Mapendekezo ya TGNP Katika Maoni ya Katiba Mpya

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni.

Mapendekezo ya TGNP Katika Maoni ya Katiba Mpya

1. Utangulizi

1. 0 UTANGULIZI

1.1 SHUKRANI

 Mheshimiwa Jaji Warioba -Mwenyekiti Tume ya Katiba
 Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani – Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Katiba
 Wajumbe wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Mtandao wa Jinsia Tanzania unapenda kutoa shukrani za dhati kwa Tume ya Katiba kwa kutupa nafasi ya kipekee kutoa maoni yetu katika mchakato huu. Kwetu sisi hii heshima kubwa na ishara ya utambuzi wa juhudi na mchango wa shirika letu katika kujenga jamii na taifa lenye kujali na kusimamia haki na usawa kwa wote. Tunapenda kuchukua nafasi hii pia kukupongeza wewe binafsi na tume nzima kwa uongozi na kazi kubwa ya kukusanya maoni ya Katiba nchi nzima
Aidha Mtandao wa Jinsia unaipongeza Serikali kwa kutoa Uongozi na rasilimali za kuwezesha utekelezaji wa mchakato huu wa kihistoria ambao kwetu ni fursa ya kipekee ya kujenga muafaka wa kijamii na kutengeneza sheria mama itakayoelekeza usimamizi na uwajibikaji juu ya rasilimali zote za nchi yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
1.2 KUHUSU MTANDAO WA JINSIA
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni asasi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kupigania haki za kijamii, usawa wa jinsia, kukuza uwezo wa wanawake, na kubadilisha mifumo kandamizi kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Tangu kuanzishwa kwa shirika mwaka 1993, Mtandao umefanya kazi kubwa katika kuwezesha mjadala wa kijamii na uelewa kuhusu haki na usawa wa jinsia, ukombozi wa wanawake kimapinduzi , kuwajengea wanawake uwezo pamoja na kushawishi mabadiliko ya mitazamo ya kijamii katika ngazi zote kwa kutumia mbinu za uraghbishi, utafiti shirikishi, uchambuzi wa sera , bajeti ya kijinsia , mafunzo ya jinsia kwa wanajamii na watendaji wa ngazi na sekta zote; pamoja na kuandaa na kusambaza taarifa na maarifa. Aidha Mtandao wa Jinsia umebuni na kuendeleza majukwaa na fursa za wanajamii kukutana , kujadili , kutafakari na kujenga mikakati ya utetezi na ushawishi kuanzia ngazi za msingi. Hizi ni pamoja na Semina za Jinsia na Maendeleo, Tamasha la Jinsia , Vituo vya Maarifa na Taarifa pamoja na kujenga mashirikiano na masirika na taasisi nyingine katika ngazi ya Taifa, Kikanda na Kimataifa.
Mtandao wa Jinsia unaamini kuwa changamoto nyingi za ubaguzi dhidi ya wanawake zinatokana na mwingiliano kati ya mifumo kandamizi hususan mfumo dume , upepari na utandawazi . Kwa hiyo, juhudi za TGNP za uraghbishi na kujenga nguvu za pamoja zimetokana na chambuzi yakinifu za muktadha wetu wa sasa na tafiti mbalimbali zilizoonesha jitihada za wanawake za kupambana na mifumo kandamizi pamoja na kuonesha hali halisi ya kiwango cha ukiukwaji wa haki za msingi za wanawake katika nyanja zote za uchumi, siasa, na ustawi wa jamii.
Kutokana jitihada hizi , Mtandao wa Jinsia Tanzania ukiunganisha nguvu zake na wanaharakati wengine umetoa mchango katika mijadala ya kitaifa, kikanda na kimataifa kuhusu muktadha wa mfumo wa ubepari , soko huria na athari zake kwa uchumi wa mataifa ya kusini mwa Afrika iliwemo Tanzania. Mtandao wa Jinsia umetoa michango katika kujenga hoja ya uzingatiaji wa masuala ya jinsia katika sera, sheria na michakato mbalimbali ya maendeleo hususani ni Bajeti ya Kijinsia , ajira na maisha endelevu , kuainisha mzigo wa kazi wa wanawake kama sehemu muhimu ya mchango wa pato la taifa , utambuzi wa mchango wa wanawake katika uzazi na kupinga vifo vya wanawake katika uzazi , utetezi wa maji safi na salama kama haki ya msingi ya kila mtanzania , utetezi wa ushiriki sawa katika nyanja zote za maamuzi na kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto.

