Matokeo Darasa la Saba Yatoka, Wasichana Wang’ara

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa

• Ufaulu waongezeka kwa asilimia 8.8

WASICHANA nchini wameng’ara katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, baada ya kuongoza kwa asilimia 50.20 na kuwapita wavulana waliopata asilimia 49.80.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, alitangaza matokeo hayo jana wizarani kwake na kusema kuwa wanafunzi 560,706 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.

Alisema, kati ya wanafunzi hao wasichana waliochaguliwa ni 281,460, huku wavulana wakiwa 279,246, na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa awamu ya kwanza 2011.

Kawambwa alisema, mtihani huo uliofanyika Septemba 19 na 20, kwa mara ya kwanza ulitumia teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ ambapo mitihani ilisahihishwa kwa kutumia kompyuta.

Alisema utumiaji wa teknolojia hiyo mpya umeipunguzia serikali gharama kwa kuwa mwaka jana walimu 4000 walitumia zaidi ya mwezi mmoja kusahihisha mitihani hiyo nchi nzima, lakini kwa mwaka huu walimu 285 tu ndio waliotumika kwa siku 15 kukamilisha usahihishaji huo.

“Matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonyesha kuwa alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana. Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 3087 walipata alama za daraja la A, wakati wanafunzi 40,683 walipata daraja la B.

“Jumla ya wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja la C na 526,397 walipata alama za daraja la D. Waliobaki 73,264 walipata alama E,” alisema Kawambwa.

Hata hivyo, waziri huyo katika maelezo yake, hakuweza kutaja mikoa iliyofanya vema na ile iliyoshika nafasi ya mwisho. Kadhalika Waziri Kawamba hakuweza kutoa nafasi ya kutosha kwa waandishi kuuliza maswali kwa kile alichodai kuwa na haraka ya majukumu mengine ya kitaifa.

Akizungumzia udanganyifu katika mtihani alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema waliofutiwa matokeo 2012 ni watahiniwa 293 tu ikilinganishwa na watahiniwa 9736 waliofutiwa matokeo kwa undanganyifu mwaka jana.

“Kufuatia udanganyifu huo, serikali itawabaini wale wote waliohusika katika udanganyifu huo na kuwachukulia hatua stahiki,” alisema.

kuhusu tatizo lililojitokeza mwaka jana la wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika, serikali imeanzisha mpango mpya wa kuwachuja wanafunzi hao kwa kufanya mtihani mwingine kabla ya kuanza kidato cha kwanza.

Alisema, serikali inafanya hivyo ili kujihakikishia haitarudia kosa la kuwapeleka wanafunzi wa aina hiyo sekondari, bali endapo watabainika watafutiwa usajili na kupelekwa kwenye mfumo wa kujifunza kusoma na kuandika.

Wanafunzi 894,839 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wa kumaliza darasa la saba, wengine 29,012 sawa na asilimia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu za utoro, vifo na ugonjwa.

CHANZO: http://www.freemedia.co.tz