Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, amesema serikali itaanza kutekeleza mkakati wa kulinda thamani ya Shilingi ya Tanzania ambayo imekuwa ikiporomoka thamani yake.
Dk. Mgimwa amesema kuwa alisema Wizara yake inakuja na mkakati mpya wa kuhakikisha kwamba matumizi yote ya fedha na mahitaji ya nchi yanafanyika kwa Shilingi ya za Tanzania badala ya Dola ya Marekani ili kuliepusha taifa kuendelea kuathiriwa na kushuka kwa thamani ya fedha yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Waziri Mgimwa, ambaye aliteuliwa hivi karibuni kushika wizara hiyo akichukua nafasi ya Mustafa Mkulo, alisema kuwa mpango wa kuirejesha Shilingi ya Tanzania katika thamani yake, unatokana na mfumo mpya ulioigwa kutoka katika mataifa ya Italia, Ugiriki, Ireland na Ureno ambazo zimeamua kuondoa fedha zake kutoka katika matumizi ya Euro na kuhamishia akiba yake kwenda katika Dola ya Marekani.
“Ili kuepuka kuendelea na adha hii, tunapaswa kuhimiza zaidi matumizi yote na mahitaji ya nchi, yafanyike kwa Shilingi ya kitanzania badala ya Dola.
Tayari katika hili, Benki Kuu (BoT) imezipa matumaini taasisi za fedha na mabenki kupunguza kiwango kilichokuwa kimeruhusiwa kuweka akiba (deposit) ya fedha za kigeni kutoka asilimia 20 hadi kufikia asilimia 10.”
Alisema kupitia mkakati huo, serikali itajikita katika kuuza wa bidhaa nyingi nje ya nchi kuliko uagizaji.
Pia alisema serikali itawashauri wawekezaji waliopo nchini na wanaokuja kutumia fedha za kitanzania badala ya dola ili kuimarisha Shilingi.
MFUMUKO WA BEI
Dk. William Mgimwa, amesema tatizo la mfumuko wa bei na kupaa kwa gharama za maisha kunakoligharimu taifa kwa sasa, kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na serikali kuchelewa kutoa fedha za ununuzi wa chakula cha akiba katika maghala ya taifa.
Alisema kuwa matokeo hayo yana tafsiri moja kwa moja udhaifu huo kama ndio kichocheo cha mfumuko wa bei, ambao umesababisha kuadimika kwa baadhi ya vyakula sokoni kutokana na usambazaji wake mdogo tofauti na mahitaji ya nchi.
Akizungumzia mfumuko wa bei za vyakula hasa mchele, mahindi na maharage ambavyo vimesababisha wananchi wa kipato cha chini hususani vijijini na mijini kushindwa kumudu bei yake, alisema hali hiyo inatokana na mahitaji makubwa ya nafaka katika maeneo miji mikubwa.
“Taifa limetumbukia katika mfumuko wa bei kwa sababu serikali huko nyuma ilichelewesha kupeleka fedha kwenda kwenye maeneo yenye maghala ya taifa yanayonunua chakula, kitendo ambacho kimepelekea baadhi ya vyakula kuwa adimu kutokana na usambazaji kuwa mdogo na hivyo kutomudu mahitaji ya nchi.
Mikoa tegemeo kwa uzalishaji wa chakula hasa ile inayojulikana kama The Big Four Region, iliathiriwa na ubovu wa miundo mbinu ya barabara,” alisema.
Awali, akijibu hoja za baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani, wanaodai kwamba nchi imefilisika na iko taabani kiuchumi, Dk. Mgimwa alisema kuwa kauli hizo hazina mashiko kwa kuwa taifa lina akiba ya kutosha ya Dola za Marekani bilioni 3.6 ambazo zinakidhi mahitaji ya nchi kwa muda wa miezi minne ijayo.
“Jamani nchi iko salama, tunayo akiba ya Dola bilioni 3.6 fedha ambayo inatutosha kwa miezi minne ijayo na kwa taarifa yao waelezeni (hao wanasiasa) kwamba taifa linao uwezo wa kukopa na kuhudumia mikopo yote kwa mujibu wa vigezo vya Benki ya Dunia na IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa)…Sasa wanaosema nchi imefilisika, hatuwezi kulumbana nao badala yake sisi tunachapa kazi,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Mgimwa, Wizara yake inaangilia mambo makubwa matatu ambayo ni kuhakikisha nchi inakopesheka na kuwa na uwezo wa kuhudumia mikopo yake, akiba ya kutosha ya fedha za kigeni nauwezo wa kuingiza ndani na kusafirisha bidhaa zake nje ya nchi.
CHANZO: NIPASHE