Mtandao wa Jinsia kwa kushikiriana na wanaharakati ngazi ya jamii na kitaifa unaendeleza kampeni kampeni ya ‘HAKI YA UCHUMI: RASLIMALI ZIWANUFAISHE WANAWAKE WALIOKO PEMBEZONI’. Kampeni hii imetuwezesha kujifunza kupitia uraghibishi katika wilaya kadhaa zikiwemo Kisarawe, Morogoro Vijijini, Kishapu na Mbeya Vijijini ikiwa ni sehemu ya kukuza na kuendeleza kampeni hiyo. Sambamba na Kampeni na shughuli za uraghbishi, Shirika liliwezesha uanzishwaji wa vituo vya maarifa na taarifa, pamoja na mafunzo ya waandishi wa habari yaliyojikita katika kutetea haki za wanawake, kuhamasisha jamii kushiriki katika kutafakari na kupinga hali ya unyonyaji na unyanyaswaji wa jinsia na kitabaka, kukemea ukatili wa kijinsia, pamoja na kuimarisha vuguvugu la ukombozi wa mwanamke. Jitihada hizi zimeibua hamasa kubwa ya kuelewa haki za msingi za kila mwanajamii, hususani haki za wanawake, pamoja na haki za makundi yote yaliyowekwa pembezoni mwa mfumo rasmi.

