Mawaziri Wajadili Sheria Itakayoruhusu Mashoga Kuoana na Kupata Watoto Ufaransa

Baraza la Mawaziri

MIPANGO ya sheria mpya itakayowaruhusu wapenzi wa jinsia moja nchini Ufaransa kuoana na kupata watoto inajadiliwa katika mkutano muhimu wa baraza la mawaziri la Rais Francois Hollande.

Ufaransa inaruhusu uhusiano wa pamoja kati ya wapenzi wa jinsia moja lakini rais wa nchi hiyo alioongoza jitihda za kuwaongezea haki zao kama sehemu ya kampeini yake ya uchaguzi mapema mwaka huu.Sasa anakabiliwa na upinzani mkali kuhusu fikira hiyo kufuatia maandamano kote nchini na shutuma kutoka kwa kanisa katoliki.

Kwa wapenzi wengi wa jinsia moja, mabadiliko katika sheria hii yalipaswa kufanyika kitambo. Wanataka nafasi sawa kuwa na familia kama ilivyo kwa wapenzi wengine wa kawaida. Katika sheria hiyo iliyopendekezwa, wapenzi wa jinsia moja wataruhusiwa kuasili watoto kwa pamoja. Na kutakuwa na mabadiliko katika stakabadhi rasmi, ambapo mama na baba wataondolewa na badala yake kuwekwa mzazi wa kwanza na mzazi wa pili.

Lakini mabadiliko hayo yaliyopangwa yameshutumiwa vikali na wanasiasa wa mrengo wa kulia ambapo mmoja alisema huenda hili likachangia ndoa za wake au waume wengi. Mswada huu utakapowasilishwa kwenye baraza la mawaziri, utajadiliwa bungeni ifikapo Januari.

Chama cha kisoshalisti cha Rais Hollande kina wingi wa wabunge wanaohitajika lakini kutokana na kuwepo mzozo huenda akawa anategemea kura zote kuhakikisha kuwa mswada huo utapitishwa na kuwa sheria.
-BBC