Maria: Mume Wangu Aliiongopea Mahakama Ikavunja Ndoa Yetu
Nkasi, Rukwa
NOVEMBA 18, 2013 Mahakama ya mwanzo, Namanyere, Wilaya ya Nkasi iliamua kuvunja ndoa ya Ndebile Kazuri na Bi. Maria Tarafa wote wakazi wa Kijiji cha Isale Mji mdogo wa Namanyere wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa. Ndoa hiyo ambayo hadi mahakama inaivunja ilikuwa na watoto wanne, yaani watoto wawili wakiwa na miaka 9 na 7 huku wengine wawili wakiwa na miaka 3 na mwingine mwaka mmoja.
Mume ndiye aliyeenda mahakamani kufungua kesi akiomba kutengana na mkewe akidai anatabia mbaya hivyo hawezi kuendelea kuishi naye. Kazuri anaomba mahakama itengue ndoa hiyo akiwa tayari na mke mwingine ambaye anaishi naye tofauti na Bi. Tarafa.
Bi. Tarafa anasema shauri hilo lilifunguliwa Oktoba 22, 2013 na Novemba 18 mahakama baada ya kuridhika na sababu zilizotolewa na mlalamikaji na bila kumpa nafasi ya kujieleza mlalamikiwa iliamua kuvunja ndoa hiyo. Bi. Tarafa katika mahojiano na mwandishi wa makala haya alipotembelea Wilaya ya Nkasi kwa msaada wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA); anasema sababu zilizotolewa na mumewe mahakamani kuomba ndoa ivunjwe si za kweli japokuwa mahakama iliridhika na kuamua kuvunja ndoa yao na kuwagawa watoto.
Anasema chanzo cha mumewe kuamua kuvunja ndoa hiyo ni pamoja na yeyé kudai mahitaji yake na familia yao kwa mumewe ambaye kipindi hicho alikuwa tayari amemtelekeza bila huduma hizo huku akiishi na mwanamke mwingine aliyezaa naye pia.
“…Hadi anafungua kesi hiyo kuomba ndoa itenguliwe alikuwa tayari amenitelekeza maana alikuwa hatoi chochote kwangu licha ya kuwa naishi na watoto wake, alikuwa hanihudumii hata nikiumwa nilikuwa nikiishi kwa kutegemea kilimo mimi pamoja na watoto wangu…alinitelekeza kihuduma tangu Oktoba 2012.”
“…Hata mazao ambayo yalipatikana baada ya mimi kulima na wanangu nayo alikuwa akiyasimamia yeyé na wakati mwingine kumnufaisha zaidi mke mwenzangu na familia yake zaidi yangu mimi ambaye ndiye niliteseka kiuzalishaji,” anasema Bi. Tarafa katika mazungumzo.
Anasema mbali na unyanyasaji huo pia alikuwa akipigwa sana na mumewe mara kwa mara kwa sababu zisizokuwa na msingi. “…Kuna wakati nilikuwa mjamzito wa miezi nane alinipiga hadi nikaenda kulazwa aliniumiza sana kiuno pamoja na shingo, lakini mbali na kuniumiza kiasi hicho aligoma kabisa kunipeleka hospital ili niweze kutibiwa. Walilazimika kuja wazazi wangu ambao walinipeleka hospitali na kulazwa. Baada ya mimi kulazwa yeyé alikamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka kutokana na kitendo alichokifanya,” anasema Bi. Tarafa.
Anabainisha kuwa baada ya kumuomba sana mke wake aliingiwa na huruma na kufuta kesi ili waende wakayazungumze kinyumbani na wazee wa pande zote ili kutafuta suluhu, hivyo aliridhia na kufuta kesi hiyo. Kikao cha wazee kilimuamuru kulipa gharama na muda kwa wazazi wangu ambao walilazimika kusafiri kutoka kijijini kwao na kuacha shughuli zao na kuja kuniuguza mimi zaidi ya wiki moja hadi hali ilipokuwa nzuri.
Pamoja na hali hiyo mateso kihuduma kwangu yaliendelea alikuwa hatoi chochote kutoka kwa mkewe mwingine anayeishi naye kuja kwangu kwa ajili ya wanae. Wakati mwingine aliwafukuza wanangu kukanyaga kwa mkewe huyo mwingine, licha ya watoto hao kuwa wakimsaidia kazi nyingine. Anasema mtoto wangu mmoja ndiye aliyekuwa akichunga ngombe ambazo ambazo zinainufaisha zaidi familia ya mke mwenzake, lakini wao hawapati hata maziwa ya ng’ombe wanapokamuliwa.
“Nilivumilia nikachoka siku moja nikamfuata na kumwambia kama ataendelea kuwatenga wanangu ki-huduma hata mifugo ambayo wao ndio wachungaji basi nitawazuia kuchunga ng’ombe hizo maana zinawanufaisha wao pamoja na mke mwenzangu lakini sio mimi na watoto wangu ambao ndio wachungaji.