Kwa mantiki hii, madai yaliyoainishwa katika makala hii ni madai yaliyotokana na mchakato wa muda mrefu, yakiwa yameibuliwa na wana jamii hususani wanawake kutoka ngazi mbalimbali za kitaifa, yakiweka sauti ya pamoja ya mambo ya msingi ya katiba mpya. Sisi wanamtandao tunaamini kwamba, katiba yenye mrengo wa jinsia sharti itokane na mchakato shirikishi ili katiba hiyo ipate ridhaa ya wanawake na wanaume. Vile vile wanamtandao tunaamini kwamba katiba yenye mrengo wa jinsia lazima ijikite kwenye misingi ya usawa wa jinsia, heshima na utu wa wanawake na wanaume wa Tanzania yetu. Kwa mantiki hii, wanamtandao tumeamua kuendesha mchakato shirikishi wa kuibua masuala ya msingi ya kijinsia hususani madai ya wanawake katika utayarishaji wa Katiba hii mpya.
2. Mchakato wa kuainisha masuala ya wanawake Kikatiba
Mchakato wa Mtandao wa Jinsia wa kuainisha masuala ya wanawake kikatiba umetokana na ushiriki mkubwa wa wadau mbalimbali wa Mtandao wa Jinsia. Kwanza kabisa ni ushiriki mkubwa wa wadau wa mikutano ya kila Jumatano (GDSS) inayofanyika katika viwanja vya TGNP. Vile vile TGNP ilishiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) lililohusisha wanawake takribani 110 kutoka taasisi zaidi ya hamsini zilizowakilisha asasi mbalimbali kutoka mikoa 19 ya Tanzania bara na visiwani tangu tarehe 22 hadi 24 Oktoba mwaka wa 2012. Kongamano hili lilijadili na kukubaliana mambo ya msingi ya masuala ya wanawake katika katiba mpya. Masuala haya yameainishwa katika rasimu hii. Vile vile mchakato ulinufaika na mkutano wa wahariri wa vyombo mbalimbali vya Tanzania uliyoitishwa na TGNP kwa ajili ya kujadili nafasi ya wahariri katika kuwezesha sauti za wanawake zifikie Tume ya Katiba Mpya. Baadhi ya mapendekezo ya wahariri yamejumuishwa katika rasimu hii. Kwa kifupi tunaamini kwamba masuala haya yametokana na sauti mbalimbali za wadau wanaotetea haki za wanawake na hususani haki za kikatiba.
3.0. Mapendekezo ya TGNP Kuhusu Haki za Wanawake Katika Katiba Mpya
1. Pendekezo la Kwanza: Katiba iwe na mrengo wa Jinsia. Sisi wanaharakati wa haki za wanawake tunapendekeza katiba mpya iwe na mrengo wa Jinsia.
Katiba Inayozingatia Masuala ya Jinsia Ikoje?
Kwanza kabisa ni katiba iliyotokana na mchakato uliyoshirikisha sauti za wanawake na wanaume, na iliyoweka bayana makubaliano ya misingi mikuu itakayoongoza nchi yao. Vilevile ni katiba iliyojengewa misingi ya usawa, utu na inayokataza aina zozote za ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia hivyo basi, katiba hii mpya , imtambue mwanamke na mwanaume, ihamasishe ukuaji wa mwamke na mwanaume katika uchumi, siasa, utamaduni na ukuaji wa jamii na kwamba imetokana na muafaka wa kitaifa uliyopata ridhaa ya wanawake na wanaume, wenye haki ya kuwa na katiba, kuijua na kuitumia kama sheria mama ya ulinzi wa haki zao. Hivyo katiba iwajibishe serikali kuhakikisha raia wote, wanawake na wanaume wanapata haki sawa na zinalindwa na katiba wana katiba, yenye lugha nyepesi na rafiki kwa makundi yote.
2. Pendekezo la Pili: Haki za msingi zilizoko kwenye katiba ya sasa ziendelezwe:
3. Mambo muhimu yanayopaswa kulindwa katika katiba ya sasa ni:
Tunapendekeza kuendeleza zile haki za msingi zilizobainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 lakini zipewe mrengo wa Jinsia.
Haki hizo ni zipi??

