Marekani Yatamba Kufanikiwa Mapigano na Islamic State

Wapiganaji wa kundi la Isamic State.

Wapiganaji wa kundi la Isamic State.

MKUU wa majeshi ya Marekani Generali Jack Dempsey amesema kampeni ya miezi mitatu dhidi ya dola ya kiislamu ‘Islamic State’ imekuwa na mafanikio, lakini akaeleza wazi kuwa kwa oparesheni hiyo Marekani na washirika wake walikabiliana na vikwazo kwa muda mrefu.

Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Chuck Hagel aliliambia Bunge la Congress kuwa dola ya kiislamu imedhibitiwa na haiwezi kusonga mbele na maeneo mengine imesambaratishwa japo wanaonekana kuendeleza ushawishi kwenye ukanda wa Iraq na Syria.

Mkuu wa kikosi cha majeshi ya Marekani Generali Jack Dempsey anakadiria idadi ya wanamgambo wa dola ya kiislam kufikia 31,000. Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya kundi hilo, ambapo pia limekuwa likitoa ushauri na mafunzo kwenye majeshi kwa majeshi ya Marekani.

Wakati huo huo, dola ya Kiislam Islamic State imesambaza sauti iliyorekodiwa wanayodai ya Kiongozi wao. Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Marekani dhidi ya wapiganaji wa dola ya Kiislam ambapo ilidaiwa yalimuua au kumjeruhi vibaya kiongozi wao Abu Bakr Al Baghdadi.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Marekani amesema hawezi kuthibitisha ukweli wa sauti hiyo ambayo imeweka kumbukumbu na matukio yaliyotokea tangu siku ya kwanza ya mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya dola ya kiislam.

Kumbukumbu hizo ni pamoja na Tangazo la Rais Barack Obama la kuongeza wanajeshi zaidi nchini Iraq na ahadi mpya kwa wapiganaji kuwaunga mkono wapiganaji kutoka Libya, Yemen, na Misri.