Mapinduzi ya Kitekinolojia Katika Sekta ya Afya

Dk. Reddy Telemedicine

Dk. Reddy Telemedicine


KATIKA muongo uliopita sekta ya afya imeshuhudia mabadiliko fulani ya ajabu katika maendeleo ya kiteknolojia na uvumbuzi ambao umeleta mchango mkubwa katika utoaji wa ushauri na matibabu kwa wagonjwa. Mapinduzi hayo yamesaidia kuboresha utoaji huduma za afya na matokeo mazuri kwa wagonjwa. Maendeleo ya kiteknolojia yamepindua sekta ya huduma za afya kwa njia nyingi na kuleta njia za kisasa na bora zaidi za matibabu; Ukuaji wa technolojia umesaidia sana katika upatikanaji wa data na pia katika kuwezesha shughuli mbalimbali zinazohusiana na matibabu, kwa ujumla imeleta faida nyingi sana katika sekta ya afya.

Teknolojia ile ambayo mara kwa mara hutumika kwa ajili ya mitandao ya kijamii na shughuli nyingine za kibiashara sasa inatumiwa na wataalamu wa afya ili kuleta manufaa zaidi katika afya ya binadamu. Kuenea kwa maendeleo ya teknolojia na kupanuka kwa matumizi yake katika huduma za afya zimechangia si tu kuunganisha madaktari kwa madaktari wenzao lakini pia kutoa jukwaa kwa ajili ya madaktari kuungana na wagonjwa wao.

Kuwepo kwa huduma kama vile ya telemedicine imewapa madaktari uwezo wa kufanya kazi bila mipaka. Kwa kitendo cha kubonyeza kifufe mara moja tu madaktari wana uwezo wa kutoa na kupata utaalamu na utambuzi kutoka kwa madaktari wenzao au kutoa huduma kwa wagonjwa waliopo katika maeneo yaliyopo mbali zaidi.

Kulingana na utafiti wa hivi karibuni wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ina uwiano wa 1:30,000 wa daktari na idadi ya watu, ikimaanisha kuwa kila watu laki tatu wanahudumiwa na dakitari mmoja. Kutokana na ukuaji wa haraka wa idadi ya watu nchini kwa ujumla uwiano huo hauja badilika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Takwimu hiyo ipo mbali sana na uwiano uliopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) wa daktari maalumu mmoja kwa kila watu 1,000. Kutokana na uhaba huo unaojionyesha, ufumbuzi ni kuongeza idadi ya madaktari katika maeneo mbalimbali ya nchi. Na jambo hili linaonekana kama litakuwa mkakati wa mda mrefu nchini, ufumbuzi wa haraka itakuwa kutumia teknolojia kama vile telemedicine katika maeneo hayo. Kwa kufanya hivyo itaruhusu maeneo ya mbali zaidi kama vile vijijini kuwa na upatikanaji wa mtaalamu katika hospitali atakayetoa ushauri na matibabu katika hosipitali na kliniki hizo bila kusafiri mamia ya maili.

Tekinolojia ya Telemedicine bado ni changa nchini Tanzania, na ina nafasi kubwa ya kujifunza kutoka kwa nchi nyingine duniani kote. India ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa na uwezo na mafanikio makubwa katika kutumia teknolojia ya telemedicine katika utoaji wa matibabu nchini na kwingineko duniani. Taasisi kubwa kama vile hosipitali za Apollo wa Hospitali zimefanikiwa sana katika technolojia hii nchini India. Technolojia hii imetumika katika maeneo ya mijini na vijijini. Kwa hospitali za Apollo zilizopo majimbo mbalimbali nchini India ikiwa ni pamoja na Bangalore, Hyderabad na Delhi teknolojia hii inawapa fursa wataalamu wa afya kupata habari kwa urahisi na kujadili kesi za wagonjwa mbalimbali katika muda huohuo kama watu waliopo eneo moja.

Wakati wa mkutano wa siku mbili wa Telemedicine uliofanyika Septemba mwaka huu mjini Bagamoyo ulioandaliwa na wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Universal Communications Service Access Fund (UCSAF).

