Matumaini Katiba Mpya Arijojo…!

Mwenyekiti Bunge la Katiba, Samuel Sitta

Mwenyekiti Bunge la Katiba, Samuel Sitta


IKULU imeeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014. Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue alilieleza gazeti hili kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa, wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu kupatikana Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.

“Kweli matarajio ya awali yalikuwa hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine, ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya,” alieleza Balozi Sefue.

Katika hali isiyoeleweka Balozi Sefue alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa Serikali kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.

Alisema muda huo wa kupatikana Katiba Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini ambao aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.

Dk. Slaa alisema walipendekeza kwamba badala ya kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15 Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu ujao kwa lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba Mpya.

“Lakini walitukebehi na kututukana sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za mchana,” alieleza Dk. Slaa.

Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali kuna watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba. Alisema ana taarifa za Bunge Maalumu kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.

“Kwa akili ya kawaida tu isiyohitaji elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi siyo watoto wadogo,” alieleza Dk. Slaa.

Kauli ya LHRC
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema siyo tu Serikali imeshindwa kutimiza ahadi ya muda iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.

Dk. Bisimba alisema kwa hali ilivyo, hawana hakika ya kupata Katiba na ikipatikana haitakidhi matakwa ya wananchi, kwa kuwa wanataka Katiba ya watu siyo ya kundi moja la watu.

“Mambo ya nchi hii tunayafahamu, inaweza ikapatikana kwa nguvu lakini wajue wananchi wataikataa na hata ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza kuathiri ustawi wa taifa,” alieleza Dk. Bisimba.

Alisema hilo waliliona mapema, wakataka kila hatua ya mchakato ipewe muda wa kutosha kabla ya hatua nyingine, ili wananchi waelimishwe lakini hawakusikilizwa.

Alisema kuwa katika mazingira hayohayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi kubwa hadi kufanikisha maoni ya wananchi kupatikana na kutengeneza Rasimu ya kwanza na ya pili iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014, lakini kwa jinsi Bunge Maalumu linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba kazi hiyo itaharibiwa.

“Wakichezea Rasimu wajue wanachezea maoni ya wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia kura ya maoni na hivyo kusababishia taifa hasara isiyomithilika,” alieleza Dk. Bisimba.

Dk. Bisimba alisema mchakato huo umegharimu taifa fedha nyingi, muda mwingi, nguvu, akili, afya na hata uhai wa watu, hautakiwi kufanyiwa mzaha.

Alipotafutwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala hilo jana hakupatikana, lakini Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo ni dhahiri haiwezekani kupata Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na ilivyodhaniwa awali.

Hata hivyo, Kairuki alisema hawezi kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel Sitta.

“Hata hivyo tunachotakiwa kuzungumzia ni ubora wa kazi inayofanyika ili kufikia lengo la kupata Katiba itakayoongoza nchi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Kairuki.

CHANZO: Mwananchi