Na Mwandishi Wetu
MASHIRIKA 25 kutoka Tanzania Bara ambayo yanaendesha kampeni za kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, watoto na makundi mengine yaliyoko pembezoni yatapatiwa stadi za kutambua habari na nini cha kufanya vyombo vya habari viweze kutangaza habari hizo.
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, Ananilea Nkya. Akifafanua Nkya amesema lengo la mafunzo hayo ni kuyawezesha mashirika kutimiza wajibu wake kuviwezesha vyombo vya habari kutangaza habari zitakazoweza kuhamashisha viongozi wa serikali, taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kijamii na wananchi wanawake na wanaume kuchukua hatua kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Alisema mafunzo hayo yameandaliwa kama sehemu ya shughuli za kuadhimisha siku 16 za kampeni ya kimataifa inayoendeshwa kila mwaka duniani kote kupinga ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto ambapo kwa hapa nchini mwaka huu kauli mbiu inasema “Miaka 50 ya uhuru: Pinga ukatili wa kijinsia kuimarisha Tanzania huru”.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kuanzia saa nne na nusu asubuhi Novemba 28, 2011 yameandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya idadi ya watu (UNFPA) kama sehemu ya shughuli za pamoja za Umoja wa Mataifa,” alisema Nkya.
Alisema TAMWA imeandaa mafunzo hayo kwa kuwa inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na changamoto za vyombo hivyo kupata habari.
Aidha TAMWA inatambua kuwa mashirika mengi ya kijamii yakiwemo yale yanayoendesha kampeni dhidi ya ukatili wa kijinsia hayakusanyi taarifa zinazotokana na kazi zao na kusambaza kwa vyombo vya habari hivyo umma kupata habari zinazogusa roho ili kila mtu achukie ukatili na kuchukua hatua kuzuia vitendo hivyo viovu.
Hata hivyo aliongeza kuwa vitendo vya ukatili vilivyoshamiri hapa nchini ni pamoja na ubakaji unaosababisha mimba miongoni mwa wasichana mashuleni na maambukizi vya Virusi Vya UKIMWI (VVU) kwa wanawake wenye umri mdogo.
Aliongeza vitendo vingine ni watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 18 kuozeshwa kwa nguvu ili familia zipate mahari, waume kupiga wake zao, kurithi wajane, mauaji ya Albino na matusi ya kumdhalilisha mwanamke ambayo hutolewa hadharani ikiwa ni pamoja na kwenye mabasi.
Katika miaka ya hivi karibuni ukatili wa kijinsia umetambulika kimataifa kama moja ya vikwazo vya maendeleo na hivyo mataifa yameanza kufanya kampeni kubwa za kimkakati kuelimisha watu madhara ya ukatili kwa maendeleo ya mtu binafsi, familia na taifa.
Kwa hapa Tanzania vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vimekuwa ndicho chanzo kikubwa cha kuvunjia ndoa, ongezeko la maambukizi ya virusi vya UKIMWI ndani ya ndoa na wimbi la watoto kuishi mitaani.
Aidha imethibitika wazi kuwa familia zinazoishi kwa amani bila vitendo vya ukatili zimeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa haraka na wazazi, baba na mama kuweza kuishi maisha marefu.
Utafiti wa Kitaifa (DHS) wa mwaka 2010 unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 39 ya wanawake hapa nchini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili tangu wakiwa na umri wa miaka 15 na hivyo kuwapunguzia uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na pia kuwaweka katika hatari kupata magonjwa ukiwepo UKIMWI na shinikizo la damu.