Mauzo DSE Yashuka kwa Asilimia 81

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa akizungumza

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa akizungumza

Na Ally Daud-Maelezo

MAUZO katika Soko la Hisa Dar es salaam (DSE) yameshuka kwa asilimia 81 kutoka Tsh. Bilioni 9 mpaka kufikia shilingi bilioni 1.7 kutokana na kushuka kwa idadi ya uuzaji wa hisa kufikia shilingi 340,000 kwa wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Afisa Mwandamizi wa masoko wa DSE, Bi. Mary Kinabo amesema kuwa mauzo hayo yameshuka kutokana na ukubwa wa mtaji wa soko kushuka kwa asilimia 2.79 kutoka trilioni 21.3 kufikia trilioni 20.7.

Aidha Bi. Mary amesema kuwa ukubwa wa mtaji kutoka makampuni ya ndani umebaki kwenye kiwango kile kile cha shilingi trilioni 8.2 kutoka wiki iliyopita. Bi. Mary amesema kuwa licha ya idadi ya mauzo kushuka pia Benki ya CRDB imeshika nafasi ya kwanza katika kuuza na kununua hisa kwa asilimia 53 ikifuatiwa na kampuni ya Bia nchini TBL kwa asilimia 35 huku kampuni ya Swissport ikishika nafasi ya tatu ya kununua hisa kwa asilimia 3.

Mbali na hayo Bi. Mary amesema kuwa licha ya viashiria vya soko kushuka kwa alama 36.6 baada ya bei za hisa kutoka TBL kushuka kwa silimia 1.08, viashiria vya huduma za kibenki na kifedha vimepanda kwa alama 3.64 baada ya mauzo ya DSE kupanda kwa asilimia 11.5.