Mashindano Kombe la Taifa Yasonga, Amavubi Kutua Mwanza…!

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
MICHUANO ya Kombe la Taifa kwa Wanawake inaingia raundi ya pili kesho (Januari 17 mwaka huu) kwa mechi za kwanza za raundi hiyo zitakazochezwa katika miji ya Bukoba, Arusha, Mlandizi, Dar es Salaam na Katavi.
 
Jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi mbili ambapo mkoa wa kisoka wa Ilala utacheza na Mtwara kwenye Uwanja wa Karume, wakati Uwanja wa Chuo cha Bandari uliopo Tandika utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Temeke na Dodoma.
 
Mechi nyingine za michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin zitakuwa kati ya Kagera na Mwanza itakayochezwa mjini Bukoba, Arusha na Tanga (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid), Pwani na Kinondoni (Uwanja Mabatini, Mlandizi), na Katavi na Mbeya zitakazoonesha kazi kwenye Uwanja wa Azimio.
 
Nazo Ruvuma na Iringa zitacheza Januari 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji. Mechi hiyo itachezwa tarehe hiyo ili kusubiri matokeo ya mechi ya marudiano kati ya Shinyanga na Simiyu.
 
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Januari 15 mwaka huu) kupitia ripoti ya mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza kati ya Shinyanga na Simiyu ambayo ilivunjwa na mwamuzi katika daika ya 70.
 
Baada ya kupitia ripoti, Kamati imebaini kuwa licha ya vurugu alizofanyiwa mwamuzi, bado mechi hiyo ingeweza kuendelea kwa kuchezeshwa na mwamuzi wa akiba kwa vile usalama ulikuwepo baada ya yeye kupigwa.
 
Pia Kamati imeagiza Katiba wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo aliyeripotiwa kumpiga mwamuzi suala lake lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa hatua zaidi, wakati Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye naye alishiriki kumpiga mwamuzi amesimamishwa wakati akisubiri kuchukua hatua zaidi. Kamishna wa mechi hiyo Idd Mbwana, na mwamuzi Joseph Pombe wamefungiwa kwa miaka miwili.
 
Mechi kati ya Shinyanga na Simiyu itamaliziwa dakika kumi zilizobaki kesho (Januari 17 mwaka huu) mjini Shinyanga. Kila chama cha mkoa kitabeba gharama zake katika uendeshaji wa mechi hiyo ambayo mwenyeji ni Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
 
Timu itakayosonga mbele baada ya mechi hiyo itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili ugenini Januari 19 mwaka huu dhidi ya Kigoma. Mechi za marudiano za raundi ya pili zitachezwa kati ya Januari 21 na 22 mwaka huu.
 
Hatua ya robo fainali hadi fainali ambayo mechi zake zitachezewa jijini Dar es Salaam itaanza Januari 26 mwaka huu. Fainali itachezwa Februari Mosi mwaka huu.
 
Vilevile Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF imemfungia kwa miaka miwili Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kwa kushindwa kuingiza timu yake uwanjani kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza dhidi ya Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
 
AMAVUBI KUTUA MWANZA JANUARI 21
Timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) inawasili Mwanza, Januari 21 mwaka huu kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Taifa Stars Maboresho itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo.
 
Amavubi yenye msafara wa watu 26, wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itawasili kwa ndege ya RwandAir na siku hiyo hiyo jioni itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya JB Belmont.
 
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaingia kambini keshokutwa (Januari 18 mwaka huu), na siku inayofuata itakwenda Mwanza tayari kwa ajili ya mechi hiyo itakayofanyika Januari 22 mwaka huu.
 
Kikosi hicho cha Kocha Mart Nooij ambacho ni sehemu ya maandalizi ya mechi za mchujo za michuano ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) kinaundwa na wachezaji 26.
 
MAREKEBISHO YA MECHI ZA VIPORO VPL
Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) imeingizwa mechi za viporo zilizotokana na timu za Azam, Mtibwa Sugar na Simba kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 iliyomalizika wiki hii kisiwani Zanzibar.
 
Vilevile mechi za viporo zimeingizwa kwa kuzingatia ushiriki wa timu za Azam kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika (CL) na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho (CC) pamoja na mechi za kirafiki za Taifa Stars.
 
Yanga itacheza na BDF ya Botswana kwenye mchezo utakaofanyika Februari 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa wakati Azam itaikabili El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex, Februari 15 mwaka huu.
 
Mechi za viporo itakuwa kama ifuatavyo; Januari 20- Kagera Sugar na Azam (Mwanza), Januari 28- Simba na Mbeya City (Dar es Salaam), Februari 4- Coastal Union na Yanga (Tanga), Februari 11- Azam na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam) na Februari 11- Mgambo Shooting na Simba (Tanga).
 
Februari 11- Yanga na Ndanda (Dar es Salaam), Februari 21- Mbeya City na Yanga (Mbeya), Februari 25- Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons (Morogoro), Februari 28- Simba na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam), Machi 4- Ruvu Shooting na Azam (Pwani), na Machi 4- JKT Ruvu na Yanga (Dar es Salaam).
 
Machi 4- Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro (Morogoro), Machi 8- Simba na Yanga (Dar es Salaam), Machi 11 Azam na Mbeya City (Dar es Salaam), Machi 11- Yanga na Kagera Sugar (Dar es Salaam), Machi 18- Azam na Ndanda (Dar es Salaam), Machi 18- Yanga na Stand United (Dar es Salaam), Aprili 8- Simba na Tanzania Prisons (Dar es Salaam).
 
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)