HATIMAYE mashine aina ya Magnetic Reasonance Imaging (MRI) iliyokuwa imesimama kwa muda wa miezi miwili kiasi cha kuleta kero kwa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili leo imeanza kufanyakazi kama kawaida ikiwa ni siku tatu tangu Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli afanye ziara ya kushtukiza hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema mashine hiyo imeanza kazi leo baada ya mafundi wa kampuni ya Phillips kuifanyia matengenezo tangu mchana.
MRI ni mashine inayopiga picha za uchunguzi kwa mgonjwa kwa ubora zaidi kwa kutumia sumaku badala ya mionzi na picha zake zinaubora zaidi ya zile zinazopigwa na mashine ya CT-Scan. Aligaesha aliongeza kuwa jitiada za kuitengeneza tena mashine nyingine ya CT-Scan ambazo kwa pamoja zilikuwa zimeharibika zinaendelea na taarifa zaidi itatolewa kwa wananchi.
Rais Dk. Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza na kushuhudia mashine hizo mbili zikiwa hazifanyi kazi kwa zaidi ya miezi miwili jambo ambalo lilimsikitisha na kumpa maelekezo Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ambaye alilazimika kufanya mabadiliko ya kumuondoa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Hussein L. Kidanto na kumteuwa Prof. Lawrence Mseru kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili.
Baada ya ziara hiyo, Wizara ya Fedha ilitoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini. Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).