Mauaji Haya ya Albino Mpaka Lini?

 

Mmoja wa wahanga wa imani hizi za kikatili na za aibu

Mmoja wa wahanga wa imani hizi za kikatili na za aibu.

 

 

Na Evarist Chahali

25/2/2015

 

“Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote, Nchi yangu Tanzania, jina lako ni tamu sana Nilalapo nakuwaza wewe, niamkapo ni heri mama wee. Tanzania Tanzania, nakupenda kwa moyo wote.” Huu ni ubeti wa wimbo maarufu ambao ‘zamani hizo’ tulipouimba tulijisikia ‘raha’ flani kuhusu nchi yetu. Tulikuwa na kila sababu za kuipenda Tanzania kiasi cha kuiota tulipolala. Peleka mbele (fast-forward) hadi zama hizi tunaoishi, hutolaumiwa ukijiuliza ‘ninaipenda Tanzania kwa lipi hasa, maana kila kukicha tunakumbana na habari au matukio yanayoweza kumfanya mtu amlaumu Muumba kwa kumfanya azaliwe katika nchi yetu.
Tuweke kando ufisadi unaokurupuka kila kukicha, tusahau kuhusu wawakilishi wetu wanaotugharimu mamilioni ya shilingi kila mmoja kwa mwezi kisha wakifika bungeni inakuwa ni matusi, vijembe, na upuuzi kama huo. Tufumbie macho nchi yetu inavyouzwa rejareja kwa kisingizio cha uwekezaji huku baadhi ya wawekezaji hao wakija na briefcase tupu na kuondoka na mabilioni. Na tusamehe aibu ya kugeuka ombaomba wa kimataifa huku Rais wetu akiwa ziarani nje mara kwa mara kwa ‘kisingizio’ hicho. Twaweza kuweka kando kila jambo ‘baya’ kuhusu Tanzania yetu lakini haiwezekani kabisa kupata kisingizio katika unyama wa hali ya juu unaoendelea nchini mwetu dhidi ya ndugu zetu maalbino. Kinachofanywa kwao si dhambi tu bali ni aibu kubwa kwa taifa letu.
Majuzi tu rafiki yangu mmoja hapa Uskochi aliniuliza, “Evarist, hivi asili yako ni Zimbabwe au Tanzania?” Nami bila uoga nilimjibu kuwa ninatokea Tanzania. Kisha likafuata bomu, “Nimeona kipindi flani kwenye televisheni kinaonyesha jinsi maalbino wanavyouawa Tanzania kwa imani kuwa viungo vyao vinaleta utajiri. Ni kweli?” Nilipatwa na mchanganyiko wa aibu na hasira. Aibu kwa sababu nchi yangu inaonekana kuwa na viumbe wa ajabu kabisa wanaomudu kudiriki unyama huo. Pia nilipatwa na hasira kwa sababu ni ukweli usiopingika kuwa laana ya mauaji ya albino limeachwa kustawi kana kwamba uhai wa Watanzania wenzetu maalbino hauna thamani.
Wiki iliyopita, vyombo vya habari huko nyumbani viliripoti kuhusu tukio la kusikitisha ambapo maiti ya mtoto albino, Yohana Bahati, aliyetekwa tarehe 15 mwezi huu, uliokotwa ukiwa umekatwa miguu na mikono. Taarifa ya mauaji ya kinyama ya mtoto huyo asiye na hatia yoyote imesambaa sehemu mbalimbali duniani huku vyombo vya habari vya kimataifa vikiipa uzito mkubwa. Aibu gani hii kwa nchi inayojigamba kuwa ni ‘kisiwa cha amani na utulivu’ huku ikitumia mabilioni ya shilingi katika kampeni za kimataifa kutangaza vivutio vyetu? Kwa bahati nzuri, Watanzania wengi hususan kwenye mitandao ya kijamii wameonekana kuguswa mno na unyama huu kiasi cha kupelekea kampeni ya ‘Stop Albino Killings.’ Katikati ya wiki iliyopita, kampeni hiyo ilivuma katika mtandao wa kijamii wa Twitter hadi kufanikiwa kufikisha ‘impressions’ zaidi ya milioni moja.
Tupigeni vita ukatili wa aina hii kwa nguvu zote. Albino nao wanastahili sio tu kuishi, bali kuwa na viungo vyao kamili walivyojaaliwa na Mungu

Tupigeni vita ukatili wa aina hii kwa nguvu zote. Albino nao wanastahili sio tu kuishi, bali kuwa na viungo vyao kamili walivyojaaliwa na Mungu.