TGNP bango linaloonesha ofisi za TGNP


Katika utangulizi wake, katiba inatamka wazi kwamba ‘ Sisi Wananchi wa Tanzania tumeeamua rasmi na kwa dhati kujenga nchi yetu jamii inayozingatia msingi ya uhuru, haki, udugu, amani’ ( tuongeze usawa wa jinsia)
Sehemu ya Pili Ibara ya 8 inazidi kufafanua kwamba:
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia, na haki ya kijamii na kwa hiyo_
a. Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii
b. Lengo kuu la serikali ni ustawi wa wananchi;
c. Serikali itawajibika kwa wananchi;
d. Wananchi watashiriki katika shughuli za serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii
N.B. Tunataka itambulike kwamba wananchi, ni jumuisho la wanawake na wanaume, wa rika zote, wa tabaka zote bila kujali hali na tofauti za ujinsia wao umri wao au rangi zao. ( tunapendekeza hili libainishwe kwenye katiba mpya)
Katiba ibebe tafsiri ya neno wananchi ili matumizi yake yasije kutumika katika mwelekeo unaovunja misingi na haki za wananchi hasa katika mrengo wa kijinsia.
Ibara ya 9 inazidi kufafanua wajibu wa vyombo vya mamlaka ya nchi vinavyopaswa kutekeleza malengo yake kwa kuzingatia :
(a) Utu na haki nyinginezo za binadamu zinaheshimiwa
(c) Shughuli zote za serikali zinahakikisha kwamba utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa, na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote ( kuongeza wake kwa waume wa rika zote, tabaka zote) kwa ujumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine
(e) Kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi..
(f) Kwamba Heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa
(g) Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu;
(h) Kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu, au upendeleo zinaondolewa nchini
(i) kwamba matumizi ya utajiri wa taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanayoelekezwa kwenye jitihada ya kuondoa umaskini, ujinga na maradhi;
(j) Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi.
Haya ni mambo muhimu ambayo katiba mpya lazima iyabebe.
Ibara ya 11 (i) inazidi kubainisha wajibu wa mamlaka ya nchi kwa raia kwa kusema kwamba: ‘ Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu kwa ajili ya kuhakikisha kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi, haki ya kujipatia elimu, na haki ya kupata msaada kwa jamii wakati wa uzee na maradhi, au hali ya ulemavu, na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi ( tukazie bila ubaguzi wa aina yoyote uliyojikita katika ubaguzi wa jinsi, hali, rangi, dini au ukabila)
Kwa kuwa hizi haki zilizobainishwa hapo juu hazipo katika kifungu cha haki za binadamu, ibara ya 11 – 24, tunataka katiba mpya iingize haki hizi katika kifungu hiki ili haki hizi ziweze kudaiwa kwa mujibu wa sheria iwapo mwananchi atakosa haki hizi.
Ibara hiyo hiyo ya 11(2) inasema’ Kila mtu ana haki ya kujielimisha na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayotaka hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake. Serikali iwajibike kusimamia na kutoa huduma zote za msingi kwa jamii kama vile elimu, afya, maji nk. Na ihakikishe elimu ya msingi inakuwa ni ya sekondari na ni lazima kila mtanzania kuipata. Pia serikali ihakikishe elimu ya juu inatolewa bila ubaguzi.
Kifungu cha (3) kinaitaka serikali kuhakikisha kwamba watu wote ( tuongeze bila kujali hali, jinsi, rangi au dini) wana fursa sawa na za kutosha kupata elimu.
Sehemu ya Tatu ya katiba ni matamko ya Haki na wajibu wa raia.
(a) Kwamba binadamu wote huzaliwa huru na ni sawa, kwamba ,
(b) kila mtu ni sawa mbele ya sheria,
(c) kwamba kila mtu ana haki ya kulindwa, na kutobaguliwa,
(d) na vilevile ibara ya 12 kifungu cha 2 kinapiga marufuku sheria zote za ubaguzi zilizotungwa na chombo chochote cha Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania. ( tunapendekeza katiba mpya ipige marufuku sheria zote kandamizi hususani sheria zinazowakandamiza wanawake. Ni wajibu wa chombo kinachotumika kutunga sheria kutunga sheria zinazomkandamiza mwanamke na mtoto.
(e) Haki ya ya kuwa huru, haki ya hifadhi, haki ya kufanya kazi, kutoa maoni zimeainiswa katika sehemu hii pamoja na wajibu wa kila mtu. ( hizi haki zianishwe kwenye katiba mpya )
Ibara ya 21 inasema kwamba kila raia,( Wanawake na waume) wana haki ya kushiriki katika shughuli zozote za utawala wa nchi aidha kwa kuchaguliwa au kuteuliwa. Huu ni msingi tunaopendekeza uendelee kuonekana katika katiba mpya)
Ibara ya 22 na 23 zinatamka kuwepo fursa sawa ( equal opportunity employer in public services) katika utumishi wa umma. ( huu ni msingi utakaolinda wanawake dhidi ya ubaguzi na utakaowajibisha mamlaka ya nchi kuweka utaratibu wa kuhakikisha fursa sawa zinatekelezwa)
Ibara 24 (2) inapiga marufuku kwa mtu yoyote kunyaganywa mali yake kwa madhumuni ya kutaifisha, au madhumuni mengineyo bila ya idhini ya sheria inayotoa idhini ya fidia inayostahili. ( msingi huu uwepo katika kulinda mali ya wanawake hasa wajane wanaoporwa mali yao, na hapa kusiwepo sheria ya kuhalalisha uporaji wa mali ya wanaje, watoto wa kike, )
Kwa kutambua ushiriki mdogo wa wanawake katika uongozi wa taifa, katiba imeweka masharti ya kuwezesha uwakilishi wa wanawake usiopungua asili mia thelathini katika Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania na katika mabaraza ya Madiwani. ( Katiba mpya iendeleze msingi huu wa kuweka mikakati ya makusudi ya kuwezesha wanawake kushiriki katika uongozi siyo bungeni tu bali uwe katika nyanja mbalimbali ndani ya jamii zetu)
Kwa kifupi sisi wanamtandao tunasema misingi iliyoko kwenye katiba hii inayotumika iingizwe kwenye katiba mpya kwa kuzingatia mrengo wa jinsia. Na kwamba katiba ijulikane ni mali ya Watanzania wote wanawake na wanaume hivyo iwekwe kwenye lugha nyepesi itakayowawezesha wanawake kuitumia katika kutetea haki zao.
4. Pendekezo la Tatu: Mikataba kuhusu haki za wanawake na watoto ziwe sheria mara tu Tanzania inaporidhia:
Wanaharakati wa Haki za wanawake tunapendekeza kwamba Mikataba na Matamko yote ya Kimataifa, na kikanda ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia kuhusu haki za wanawake, ziwe sheria za nchi moja kwa moja. Mikataba hii ni pamoja na: Tamko La Kimataifa Kuhusu Haki za Binadamu, na ( Bill of Rights), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake, (CEDAW), Mkataba wa Haki za Watoto, (CRC) Tamko la Beijing Kuhusu Haki za wanawake, mikataba mbalimbali ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) inayokataza ubaguzi wa jinsia katika ajira ikiwa ni pamoja na Mkataba wa ILO wa 100 na 111 zinazozuia ubaguzi katika uajiri na kwenye mahali pa kazi, ILO 182 inayohusu kulinda watoto dhidi ya ajira hatarishi, Mikataba ya Kikanda kama vile , Tamko la SADC kuhusu Maendeleo na Jinsia, Mkataba wa Haki za Binadamu za Umoja wa Afrika, pamoja ( Constituent Act 2000), Maputo Protocal, ambayo Tanzania imeridhia iwe sheria ya nchi.

