Na Mwandishi Wetu
MPIGANAJI mwanahabari na Mhariri Mkuu wa Gazeti la Jambo Leo hatunaye tena duniani. Wille Edward amefariki usiku wa kuamkia leo akiwa mjini Morogoro alipokuwa akihudhuria semina ya sensa ya watu na makazi iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu ulizipata mapema asubuhi ya leo kutoka mjini Morogoro na kuthibitishwa na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Wille Edward amefariki majira ya saa sita usiku wa kuamkia Jumapili akipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kuanguka ghafla akiwa hotelini.
Tayari mwili wa marehemu Edward umesafirishwa leo kuelekea jijini Dar es salaam kwa taratibu za awali kabla ya kusafirishwa kuelekea kijijini kwao kwa mazishi Jumatano ya wiki hii. Msiba kwa sasa unafanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam alipokuwa akiishi kabla ya kukubwa na mauti hayo.
Marehemu Edward atabaki akikumbukwa kutokana na msimamo wake thabiti katika kazi ya uandishi wa habari kwa kile kusimamia haki muda wote, ikiwa ni pamoja na kukiendeleza na kuikuza lugha ya Taifa (kiswahili) hasa katika matumizi ya misamihati ya maneno ya lugha hiyo katika uandishi wake, hivyo kuwa na mvuto.
Mtandao wa dev.kisakuzi.com utakuwa ni mmoja wawaathirika wakubwa wa mauti ya Edward kwani alikuwa akifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na mtandao huu, ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa muhimu za kijamii jambo ambalo lilikuwa kiungo kikubwa kitaaluma. Uongozi, wafanyakazi na wadau wa dev.kisakuzi.com unatoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wa marehemu hasa katika kipindi hiki cha majozi.
Bwana alitoa na sasa ametwaa hivyo jina lake lihimidiwea. Amina.