Cha kusikitisha, hadi wakati ninaandika makala hii, Rais Jakaya Kikwete ambaye akaunti yake ya Twitter imerejea hewani baada ya kupotea kwa siku kadhaa, ameshindwa kujumuika na Watanzania lukuki pamoja na watu wengine duniani, kuunga mkono kampeni hiyo. Na kana kwamba ni chama anachoongoza Rais Kikwete, CCM, kimeona suala hilo ni mzaha flani wa kupuuzwa, licha ya kutounga mkono kampeni hiyo, Jumapili iliyopita kiliweka bandiko katika mtandao huo kikijigamba kuwa, ninanukuu, “Tumeendelea kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kulinda amani na utulivu…” Haya ni matusi. Amani na utulivu gani ilhali Watanzania wenzetu albino wanachinjwa kinyama zaidi ya kuku (maana tunapochinja kuku hatumkati mikono, mguu au kucha zake hadi muda wa matayarisho ya kumpika)?
Kadhalika, katika hali inayoweza kutafsiriwa kama serikali yetu kupuuza mauaji ya albino , hakuna kiongozi yeyote wa ngazi za juu wa serikali aliyeona umuhimu wa kushiriki katika mazishi ya mtoto Yohana. Siku alipozikwa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikwenda kuhani msiba wa chifu mmoja huko Iringa. Hivi hata tukiweka kando protokali, serikali ilishindwa kumtumia japo Waziri mmoja kumwakilisha Rais Kikwete? Binafsi, pamoja na nyingi ya ‘tweets’ zangu wiki iliyopita za kuhamasisha kampeni hiyo inayoandikwa #StopAlbinoKillings, pia nilitanabaisha kuwa mauaji hayo ya albino ni zaidi ya suala la kisheria bali la kibinadamu. Nilisema hivyo kwa sababu, kwa upande mmoja, sheria dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu na za mauaji zipo lakini hazijatumika ipasavyo kukabiliana na tatizo hilo, na kwa upande mwingine, hata pale sheria zinapofanya kazi ipasavyo, hazimaanishi kuwa zitamaliza kabisa uhalifu flani. Hata hivyo, sheria zikitumika ipasavyo huwezi japo kwa kiasi flani kukwaza uhalifu (deterrence).
Wakati matukio ya mauaji ya kinyama ya albino yakiendelea huko nyumbani, mwezi uliopita serikali ilipiga marufuku waganga wa kienyeji sambamba na kupiga marufuku wapiga ramli wote ambao wanaelezwa kuchangia mauaji ya watu hao wenye ulemavu wa ngozi. Haihitaji ujuzi wa kuchambua matamko ya serikali kumaizi kuwa amri hiyo ilikuwa ni porojo kama zilivyo porojo nyingine kuhusu ufisadi, ujangili, madawa ya kulevya, nk. Lakini pia ni muhimu kujiuliza, kwanini mauaji ya albino yamekuwa yakiongezeka kila tunapokaribia uchaguzi mkuu. Katika mazingira ya kawaida tu ni rahisi kutambua kuwa baadhi ya wanasiasa wetu ni wateja wa waganga wa kienyeji wanaotoa masharti ya kupatiwa viungo vya albino ili ‘kuwasafishia mambo’ wanasiasa hao.
Picha za wanawake mbalimbali wa kialbino kutoka Tanzania walivyofanyiwa mahojiano na gazeti la Huffingon Post.

Picha za wanawake mbalimbali wa kialbino kutoka Tanzania walivyofanyiwa mahojiano na gazeti la Huffingon Post.