5. Pendekezo la Nne: Katiba Mpya itoe mwongozo utakaobatikisha sheria Kandamizi:
Katiba mpya ibatilishe sheria zote zinazokinzana na haki za msingi za wanawake na watoto wa kike hususani kubatilisha sheria na mila zote za ubaguzi wa jinsia katik maswala ya ndoa, mirathi, haki za uraia na haki za kumiliki utajiri wa Taifa hili. Kwa mantiki hii, katiba ibainishe kwa uwazi wajibu wa serikali wa kuchukua hatua zote za kisera na sheria ili kulinda na kuhifadhi haki za wanawake katika maeneo hayo (rejea sehemu ya 3 ya katiba ya sasa kifungu d kama kilivyofafanuliwa hapo juu)
6. Pendekezo la Tano: Haki sawa za Uraia
Katiba mpya iwape wanawake haki sawa za uraia, hivyo mwaname atakayeolewa na raia ambaye siyo Mtanzania ana haki ya kuridhirisha uraia kwa mwenzi na watoto wake
7. Pendekezo la Sita: Kulinda Utu wa Mwanamke :
Katiba iweke msingi ya kuulinda utu wa mwanamke dhidi ya uonevu na ukatili wa jinsia ndani ya ndoa na kwenye jamii. Ikiwa ni pamoja na kukataza ubakaji ndani ya doa, kukataza mila zinazomdhalilisha mwanamke, ( tohara, kurithiwa bila hiari, ) na kubainisha haki sawa ndani ya ndoa. Pamoja na kukataza ndoa za watoto wa kike.Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za kisera na kisheria na bajeti ili kukaza utekelezaji
8. Pendekezo la Saba: Haki ya kumiliki Rasilimali ya Nchi:
Katiba ikiri kwamba rasilimali tuliyonayo, ni mali ya Watanzania wanawake na wanaume, na kwamba ni wajibu wa serikali kuchukua hatua za kisera na sheria zitakazoweka misingi ya kumwezesha mwanamke kumiliki na kunufaika na utajiri huu wa taifa letu kwa njia zifuatazo: (i) kuzuia uuzaji wa ardhi ya familia bila ridhaa ya wanafamilia wote,( ii) kuzuia uporaji wa ardhi unaofanywa na wawekezaji wa ndani na nje (iii) kuwawezesha wanawake kupata taarifa za kuwekeza katika sekta mbalimbali za taifa husani skta ya kilimo
9. Pendekezo la Nane: Haki za wanawake ya kufikia na Kunufaika na huduma za msingi za Kijamii
Katiba ibainishe huduma za msingi zinazomwezesha Mtanzania kuishi maisha yenye utu na heshima na kama vile chakula, malazi, mavazi, maji, huduma za afya kwamba ni stahili ya kila mtanzania . Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za kisera, kisheria ili kumhakikishia mwanamke na mtoto wa kike anafikia na kunufaika na huduma hizi.
10. Pendekezo la Tisa: Michango ya Wanawake katika Uchumi na Pato la Taifa
Katiba mpya iweke misingi ya kuwezesha kutambua michango ya wanawake katika kuendeleza uchumi hususani rasilimali watu, ili kuzuia sera zinazoelekeza kumwongezea mwanamke mzigo mkubwa zaidi kama vile sera za kurudisha wagonjwa mahututi majumbani, na ili serikali iwajibishwe kuchukua hatua za kisera, sheria na bajeti kuwekeza katika huduma zitakazompunguzia mwanamke mzigo wa ziada katika kuendeleza uhai wa taifa letu. Huduma kama vile vituo vya kuwalelea watoto, kuwatunza wazee, na kuwatunza watu wenye ulemavu wasiyoweza kufanya kazi za kujikimu.

