Marehemu Willy Edward azikwa Morotonga Mugumu

Ndugu wa marehemu Willy Edward wakilia wakati wakipokea jeneza lake lilipowasili kijijini kwao

Na Mwandishi Wetu, Morotonga Mugumu

MWILI wa aliyekuwa mwanahabari na Mhariri Mkuu wa Gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Ogunde amezikwa jana jioni (majira ya saa tisa) kijijini kwao Morotonga Mugumu, wilayani Serengeti katika Mkoa wa Mara.

Marehemu Edward Ogunde amezikwa kijijini hapa eneo la makaburi ya familia yao Morotonga baada ya ibada ya maziko iliyoanza majira ya saa tano asubuhi, huku ikiongozwa na maaskofu Hilikia Omindo (Dayosisi ya Mara) pamoja na John Adiema (kutoka Dayosisi ya Rorya) wote kutoka Kanisa la Anglikana.

Wanahabari na waombolezaji anuai juzi jijini Dar es Salaam walishiriki kuuaga mwili Edward Ogunde kabla ya kusafirishwa kuelekea wilayani Serengeti kwa shughuli za maziko.

Umati huo wa waombolezaji ukiongozwa na viongozi kadhaa wa vyama vya siasa na wamiliki wa vyombo vya habari ulikusanyika jijini Dar es Salaa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo ndipo ilipofanyika ibada ya kumuombea marehemu Ogunde kabla ya kutoa heshima zao za mwisho kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Upande wa wamiliki wa vyombo vya habari uliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi huku vyama vya upinzani vikiwakilishwa na Mwenyekiti wa CUF, Taifa Prof. Ibrahim Lipumba na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwakilishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mengi alisema vifo vya wanahabari vimekuwa vikiwaathiri wamiliki wa vyombo vya habari kwa kiasi kikubwa pamoja na wadau wengine wa tasnia hiyo, hivyo kuwatia moyo waombolezaji kuendelea kumuombea marehemu Willy Ogunde. Kwa upande wake Prof. Lipumba alisema tasnia ya siasa imepoteza mtu muhimu ambaye ndiye mpigania demokrasia kwenye ushindani wa kisiasa.

“Vyombo vya habari ni muhimu katika ushindani wa kisiasa hasa kidemokrasia…kupoteza mwanahabari kwa njia yoyote tunaathirika wanasiasa…lakini njia pekee ya kumuenzi marehemu Willy ni kuendeleza yale yote mema ambayo alikuwa akiyaamini na kuyasimamia,” alisema Prof. Lipumba.

Marehemu alifariki dunia ghafla mjini Morogoro baada ya kuanguka usiku nyumbani kwa ndugu yake, alipokuwa amekwenda kuwasalimu watoto wake ambao huishi hapo. Marehemu Edward alikuwa mjini Morogoro akihudhuria semina ya wanahabari iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini.

‘Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Willy Edward Ogunde,’