MAREKANI na Urusi Septemba 14, 2013 wamefikia makubaliano ya kihistoria baada ya mazungumzo ya siku tatu juu ya mpango mkubwa wa kutokomeza silaha za sumu za Syria kufikia katikati ya mwaka ujao wa 2014.
Kulingana na makubaliano hayo mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani yamempa Rais Bashar al Assad wa Syria wiki moja kuwasilisha maelezo juu ya silaha za sumu zilizolimbikizwa na utawala wake.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry amesema utawala wa Assad lazima utowe nafasi mara moja kwa wakaguzi kutoka Shirika Lenye Kupiga Marufuku Silaha za Sumu (OPCM) kuziona silaha hizo.
Kerry ameuambia mkutano wa waandishi wa habari wa pamoja na waziri mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kwamba wakaguzi hao wanapaswa kuwa huko kabla ya mwezi wa Novemba na lengo ni kuanza kuondowa silaha hizo kuelekea mwakani.
Akirudia onyo kutoka kwa Rais Barack Obama kwamba hatua za kijeshi zitachukuliwa na Marekani na washirika wake iwapo diplomasia itashindwa kufanya kazi, Kerry ameonya kwamba hakupaswi “kuwepo mchezo na chochote kile ziada ya utawala wa Assad kutii kikamilifu uwondoaji wa silaha hizo.”
Makubaliano kujumuishwa kwenye azimio la Umoja Mataifa
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wakipongezana mjini Geneva. Kerry amesema hatua zilizokubaliwa Jumamosi zitajumuishwa katika azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakalotayarishwa chini ya kifungu nambari saba cha katiba ya umoja huo ambacho kinazungumzia uwekaji wa vikwazo na uwezekano wa matumizi ya nguvu za kijeshi.
Lakini kutokana na Urusi kupinga vikali vitisho vya matumizi ya kijeshi na ikiwa na uwezo wa kura ya turufu katika Baraza la Usalama, Kerry amekiri kwamba ilikuwa haiwezekani kufikiwa makubaliano ya mapema juu ya kile kitakachotokea iwapo Syria itashindwa kutii azimio hilo.
Lavrov amedokeza kwamba serikali ya Urusi itaunga mkono aina fulani ya vikwazo kwa kusema kwamba Baraza la Usalama litachukuwa hatua chini ya Kifungu nambari Saba iwapo Syria itashindwa kutimiza masharti yake.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva. Kerry amesema vita vya maafa vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambayo vimesababisha zaidi ya vifo 110,000 katika kipindi cha miaka miwili na nusu vitaweza tu kukomeshwa kwa kupitia mazungumzo.
Huo unaonekana kuwa ni uungaji mkono mwengine kwa upinzani wa Urusi kwa aina yoyote ya uingiliaji kati kijeshi na unaweza kutafsiriwa kama Marekani inaachana na msimamo wake kuwapatia msaada waasi kuwasaidia kumn’gowa madarakani Assad.
Kerry amekaririwa akisema ” hakuna ufumbuzi wa kijeshi kwa mzozo nchini Syria na unabidi uwe wa kidiplomasia na tunahidi kuendelea kuishirikiana kufanikisha hilo.”
Lavrov ameyapongeza makubaliano hayo kama ni makubaliano mazuri kabisa ambapo umuhimu wake ni vigumu kukadiria kupindukia.
Makubaliano hayo yamepokelewa kwa fadhaa na muungano wa upinzani wa Syria ambao umetumia miaka miwili kuyaomba mataifa ya magharibi kuwapatia silaha wanazohitaji kuupa nguvu katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.Generali Selim Idriss mkuu wa Jeshi Huru la Syria amewaambia waandishi wa habari mjini Istanbul kwamba”Hawawezi kukubali sehemu yoyote ile ya mpango huo.”
Amesema inamaanisha kwamba “Wao Wasyria wanatakiwa wasubiri hadi kati kati ya mwaka 2014, waendelee kuuwawa kila siku na kukubali makubaliano hayo kwa sababu tu silaha za sumu zitaangamizwa hapo mwaka 2014.”
Mapambano nchini Syria kwenyewe yanazidi kupamba moto ambapo waasi na vikosi vya serikali wako katika mapigano makali ya kutaka kuudhibiti mji wa kale wa Kikrito wa Maalula ulioko karibu na Damascus.
Serikali ya Marekani na Urusi zinataraji kufufuwa mipango ya mazungumzo ya amani huko Geneva ambayo yataukutanisha utawala wa Assad na upinzani katika kufikia makubaliano juu ya kipindi cha mpito cha kisiasa kukomesha vita hivyo ambavyo vimezuka hapo mwezi wa Machi mwaka 2011.
Kerry na Lavrov watakutana tena wiki chache zijazo pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kwa matumaini ya kupanga tarehe ya mkutano huo wa amani uliokwama.
Tangazo la ghafla la Urusi kwamba Syria iko tayari kukabidhi silaha zake za sumu limemfanya Obama kusitisha mashambulizi ya kijeshi ambayo Marekani na Ufaransa yalitishia kufanya dhidi ya Syria kutokana na shambulio la silaha za sumu lililofanyika hapo mwezi wa Augusti karibu na Damascus ambalo Marekani inaulaumu utawala wa Syria kwa kuhusika nalo na kusema limeuwa takriban watu 1,400.
-DW