11. Pendekezo la Kumi: Haki ya Afya ya Uzazi:
Kumekuwepo mzigo mkubwa wa majukumu anaobebeshwa mwanamke katika kuendeleza kizazi cha taifa bila kupewa nyezo na bila ulinzi wa afya yake. Serikali ipewe jukumu la kuchukua hatua za kisera na sheria, kuhakikisha uwekezaji katika afya ya uzazi, pamoja na kumpa mwanamke haki ya maamuzi ya msingi kuhusu mipango ya uzazi, umiliki wa miili yao, na ufikiaji wa huduma za uzazi na uhakika wa ulinzi wa uhai wake anapofanya kazi ya kuendeleza kizazi cha taifa hili. Katiba mpya ihakikishe afya ya uzazi inalindwa kikatiba.
12. Pendekezo la Kumi na Moja: Wajibu wa Wazazi Wanaume na Wanawake katika Malezi ya Watoto:
Katiba iainishe wajibu sawa wa wazazi hususani wanaume katika malezi ya watoto kwa kutambua mzigo wa ziada wanaobebeshwa wanawake katika kutunza mimba, kuzaa, kunyonyesha na kulea.
13. Pendekezo la Kumi na Mbili: Haki za Watoto wa Kike:
Kumekuwepo na ukiukwaji wa haki za watoto na ubaguzi wa watoto wa kike, hasa taratibu za ndoa za utotoni, umiliki wa mali ya wazazi wanapofariki, ambalo chumbupo lake kubwa ni katiba kuendelea kuzitambua sheria za mila na tamaduni zinazonyima haki, hivyo Katiba iwajibishe serikali kuchujua hatua za kisera na sheria pamoja na kusimamia utekelezaji wa haki za watoto wa kike na kiume katika maswala ya elimu, ufikiaji huduma, ulinzi na heshima ya utu wao. Katiba mpya ipige marufuku na kubatilisha sheria kandamizi za kimila ikiwemo ndoa za utotoni
14. Pendekezo la Kumi na Tatu: Ushiriki Wa Wanawake katika uongozi:
Katiba mpya ibainishe misingi itakayozuia kuhothiwa kwa madaraka katika mihimili mikuu ya utawala kwa jinsia moja. Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za kisera na sheria ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa uwiano sawa katika uongozi wa mihimili mikuu ya utawala ( serikali, Bunge na mahakama) . Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za kisera na sheria na bajeti kuhakikisha utekelezaji wa misingi ya usawa kwa kuzingatia mkataba wa African Union (AU) wa 50/50 %.