Waziri wa Sayansi na Teknolojia Prof Makame Mbarawa alionyesha matatizo mbalimbali yanayowakabili sekta ya afya nchini na pia alielezea umuhimu wa kukumbatia teknolojia ili kukabiliana na changamoto zilizopo. Alisema kuwa kwa sasa nchi ina watu binafsi na wataalam “ambao wanapaswa kuwa sehemu ya mapinduzi katika sekta ya afya”.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr Seif Rashid akitoa mchango wakati wa mkutano huo alitoa wito wa kujifunza kutoka kwa hosipitali na taasisi zenye uzoefu zaidi alielezea juu ya ” kwenda nje ya mipaka yetu kuanzisha ushirikiano mzuri na hospitali kubwa za kigeni”

Apollo hospitali, taasisi inayotazamia kufungua kituo cha afya nchini Tanzania itasaidia sana katika sekta ya matibabu nchini. Ikiwa na uzoefu wa miaka mingi katika kutumia zana za kisasa kwa kushirikiana na hospitali ndani ya nchi itasaidia sana kwenye kutoa huduma bora zaidi ya matibabu kwa watu wote.
Hospitali hii imekuwa na mafanikio makubwa katika tekinolojia ya telemedicine kupitia mtandao wa Apollo Telemedicine Network Foundation, mtandao huu umesaidia sana katika kutoa matibabu maeneo yaliyopo mbali zaidi na pia kutoa njia mbadala si tu kwa wagonjwa lakini pia kwa madaktari ambao kwa sababu moja au nyingine upatikanaji wa huduma ya afya ni changamoto.
Maono ya Apollo kama ilivyoelezwa Mwanzilishi na Mwenyekiti wa hosipitali hiyo Dk.Prathap C. Reddy “ni kutoa afya ya viwango vya kimataifa kwa kila mtu”.
Dk Reddy anaongeza kuwa, technolojia ya Telemedicine ni njia ya gharama nafuu kwa ajili ya kupitia upya na kufuatilia kesi za wagonjwa waliokwenda kutibiwa na hosipital ya Apollo kutoka sehemu zote duniani.
Kupitia huduma hii hospitali imekuwa na uwezo na imefanikiwa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 1,00,000 kupitia vituo mbalimbali vya telemedicine vilivoanzishwa na Mtandao wa Apollo Telemedicine ujulikanao kama Apollo Telemedicine Network Foundation. Hospitali ya Apollo inatumia programu ya mtandao iitwayo Medeintegra, ambayo ni njia ya kielectroniki inayoweza kutunza kumbukumbu kwa urahisi zaidi maarufu kama EMR (Electronic Medical Record). Njia hii ina uwezo wa kusambaza na kuhifadhi electrocardiograms (ECGs), X-ray, tomografia [CT] scans, picha za ultrasound, MRI na taarifa za matibabu mengine. Uwezo wa programu hii ya Telemedicine inaruhusu madaktari nchini India kutoa tiba na ushauri kwa wagonjwa na pia kutoa msaada wa kitaalamu kwa madaktari waliopo mbali kwa kama nchini Tanzania.

Prof. K. Ganapathy, Kiungo muhimu katika teknolojia ya Telemedicine na Muasisi wa Apollo Telemedicine, amenukuliwa akisema kwamba kupitia tekinolojia hii tuna uwezo wa “Kufanya Jiografia kuwa historia,” “kufanya umbali kutokuwa na maana,” na kurahisisha gharama za upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila mtu, wakati wowote, mahali popote.”
Kwa jinsi teknolojia inavyoendelea kutafsiri upya utoaji wa huduma za afya, Tanzania inatakiwa kuanza matumizi ya telemedicine kwa kiwango kikubwa. Kwa kutumia teknolojia hii upatikanaji na utoaji wa huduma maalumu za matibabu utakuwa rahisi kwa wananchi wote.

Madaktari bingwa waliopo katika hospitali muhimu na kubwa kama vile Muhimbili au KCMC wana uwezo wa kubofya kitufe mara moja tu na kuhudumia wagonjwa au kutoa msaada wa kitaalamu kwa madakitari wenzao waliopo katika maeneo ya mbali zaidi hasa vijijini. Endapo tekinolojia hii itatumika kwa uyakinifu inatarajiwa kusaidia kuondoa vikwazo mbali na kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu ambazo hazipatikazi maeneo yaliyo mbali zaidi.