Na katika suala hilo linalohusiana na ushirikina, nina mifano miwili hai. Nina ndugu yangu kiukoo ambaye ni mganga huko wilayani Kilombero. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, mmoja wa wagombea urais alilala katika makazi ya mganga huyo ili ‘kutengenezwa’ kwa ajili ya uchaguzi huo. Kadhalika, wakati huohuo, mmoja wa watendaji wakuu wa taasisi moja nyeti alikumbwa na kashfa ya kuajiri waganga wa kienyeji ili wamsaidie kupata ukurugenzi mkuu. Japo hakufanikiwa katika azma yake hiyo, mtendaji huyo kwa sasa ni mwakilishi wetu katika nchi moja jirani. Mifano hiyo hai inaonyesha ni kwa jinsi gani imani za kishirikina zilivyoota mzizi katika Tanzania yetu. Na suala la ushirikina si kwa wanasisasa au ‘vigogo’ wengine pekee kwani wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam, kwa mfano, wanafahamu kuhusu misururu ya magari inayoelekea Mlingotini hasa mwishoni mwa wiki katika kinachoaminika kwenda kutafuta huduma za waganga wa kienyeji.
Nilipokuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilisoma Sosholojia ya Dini ambapo pamoja na mambo mengine tulifundishwa kuhusu imani za asili. Kimsingi, kabla ya ujio wa ‘dini za kimapokeo’ yaani Uislam na Ukristo, ‘dini’ kuu ilikuwa imani za asili. Takriban kila jamii ilikuwa na wataalamu wa tiba, ambao kwa mazingira ya sasa ni sawa na waganga wa asili. Uji0 wa dini za kimapokeo haukufanikiwa kuondoa imani za asili, lakini ‘kwa bahati mbaya’, wakati utabibu wa asili zama hizo ulilenga katika kutatua ya mtu binafsi, ‘mabadiliko’ katika fani hiyo yalipelekea ‘matibabu’ hayo kujumuisha kudhuru watu wengine. Kwa mujibu wa maelezo ya ndugu yangu anayejishughulisha na uganga wa jadi huko wilayani Kilombero, kuna waganga wanaozingatia ‘asili ya fani hiyo’ ambao kamwe hawakubali kufanya tiba za kumdhuru mtu. Hata hivyo, alinieleza kuwa kutokana na ukosefu wa maadili, tamaa na ugumu wa maisha, idadi kubwa ya waganga sio tu ‘wanadhuru walengwa’ bali pia hutumia dawa zinazotokana na madhara kwa binadamu, kwa mfano viungo kama hivyo vya albino.
Albino
Tufanyeje? Ni vigumu kupata ufumbuzi mwepesi kwa tatizo hili kubwa. Amri ya serikali kupiga marufuku waganga wa kienyeji na ramli ni ya kipuuzi, kwa sababu kama serikali hiyohiyo inashindwa kuwadhibiti mafisadi wanaokwapua mabilioni sehemu kama Benki Kuu penye CCTVs lukuki itawezaje kuwabana waganga na wapiga ramli wanaofanya shughuli zao kwa siri? Binafsi, kama nilivyobainisha awali, ufumbuzi wa tatizo la mauaji ya albino ni wapaswa kuwa wa kibinadamu (humanity) zaidi kuliko kisheria (legislative). Wanunuzi wa viungo vya albino twaishi nao katika jamii zetu, kama ilivyo kwa wahalifu wanaiwinda na kuuwa ndugu zetu hao. Kadhalika, waganga wanaotumia viungo vya binadamu twaishi nao katika jamii zetu. Kinachohitajika ni kuweka mbele ubinadamu wetu ili kuwadhibiti maharamia hao.
Japo serikali ina jukumu la msingi la kuhakikisha usalama wa raia wake, na Katiba yetu inasisitiza umuhimu wa haki ya kuishi, sote twafahamu kuhusu uzembe wake katika masuala yanayohusu ‘wanyonge.’ Mazingira tu wanayoishi watawala wetu ni kinga tosha kwao na jamaa zao kudhuriwa na wanaiwinda viungo vya binadamu. Na taarifa kwamba baadhi ya wanasiasa na ‘vigogo’ wengine ni wateja wa waganga wanaohitaji viungo vya albino zinafanya utegemezi kwa serikali kuwa ‘kazi bure.’ Nimalizie kwa kuhamasisha wakazi wa jiji la Dar kujitokeza kwa wingi katika maandamano yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni kulaani mauaji ya albino na kushinikiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Sambamba na hilo, ninashauri maandamano hayo yafanyike nchi nzima ili kufikisha ujumbe kuwa hatuwezi kuvumilia mateso na mauaji kwa ndugu zetu albino. Na kwa Watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii, ninawasihi waendelee kutumia ‘hashtag’ #StopAlbinoKillings angalau mara moja kwa siku.
#StopAlbinoKillings (Zuwia Mauaji ya Albino) – See more at: http://www.raiamwema.co.tz/mauaji-haya-ya-albino-mpaka-lini#sthash.QJnt84fX.dpuf
Chanzo: Raia Mwema
Picha: Kutoka Mtandaoni