Mawakala Morogoro kuishtaki Serikali

Na Mwandishi Wetu
Morogoro

MAWAKALA wa pembejeo wanakusudia kuiburuza mahakamani Serikali mkoani Morogoro kwa kile kushindwa kulipa deni la zaidi ya sh. bilioni 3, gharama ambazo zilitumiwa na mawakala hao kusambaza pembejeo msimu wa kilimo wa 2009/10 na 2011/12.

Hatua hilo imepitishwa juzi mara baada ya kumalizika kwa kikao cha mawakala hao kilichokaa kutafuta ufumbuzi wa madeni ambayo wamekuwa wakiidai Serikali kutokana na huduma mbalimbali wanazozitoa kwa mujibu wa makubaliano.

Mwenyekiti wa mawakala hao, Seladius Tesha amesema kwa sasa wanawasiliana na wanasheria kuangalia namna ya kufanikisha azma yao ya kuipeleka mahakamani Serikali mkoani hapo.

Akifafanua zaidi, Tesha alisema kwa msimu wa 2010/ 11 tayari wamesambaza pembejeo kwa zaidi ya asilimia 60 hivyo wanaidai Serikali zaidi ya bilioni 3, huku deni la nyuma ambalo ni sh. milioni 800 kwa wilaya za Kilombero na Kilosa likiwa bado halijalipwa.

Alisema wanachohitaji kwa msimu huu ni tamko la Serikali kuwa ni lini fedha zao zitaanza kulipwa, huku wakitaka mwanasheria wao atoe ufafanuzi wa namna ya Serikali kulipa fidia kwa mawakala hao kutokana na uzembe unaojitokeza katika ucheleweshwaji wa malipo.

Mawakala hao wote kutoka Mkoa wa Morogoro; Mohamed Ngaula, Leisius Msagala, Gerald Mlenge na Mwahija Mohamed walisema hivi sasa wanakabiliwa na madeni makubwa na kwamba baadhi ya mali zao zikiwemo nyumba zipo hatarini kupigwa mnada na wadeni wao zikiwemo benki na saccos.

Aidha kwa nyakati tofauti walibainisha kuwa madeni mengine ni kutoka kwa wazalishaji wa mbegu na mbolea, kama kampuni za TANSEED na MINJINGU, ambao huingia nao mkataba wa kusambaza mbegu na mbolea kwa wakulima na mawakala wenzao zikiwemo pembejeo.

Hata hivyo, mawakala kutoka Wilaya ya Kilosa wameeleza kushangazwa na hatua ya benki kukataa kupokea vocha zao ili kuondoa wakati wa malipo, sambamba na urasimu unaofanywa wakati wa kusainiwa kwa vocha hizo ngazi ya wilaya. Wamelalamikia kitendo cha kiongozi mmoja ngazi ya wilaya asiye na dhamana kulazimisha vocha zipitie ofisini yake jambo ambalo limeleta usumbufu.

Naye Meneja wa Benki ya NMB, Tawi la Wami, Morogoro, Emmanuel Bushiri, amekiri ucheleweshaji wa malipo kuathiri benki hiyo katika mzunguko wa fedha, huku akidai mawakala wanadaiwa riba kuendelea kukua. Aliongeza kuwa kwa mawakala ambao wameshapitishiwa vocha zao tayari wameingiziwa fedha kwenye akaunti, ingawa baadhi walipinga hatua hiyo kufanyika.

Mshauri wa Kilimo Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro, Aulelia Minja alisema hajui ni lini fedha hizo zitalipwa japokuwa aliwataka walalamikaji kuwasilisha vilio vyao katika mamlaka husika badala ya kuishia kulalamika pembeni.