Hapa napo alinipiga sana na kudai kwanini ninawazuia watoto wangu kuchunga ng’ombe za baba yao, alisema watoto lazima wachunge maana watakapotaka kuoa ukubwani watatumia ng’ombe hizo kama mahari hivyo siwezi kuwazuia…mgogoro uliendelea. Ndipo nilipoamua kumshtaki kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isale ‘A’, anasema.
Bi. Tarafa anasema hata siku anaenda kujifungua mtoto wa nne ambaye ni wa mwisho kuzaa na Kazuri alilazimika kuwafungia watoto wake ndani usiku na kwenda hospitali mwenyewe. “…Nilipoanza kuhisi uchungu nilituma watoto wakamjulishe kuwa hali yangu ni mbaya hivyo naitaji msaada nipelekwe hospitali, aligoma kabisa kuja, majirani wakamfuata tena wao akagoma ndipo walipokuja mama na kaka yangu na kunipeleka wao hadi hospitalini nikajifungua salama mtoto wake wa nne,” anasema.
Baada ya kujifungua manyanyaso yaliendelea alifikia hatua ya kunitaka mimi na watoto wake niondoke pale kwake na niende kuishi kwa wazazi wangu eti akidai atakuwa akinihudumia kulekule. Mimi nilikataa nikamwambia siwezi kuondoka na mzigo wa watoto na kwenda nao nyumbani kwetu.
Anabainisha kuwa Novemba 18, 2013 baada ya mvutano na yeye kukiri kuwa yupo tayari kuachana na mume huyo iwapo atapata haki zake na watoto, mahakama ilivunja ndoa hiyo na kuamuru aondoke na watoto wawili bila kueleza namna watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.
Alisema mahakama iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na yeye kuondoka na wawili wenye miaka miaka chini ya saba. Aliongeza kuwa Mahakama iliamuru apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo tulilima pamoja na bati 7.
“…Mume wangu alidanganya kuwa hatuna mali pale mahakamani, mimi nikaeleza ni uongo kwani tuna ng’ombe zaidi ya 127, buzi 30, nyumba mbili pale kijijini Isale pamoja na hekari zaidi ya 70 za ardhi…hawakunisikiliza pale mahakamani. Ukweli ni kwamba tunamali hizo ambazo tulichuma tukiwa wote,” alisema Bi. Tarafa.
Mwandishi wa habari hii amebahatika kupata nakala ya hukumu ya kesi hiyo, ambayo kweli haikuonesha namna watoto wanaobaki kwa mama watahudumiwaje na baba yao licha ya kuamuru kuwa watabaki na mamayao.
Hata hivyo akizungumzia mvutano huo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, Ramadhan Rugemalira anasema mama huyo anahaki ya kufungua kesi nyingine ya madai kuomba mgawanyo wa mali na matunzo kwa watoto endapo hakuridhika na hukumu iliyotolewa kwa shauri hilo.
“…Anachotakiwa kuomba mahakamani kwa sasa ni mgawanyo wa mali, kwamba katika kesi yao ambayo mahakama ilivunja kuna mali ambazo mahakama haikuzizungumzia kabisaa lakini na mimi (mke) ninahaki na mali hizo, unaona…ataleta ushahidi kama ng’ombe hao wapo kama kuna ardí na nini…hivyo huyo mwanaume ataitwa na kesi kusikilizwa,” anafafanua Rugemalira.
Hata hivyo, Hakimu Rugemalira anasema huenda mtoa hukumu wa mwanzo aliteleza kwa kitendo cha kutoainisha namna watoto wanaobaki kwa mama watalelewa vipi na baba (kihuduma). Anasema pamoja na hayo bado mama huyo anahaki ya kufungua madai mengine kudai haki hizo.
Anasema Bi. Tarafa anaweza kufungua kesi ya madai kudai matunzo ya watoto pamoja na mali ambazo mahakama haikuzizungumzia kabisha wakati wa kesi ya msingi ya kuvunja ndoa yao. Anaongeza kuwa au mama huyo anaweza kukata rufaa mahakama ya wilaya kupinga hukumu ya awali kwamba hakuridhika na kitendo cha mahakama kumpa watoto bila ya kueleza namna ya watakavyo pata gharama za matunzo toka kwa baba.
“…Anaweza kuleta shauri mahakamani akilalamika kwamba katika ndoa yetu iliyovunjwa kuna mali ambazo mahakama haikuongelea kabisa, na mali hizi katika kuzichuma na mimi ninauhusika, basi ataleta ushahidi mahakamani kuthibitisha uwepo wa mali hizo na walichuma wote kisha mahakama itamwita huyo mwanaume na kesi kusikilizwa ikiridhika basi mali hizo zitagawanywa,” anasema hakimu Rugemalira.
