Matokeo Kidato cha Nne: Wanafunzi 789 Wafutiwa Matokeo, 126,847 Wafaulu

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa

Na Joachim Mushi

MATOKEO ya Mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2012 yametoka huku Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikilazimika kufuta matokeo ya wanafunzi 789 baada ya kufanya udanganyifu kwenye vyumba vya mitihani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizarani ambayo pia mtandao huu umeipata jumla ya watahiniwa wa shule 126,847 kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya mtihani huo wa Kidato cha Nne 2012 wamefaulu, huku wasichana wakiwa 46,161 na wavulana ni 80,686.

Taarifa inaonesha kuwa wafulana ndiyo waliofanya vizuri zaidi katika kiwango cha ufaulu wa jumla kwani kati ya watahiniwa 23,520 waliofaulu kwa madaraja I – III, idadi ya wavulana ni 16,342 huku wasichana wakiwa 7,178 tu. Pia jumla ya wavulana 1,073 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza huku idadi ya wasichana waliopata daraja hilo ikiwa ni 568.

Wavulana 4,456, wamefaulu kwa daraja la pili huku wasichana waliopata daraja hilo pia kufikia 1,997. Kama hiyo haitoshi kati ya watahiniwa 15,426 waliopata daraja la tatu idadi ya wavulana ni 10,813, huku ile ya wasichana ikiwa ni 4,613. Jumla ya watahiniwa 240,903 wamefeli mtihani huo kwa kupata daraja sifuri.

Taarifa zaidi zinabainisha kuwa jumla ya watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo yao yote ya mtihani kwa mujibu wa kifungu Na. 52(b) cha Kanuni za Mitihani baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika mitihani hiyo iliyofanyika Oktoba 2012.

Miongoni mwa makosa ya udanganyifu ambayo watahiniwa hao walibainika nayo ni pamoja na watahiniwa kubainika kuwa na skripti zenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika skripti ya somo moja au zaidi ya moja. Watahiniwa kukamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mtihani wakiwa na ‘notes’ na wengine kukamatwa ndani ya chumba cha mtihani wakiwa na ‘notes.’

Mengine ni kukamatwa wakiwafanyia watahiniwa wengine mtihani ‘impersonation”. Watahiniwa kukamatwa na wasimamizi wakibadilisha karatasi za maswali au skripti kwa lengo la kufanya udanganyifu. Kati ya idadi hiyo watahiniwa wa shule ni 624 na watahiniwa wa kujitegemea ni 148 na wale wa mtihani wa Maarifa (QT) wakiwa jumla ya 17.

Hata hivyo, idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani hiyo ni 16,112 kati ya watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani- huku wasichana waliofaulu ni 6,751 na wavulana ni 9,361.

Taarifa zaidi imesema kuwa watahiniwa 28,582 wa Shule ambao hawajalipa ada ya Mtihani hadi watakapolipa ada wanayodaiwa pamoja na faini; na ikiwa hawatalipa katika kipindi cha miaka miwili (02) toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.
Wizara imesema shule kumi zilizoshika kumi bora kwa ufaulu ni pamoja na ST. FRANCIS GIRLS-MBEYA, MARIAN BOYS S.S-PWANI, FEZA BOYS S.S-DAR ES SALAAM, MARIAN GIRLS S.S-PWANI, ROSMINI S S-TANGA, CANOSSA S.S-DAR ES SALAAM, JUDE MOSHONO S S-ARUSHA, ST. MARY’S MAZINDE JUU-TANGA, ANWARITE GIRLS S S-KILIMANJARO NA KIFUNGILO GIRLS S S-TANGA.

Aidha shule 1o zilizoshika mkia ni pamoja na MIBUYUNI S.S- LINDI, NDAME S.S- UNGUJA, MAMNDIMKONGO S.S- PWANI, CHITEKETE S.S – MTWARA, MAENDELEO S.S- DAR ES SALAAM, KWAMNDOLWA S.S- TANGA, UNGULU S.S- MOROGORO, KIKALE S.S- PWANI, NKUMBA S.S- TANGA pamoja na TONGONI S.S- TANGA.
Kundi la watahiniwa ambao huandika matusi limeendelea kushamiri katika matokeo ya mwaka huu pia, kwani jumla ya watahiniwa 24 wamefutiwa matokeo yao baada ya kuandika matusi Katika Skripti Zao na wizara inajiandaa kuwachukulia hatua kwani kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa kifungu 5(13) cha Kanuni za Mitihani kinachosomeka.

“Written responses to any examination question which carry words, drawings or pictures connected to sex or abusive language in such a way that it becomes offensive shall consitute an examination offence and a candidate who commits such an offence shall be punished by the Council.”

“Kutokana na kosa hilo Baraza la Mitihani limefuta matokeo yao yote kwa mujibu wa Kifungu cha 6(2)(a) cha Kanuni za Mitihani kinachosomeka: “A candidate found to have committed an examination offence shall – (a) have his examination results nullified”.
“Kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu (skripti) kinaonesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Serikali haitaweza kuwavumilia hata kidogo watahiniwa wa aina hiyo. Hivyo, Serikali itaangalia hatua zaidi za kisheria za kuchukua dhidi ya watahiniwa wote walioandika matusi. Kati yao, watahiniwa wa shule ni 624 na watahiniwa wa kujitegema ni 148 na watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa (QT) ni 17.
“Kwa mujibu wa kifungu Na. 6(2)(b) cha Kanuni za Mitihani, watahiniwa wote waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani au kuandika matusi katika skripti zao hawataruhusiwa kufanya mitihani inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja (01) kuanzia tarehe ya kutangazwa kwa matokeo.
Watahiniwa 28,582 wa Shule ambao hawajalipa ada ya mtihani wamezuiliwa matokeo yao hadi watakapolipa ada wanayodaiwa pamoja na faini; na ikiwa hawatalipa katika kipindi cha miaka miwili (02) toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.
Kundi hili ni pamoja na watahiniwa 65 wa kujitegemea na 71 waliofanya Mtihani wa Maarifa (QT) mwaka 2012 bila ya kulipa ada ya Mtihani hadi watakapolipa ada pamoja na faini. Ikiwa hawatalipa ada hiyo katika kipindi cha miaka miwili (02) toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.
Matokeo hayo pia yanapatikana katika mitandao ya :- www.matokeo.necta.go.tz, • www.necta.go.tz, www.udsm.edu.ac.tz, au www.moe.go.tz