika zikaumia bila kosa.

Wanakamati na baadhi ya wanafunzi nje ya Kamati waoliozungumza kwa nyakati tofauti, wanasema wanashangaa kusikia baadhi ya watu wakieneza uvumi na upotoshaji kwa makusudi kuwa wanafunzi waligoma ilihali hata taarifa ya maandishi ya Kaimu Mkuu wa Taasisi inatamka bayana kuwa Chuo kimefungwa kutokana na mgomo usio halali wa wahadhiri. Hii inalenga kuficha makosa ya baadhi ya watu.

“Utashangaa wengine wakiwamo wasomi kabisa na wenye nafasi za juu wanasema wanafunzi walifanya kosa kukaa mkutano siku mbili; hii ni ajabu maana siku ya kwanza waliambiwa watapata majibu toka Bodi ya Magavana siku itakayofuata saa nne asubuhi, kisha watoa majibu wakawa hawaonekani na wanafunzi tukawa tunasubiri majibu kama tulivyoahidiwa sasa bila kuwapo kwa muda tulioambiwa na Rais wetu, hayo majibu wangetuletea nyumbani?” alihoji mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini huku mmoja wa wanakamati akisema, “Tunashukuru ukweli kuhusu taasisi hii unajulikana kwa viongozi wengi ambao wanasema wanaufahamu kiini chake na maslahi inayotafutwa..”

Wanafunzi hao wanasema wanashangazwa na uvuimi kuwa waligoma na kufanya vurugu, lakini wanaodai hivyo wanashindwa kueleza waligoma nini wakati wanadai masomo ambayo hayafundishwi na ama kusema vurugu zilizofanyika zilikuwa zipi.

“Ndiyo maana Kamati inapenda kuutangazia umma kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi zimeyapokea maombi ya Kamati na inawapongeza waheshimiwa mawaziri hao kutokana na ushirikiano na ukarimu waliouonesha kwa Kamati na pia, inawashukuru Mheshimiwa Mwigulu (MB) na Mheshimiwa Idd Azzan (MB) kwa ushirikiano wao,” anasema Kitamogwa na kuongeza, “Kwa mfano, kupitia kwa Waheshimiwa hao Idd Azzan na Mwigulu Nchemba, ikiwa na wajumbe kumi, Kamati kamati ilikaribishwa katika kikao cha Bunge Julai 27, 2011.”

Wakati wakiishukuru Serikali na wabunge hao wa Chama Cha Mapinduzi, wanakamati hao wakiwa Dodoma wanasema wanasikitishwa na iliyomnukuu Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Dodoma Zelothe Stephen kuwa wanafunzi wanane wajumbe wa Kamati hiyo wakiwa wa jinsi tofauti walikamatwa wakiwa katika chumba kimoja cha nyumba ya kulala wageni usiku wa manane.

Kimsingi wanasema wanaamini huenda Kamanda Zelothe alinukuliwa vibaya au hakueleweka vizuri katika taarifa yake na hivyo, wanasema kamati hiyo inapenda kuujulisha umma kuwa wajumbe walifika katika hoteli hiyo na kila mjumbe alikuwa na chumba chake.

Ndiyo maana ninasema, pamoja na kuwapa pole wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, ninawapongeza Mawaziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Waziri na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na wabunge wa CCM huku nikisema, wameonesha uzalendo kwa wanafunzi Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa uchungu wa mwana aujuae ni mzazi.