Mataifa ya Ulaya Yasitisha Misaada Rwanda

Rais wa Rwanda, Paul Kagame

MUUNGANO wa Nchi za Ulaya umeamua kusitisha misaada kwa nchi ya Rwanda baada ya kutoridhishwa na tabia zake. Uamuzi huo umefikiwa baada ya ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja huo iliyodai kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 dhidi ya Serikali ya Congo DRC.

Taarifa zaidi zinasema waasi hao wanadhibiti kimabavu sehemu kubwa ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na hata kuwatoza kodi wananchi. Kundi hilo lilianza uasi katika eneo hilo Aprili kitendo ambacho kimesababisha takriban raia laki tano wa DRC kukimbia eneo hilo wakihofia usalama.

Hata hivyo, Rwanda imeendelea kukana madai hayo. Umoja wa Mataifa unafanya mkutano na baadhi ya yatakayopewa kipaombele kwenye mkutano huo ni swala la mgogoro huo Mashariki mwa Congo. Mapema mwezi Julai Marekani ilizuia dola 200,000 zilizokusudiwa kulisaidia jeshi la Rwanda.

Msaada wenyewe uliokatwa siyo mkubwa kwa Jeshi la Rwanda, lakini hatua hiyo ilitoa ishara kubwa. Kwa kukata msaada huo, Marekani ni kama ilikuwa inasema “tunaamini ripoti kuwa Rwanda inatibua usalama wa kanda hiyo kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa Congo”.

Mwezi Juni, Umoja wa Mataifa ulikabidhi ripoti kwa Baraza la Usalama, ambayo ilisema ina ushahidi mzito kuwa Rwanda inalipatia kundi la M23, wapiganaji na zana, na kurahisisha makamanda wao wakubwa kusafiri na kuvuka mpaka baina ya Congo na Rwanda. Uasi huo ulianza mwezi wa Aprili, wakati wanajeshi kadha wa Jeshi la Congo walipofanya ghasia.

Uasi huo uliongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye anasakwa na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, kwa uhalifu wa kivita. Nayo Serikali ya Uholanzi ilisitisha msaada wa dola milioni 6.15 kwa Rwanda baada ya nchi hiyo kuhusishwa na madai hayo ingawa baadaye ilianza tena kutoa msaada kwa nchi hiyo baada ya Serikali ya Rwanda kuahidi kushirikiana na kukomesha vita.

-BBC