Na Mathias Canal, Dodoma
MAONESHO na Mashindano ya mifugo Kitaifa sanjari na Maonesho ya Kilimo yametoa changamoto ya kuleta mapinduzi katika Ufugaji, Uvuvi, na Kilimo na kutoa ajira hususani kwa vijana kuwaongezea zaidi kipato na kuondoa umasikini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana na Ajira, Antony P. Mavunde wakati akifunga maonesho ya wakulima Nane nane Kanda ya Kati Dodoma yaliyokuwa yanafanyika katika uwanja wa Nzuguni kwa kauli mbiu ya “Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni nguzo ya Maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu (Hapa Kazi Tu).
Amesema kwa kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli inatekeleza azma ya kuhamishia makao makuu mjini Dodoma ameishauri Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ile ya Biashara na masoko kuangalia uwezekano wa kuanzisha rasmi maonesho ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi ya Kimataifa (International Agriculture Trade Fair) katika uwanja wa Nzuguni ambao ndio uwanja wenye eneo kubwa kwa maonesho ya Kilimo hapa nchini.
Aidha ametoa wito kwa Wizara, taasisi/Makampuni ya umma na binafsi, Mabenki na wadau wote wa kilimo na mifugo kuendelea kuwasaidia wakulima na wafugaji hapa nchini ili kuongeza uzalishaji kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vinavyokusudiwa kuanzishwa.
“Naomba niwaambie wakulima na wafugaji wetu kuwa maonesho ninayoyafunga hii leo ni muafaka na fursa nzuri kwao hususani vijana kwenda kuanza mara moja kutumia mlichojifunza na kuleta mapinduzi yenye maendeleo chanya yanayotarajiwa kiuchumi, hivyo napenda kuchukua nafasi hii kuzikumbusha Halmashauri za serikali za mitaa zote kuwahamasisha wakulima, Wafugaji na wadau wengine kutumia teknolojia zilizooneshwa hapa kuongeza ufanisi wao katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi,” alisema Mavunde.
Naibu waziri huyo pia ametoa zawadi kwa washindi katika Halmashauri za Mkoa wa Dodoma na Singida, Wizara za serikali, Taasisi za uzalishaji wa serikali, Makampuni ya pembejeo za Kilimo na Mifugo, Makampuni ya zana za Kilimo na Mifugo, Taasisi za serikali na Mashirika ya Umma, Taasisi za fedha na Mabenki, Taaisisi za mafunzo na utafiti, Taaisisi zisizo za kiserikali (NGOs na CBOs), Taasisi za mawasiliano ya kibiashara, Mamlaka za udhibiti, Vyombo vya habari, na Kampuni za nishati mbadala kwa kufanya vizuri katika maonesho hayo.
Pia zawadi hizo zimetolewa pia kwa watu wenye mashamba makubwa ya ufugaji ng’ombe wa maziwa, Wafugaji wadogo wa ng’ombe wa nyama, Wafugaji bora, na Wakulima bora. Sambamba na hao pia Jeshi la Kujenga Taifa JKT limeibuka kidedea kwa ushindi wa jumla likifuatiwa na Jeshi la Magereza ambapo nafasi ya tatu imechukuliwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvu.
Akitoa maelezo ya awali kuhusu maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa Malengo ya maonesho hayo ni utoaji elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wadau wengi kwa muda mfupi lakini pia wadau kujionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali, mashirika ya umma na binafsi.
Mtaturu alisema kuwa mpaka tarehe 7 hapo jana jumla ya watu waliokuwa wametembelea inakadiriwa kuwa 40,000 huku matarajio ya siku ya ufungaji ikitarajiwa kuongezeka watu 12,000 na kufikia idadi ya watu 52,000.
DC Mtaturu amesema kuwa Teknolojia/Bidhaa zilizooneshwa ni pamoja na zana za Kilimo, Mbegu bora za mazao mbalimbali, Uzalishaji wa mazao katika mazingira yaliyodhibitiwa (JKT Kondoa) Taasisi za kitafiti ambazo zimeonyesha teknolojia mbalimbali za kuongeza tija zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali, Utengenezaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, Uboreshaji wa viasilu ili kupata mifugo na mazao ya kilimo yanayostahimili hali ya hewa ya kanda ya kati na udhibiti wa magonjwa.
Pia uzalishaji bora wa mazao ya nafaka, ubunifu wa teknolojia rahisi za kutotoa mayai, Kuongeza thamani mazao ya mifugo, Makampuni ya mawasiliano, Taasisis za elimu zimeonyesha ubunifu wa kumsaidia mfugaji, Tiba za asili, Wasindikaji wakubwa na wadogo wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Asali, na Nta.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya waandaaji wa Maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amemshukuru mgeni rasmi Antony P. Mavunde kwa kuitikia wito wa kufunga maonesho hayo ambapo pia ameishukuru Benki kuu ya Tanzania (BOT), Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, LAPF, Mkuu wa Mkoa wa Singida na Chuo kikuu cha Dodoma kwa uwakilishi na uchangiaji kwa ajili ya maonesho hayo.
Maonesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane Kanda ya kati Dodoma yaliyohusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi, mabenki, Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali yalifunguliwa tarehe 03 Agosti 2016 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe.