Na Joachim Mushi
JESHI la Polisi nchini limekata tamaa kuendelea na juhudi za kuwashawishi ndungu wa marehemu wa miili iliyouwawa kwa risasi baada ya kundi la watu takriban 800 kudaiwa kuvamia mgodi wa Barrick na kutaka kuiba mchanga wa madini mgodini hapo.
Akizungumza kwa njia ya simu jana kutokea Tarime, Kamishna Oparesheni wa Polisi, Paul Chagonja alisema wameamua kuwaachia ndugu wa marehemu na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao wamekuwa wakiwarubuni wanandugu kuzira kuizika miili hiyo.
Chagonja alisema viongozi wa CHADEMA, wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amekuwa akiwashawishi wananchi na ndugu wa marehemu hao kuacha kuzika miili hiyo hadi pale watakapo leta madaktari wao na kufanya uchunguzi chini ya mwanasheria wao.
Alisema kitendo anachokifanya Lema si cha kiungwana kwani amekuwa akitumia uelewa mdogo wa wanandugu na kuwazuia wasiendelee na mazishi hadi pale uchunguzi wao utakapomalizika, jambo ambalo alidai ni upotoshaji.
“Mimi sijui huyu mbunge anamatatizo gain (Lema) yaani ametoka kwenye jimbo lake (Arusha Mjini) amekuja huku anatumia uelewa mdogo wa masuala ya sheria na kuwazuia wasiendelee na mazishi, sisi tumeamua kuwaachia tuone wanafanya nini ila najua mwishoni watawatelekeza…,” alisema Chagonja.
Alisema suala hilo si kwamba polisi wamekataa kukiri kuua watu hao, lakini wameweka wazi kuwa mazingira ambayo wavamizi walifanya ndio yaliyowalazimisha kuua, kwani walikuwa wakipambana na askari kwa silaha za jadi jambo ambalo ni hatari.
Hadi Chagonja anafanya mazungumzo na gazeti hili ndugu wa wafiwa walikuwa wamefichwa nyumbani kwa Diwani mmoja wa CHADEMA na polisi walikuwa wakiangaika kuwatafuta ili kuendelea kuwashauri.