Mapigano Mapya Yazuka Congo

Mapigano Mapya Yazuka Congo

MAPIGANO mapya yamezuka Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kati ya wanajeshi wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na waasi wa M23,na kuwalazimisha watu kukimbia makaazi yao. Tarifa kutoka eneo la tukio zinasema kumekuwa na mapigano makali ya silaha kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini, Goma.

Watu wapato 50,000 hawana mahali pa kuishi tangu mwezi Aprili wakati waasi walipoasi jeshi. Umoja wa Mataifa unazishtumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo zinapingwa na nchi zote mbili. Taarifa zinasema hali imekuwa mbaya zaidi eneo la kuzunguka Kijiji cha Kibumba kiasi cha kilomita 30 kaskazini mwa Goma tangu mwezi Julai.

Amesema serikali imepeleka vikosi zaidi, katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na helikopta za kijeshi, pia askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameonekana katika maeneo ya kijiji cha Kibumba. Msemaji wa Jeshi la Serikali mjini Goma, Olivier Hamuli, amesema wapiganaji waasi 44 wameuawa na afisa mmoja wa cheo cha juu katika jeshi la serikali pia ameuawa.

Pande zote mbili wamelaumiana kwa kuanzisha mapigano hayo yaliyoanza mapema asubuhi Alhamisi. Mwandishi wa habari hizi alisema wakati alipokuwa katika eneo linalodhibitiwa na waasi Jumatano, aliwaona waasi wa M23 -ambao pia hujulikana kama Jeshi la Ukombozi la Congo wakisambaza askari wake na kujiandaa kwa vita.

Watu wanakimbilia kuelekea kusini ambako majeshi ya serikali yanadhibiti maeneo hayo wakiwa wamebeba mizigo yao vichwani. Baadhi yao wamekuwa wakienda katika kambi kubwa ya Kibai iliyopo katika vitongoji vya kaskazini mwa Goma.

Msema wa Umoja wa Mataifanchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Luteni Kanali Prosper Basse, amesema pia kumekuwa na mapigano kilomita 90 kaskazini mwa Goma, huku majeshi ya serikali yakitwaa mji wa Mabenga na kusonga mbele kuelekea mji wa Kiwanja ambao ni mji muhimu wa waasi.
-BBC