Mwandishi wa makala haya alizungumza na Kazuri aliyekuwa mume wa mama huyo kujua anazungumziaje juu ya mali ambazo mkewe anazilalamikia, yaani ng’ombe 127, nyumba 2, mbuzi 30 na ardhi hekari 70. Katika majibu yake anasema mali hizo zinazolalamikiwa alipewa na babayake mzazi amshikie wakati anaanza maisha hivyo bado ni mali ya babayake ambaye alidai yupo hadi sasa.
Pamoja na madai hayo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini baba yake na Kazuri (kwa jina Kazuri Moshi) ni marehemu na alifariki dunia tangu mwezi Machi 2004 na mali zake kugawiwa kwa watoto wake wote wenye haki ya kupata akiwemo Kazuri mwenyewe.
Hata hivyo mtalaka wake Kazuri akifafanua zaidi juu ya mali anazolalamikia; anasema walipewa ng’ombe 65 za urithi toka kwa baba yake na Kazuri, lakini wamezizalisha hadi kufikia ng’ombe zaidi ya 127. Aidha anabainisha licha ya mifugo hiyo wanamiliki mashamba na nyumba mbili lakini anashangaa mzazi mwenzake anamdhulumu zote.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye, akizungumzia sakata hilo anakiri kumfikia. Anasema Bi. Tarafa alifika katika ofisi yake akilalamika kutoridhika na uamuzi wa mahakama. Alilazimika kutembelea familia hiyo zaidi ya mara moja Kijijini Isale na kufanya mazungumzo ya kina na pande zote.
Anasema kwa maoni yake baada ya kuchunguza amegundua kuna utata juu ya sababu zilizotolewa mahakamani hadi kuvunjwa ndoa hiyo. Anasema kwa kuzingatia sheria nyingi kama Sheria ya Mtoto (2009), Sheria ya Ndoa (1971), Sheria ya Kanuni za Adhabu (1937) na zinginezo; pamoja na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na kusainiwa na taifa ni vyema kila mtu, kwa nafasi yake mzazi/mlezi, mahakama, polisi, na maofisa Ustawi wa Jamii pamoja na vyombo vingine kuona Ustawi na maendeleo ya mtoto ni jambo muhimu.
Anabainisha kuwa; Sheria ya Ndoa (1971) fungu 113 (2), inaeleza uwezo wa Mahakama kutengua/kubadili amri yake ya kutengana iwapo itatosheka kwamba amri hiyo ilitokana na maelezo ya kupotosha au yasiyo na ukweli.
“…Mahakama inaweza kuangalia upya taarifa ya sababu za kuachana (wizi na kiburi) ambazo Kazuri aliwasilisha mahakamani kwa kuwa zinaonesha hazina ukweli na zinahitaji ushahidi na uhuru wa kujitetea. Kwa kufanya hivyo mahakama itakuwa imempa Tarafa fulsa ya kufungua kesi ya madai na hivyo kupata mstakabali wa ustawi wa watoto wote wanne,” anasema Mdenye.
Kiongozi huyo wa ustawi wa jamii anasema; alivyofuatilia kwa kina mzozo huo amebaini Kazuri alimpa mimba mtalaka wake akiwa darasa la sita 2003/2004, hivyo kumpotezea fulsa ya kusoma, lakini leo anamwacha solemba (mtelekeza na watoto) kirahisi tu bila kukumbuka makosa yake ya nyuma.
“Kikubwa zaidi Sheria ya Ndoa (1971), kifungu 114 kinaeleza uwezo wa mahakama kutoa amri ya kugawana mali za waliooana. Mahakama itazingatia masilahi ya watoto, na itatazama usawa katika ugawaji. Pia kifungu 136 (1) kinaeleza uwezo wa Mahakama kuzingatia nasaha za maofisa wa ustawi na wengineo husika.”
Anabainisha kuwa Kazuri hajafanya hivyo badala yake amebomoa hata nyumba ya vyumba viwili aliyokuwa akiishi mtalaka wake na watoto na alipoulizwa kwa nini anafanya ukatili huo alijibu amebomoa ili mkewe na watoto waende kuishi kwa bibi yao yaani mama mkwe wake.
Kimsingi nashauri sote tuache mawazo mgando kama ya Kazuri ambaye anazungumza kwa kujiamini kana kwamba ni jambo jema. Nina mengi ya kusema juu ya mzozo huu ambao Kazuri anaonekana kukosa utu, lakini sina uwezo wa kupinga amri ya mahakama. Tuiachie kwa kuwa ndio chombo cha mwisho cha uamuzi kwa tatizo hili,” anasema Mdenye.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA