Marais watatu wakutana kuijadili Somalia

Ramani ikionesha mataifa ya Kenya na Somalia

MARAIS watatu wa Afrika Mashariki wamekutana katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi kuonesha umoja wao juu ya harakati za Kenya za kijeshi nchini Somalia.

Mkutano huo kati ya rais wa Kenya, Mwai Kibaki, Yoweri Museveni wa Uganda na Sheikh Sharif Sheikh Ahmed wa Somalia unafanyika ikiwa ni mwezi mmoja baada ya harakati hizo kuanza kuwasaka wanamgambo wa kundi la kiislamu la Al Shabaab.

Katika taarifa ya pamoja waliyoitoa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya saa tatu, marais hao wameelezea umuhimu wa kujumuisha harakati za majeshi ya Kenya, majeshi ya Serikali ya mpito ya Somalia na yale ya muunguno wa Afrika (AMISOM).

Marais hao pia walielezea wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa wakimbizi wa Kisomali nchini Kenya. Wametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuanzisha juhudi za kupunguzia Kenya kibarua cha kuhifadhi wakimbizi. Kupitia taarifa hiyo ya pamoja wamependekeza kuwa mashirika ya misaada yaliyoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya, yaanze kuhamishia shughuli zao kusini mwa Somalia.

Mbali na Uganda na Burundi ambazo zimepeleka wanajeshi wake nchini Somalia, nchi nyingine inayotarajiwa kupeleka wanajeshi Somalia ni Djibouti. Djibouti inatarajiwa kupeleka wanajeshi wake Somalia, mwezi ujao. Hii ni mara ya Kwanza kwa rais Sheikh Sharif kuzuru Kenya tangu kuanza kwa harakazi za kijeshi za kuwasaka wanamgambo wa kundi la alshabab.

Harakati hizo za kijeshi zilianza baada ya visa vya kuwateka waheni vilivyodaiwa kutekelezwa na Al Shabaab. Mkutano huu unajiri siku moja baada ya nchi za Afrika zinazochangia wanajeshi nchini Somalia kukutana mjini Addis Adada.