Marekani Yaimwagia Lawama Misri na Falme za Kiarabu

Libya militia

MAOFISA nchini Marekani wamesema mataifa ya Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu zilihusika na mashambulio nchini Libya wiki iliyopita kuwalenga wanamgambo wa Kiislamu wanaopambana na vikosi vya Serikali.
Ofisa mmoja Mkuu wa Marekani aliwaambia wanahabari kuwa Marekani haikushirikishwa katika mashambulio hayo na ilishangazwa. Makombora hayo yaliofyetuliwa Tripoli yanasemekana kutekelezwa na Umoja wa milki za kiarabu kwa kutumia kambi za kijeshi nchini Misri.

Misiri imekana tuhuma hizo na halijatoka tamko lolote kutoka kwa Umoja wa falme za kiarabu hadi sasa. Marekani na washirika wake wanne wa Ulaya zimeshutumu wanachokitaja kama usumbufu wa kutoka nje nchini Libya. Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza na Marekani zimelaani vikali mpigano na ghasia nchini Libya.

Zimelaani pia kuongezeka kwa mapigano na ghasia ndani na kuzunguka miji ya Tripoli, Benghazi, na nchini kote Libya, hususan dhidi ya maeneo ya maakazi ya watu, sehemu za umma, na miundombinu muhimu kutokana na mashambulio ya ardhini na pia ya angani.

Nchi hizo zimesema zinarudia wito wao, zikiungana na ule wa serikali ya muda ya Libya, Baraza la Wawakilishi na wananchi wa Libya, kwamba pande zote nchini Libya zikubaliane na usitishaji wa vita mara moja na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa, kujizuia na mipango inayoweza kudhoofisha hatua hiyo.
-BBC