Masheikh Wampongeza Sitta Bunge la Katiba

Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akikabidhi kitabu kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta (kulia), kinachoitwa ‘Kilele cha Fasaha’ kinachohusu maadili na uongozi.

Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akikabidhi kitabu kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta (kulia), kinachoitwa ‘Kilele cha Fasaha’ kinachohusu maadili na uongozi.

Sheikh Hemed Jalala (kushoto) akiongoza dua ya kuiombea Bunge Maalum la Katiba. Kulia ni Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta na katikati ni Mjumbe wa Bunge hilo, Yassmin Alloo. (Picha zote na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma)

Na Magreth Kinabo, Dodoma

BAADHI ya viongozi wa dini wamempongeza Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta kwa kitendo chake cha kuliendesha Bunge hilo vizuri katika hali ya utulivu na amani.

Kauli hiyo imetolewa leo na Sheikh Hemed Jalala kutoka Msikiti wa Ghadiir uliopo maeneo ya Kigogo Post jijini Dar es Salaam, ambaye aliambatana na Masheikh wengine ambao ni Alhaji Mohamed Mputa, Sheikh Mohamed Abdi na Masoud Mbilili.

Aidha Sheikh Jalala akizungumza kwaniaba ya viongozi wenzake wa dini alisema kuwa wamekuja kutembelea Bungeni hapo kwa ajili ya kumshukuru, Sitta na kumuunga mkono kwa kazi nzito nzuri anayoifanya huku akisisitiza kuwa wako nyuma yake katika suala hilo.

“Pamoja na changamoto zilizojitokeza umeweza kukabiliananazo vizuri. Sisi na wananchi kila tunapolifuatilia tunaona mmeweza kulipeleka vizuri. Jambo hili ni zito linahitaji amani, utulivu na kuvumiliana,” alisema Sheikh Jalala.

Sheikh Jalala alisema wao kama viongozi wa dini, wameona kuna changamoto ya maadili hivyo, wameandaa kitabu maalum kinachoitwa ‘Kilele cha Fasaha’.

Alisema kitabu hicho kitasaidia kutoa mchango wao kwenye masuala ya uongozi na maadili, ambacho alikikabidhi kwa Sitta. Akipokea kitabu hicho, Sitta amesema ni jambo la baraka kwake, ambapo aliahidi kutoa taarifa juu ya jambo hilo na kukikabidhi kitabu hiko katika Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo.

Sheikh Jalala alisema kuna jumla ya nakala 632 ya vitabu hivyo na vimeshakabidhiwa kwenye ofisi ya Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Katika hatua nyingine Sheikh Jalala ameongoza dua maalum kwa ajili ya kuliombea Bunge hilo ili liweze kuendelea kwa amani, utulivu, busara, maelewano na upendo.