a. Kwa mfano: Katika Uongozi wa juu wa utawala : ikiwa ni pamoja na Rais, Makamo wa Raisi na Waziri Mkuu, lazima kuweko na jinsia zote. ) uteuzi wa wakuu wa mikoa, na wilaya, bodi za mashirika ya umma, na viongozi wa mashirika haya uzingatie kanuni ya AU kuhusu 50/50%, kama serikali yetu ilivyoridhia.
b. Vilevile serikali iwajibishe sekta binafsi kuzingatia sheria hii ktk uongozi wa mashirika yao.
c. Vilevile katiba mpya iwajibishe vyama vya siasa kuweka taratibu za kutekeleza sera za usawa wa jinsia katika uongozi wa vyama, katika kuchagua na kuwezesha ushiriki wa wanawake katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi hususani za uwakilishi na za kuteuliwa ktk ngazi zote ndani ya chama.
d. Katiba mpya iruhusu wagombea binafsi ili kuwezesha wanawake na wanaume wanaopenda kuwakilisha watanzania bila kupitia mgongo wa vyama waweze kupata fursa hiyo, tukitambua kubwa kuna asilimia kubwa ya Watanzania ambayo siyo wanachama wa chama chochote.

• Katiba mpya iweke mwongozo ambao kila mgombea kwa ngazi zote atatakiwa kupitia hatua kuu za kuchuja wagombea kwa ngazi zote kwa kuzingatia jinsi zote ,hatua hizo ni:Uteuzi wa wagombea kwa kufuata misingi ya haki na shirikishi
• Wagombea kunadi sera zao kwa wananchi
• Na kisha kuweka vigezo vya kiushindani vitakavyo wezesha kupatikana kwa viongozi kwa kuzingatia uwiano wa 50 kwa 50.

• Tuwe na wabunge wa kuchaguliwa tu isipokuwa wale watano (5) kutoka Zanzibar
• Jimbo la uchaguzi liwe Wilaya
• Kila wilaya itoe wabunge wawili (2) mwanamke na mwanaume, wote wapigiwe kura na wananchi, hivyo wananchi wapigie kura wabunge wawili ke na me kwa listi mbili tofauti ya mwanamke na mwanaume, tunazo Wilaya 148. Hivyo wilaya zote kutakuwa na wabunge 296 na watano jumla 301. Bunge hili ni zuri sana dogo na litatupeleka kwenye dhana ya kutafakari viti maalum vya wanawake lakini pia tutapata zaidi ya 50: 50 kwa maana ya kuongeza wabunge wa makundi maalum kama vile walemavu wa aina zote. Tukitumia wilaya kuwa jimbo la uchaguzi tutaondoa lalamiko la Tume ya uchaguzi kugawa majimbo kwa shinikizo la vigogo.

15. Pendekezo la Kumi na Nne: Ushiriki Wa Wanawake katika Ajira Salama yenye Kukimu maisha :
Katiba iweke misingi itakayowezesha utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu ajira salama, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku ubaguzi wa ki jinsia kutokana kuwepo mifumo kandamizi na , kuweko kwa mazingira yasiyo salamaya kazi kwa wanawake wajawazito,wagonjwa na wazee,pia likizo ya uzazi kwa wanawake wote, , katika sekta binafsi, sekta rasmi na katika sekta isiyo rasmi. Kwa mfano kwa wafanyakazi wa majumbani,mabaa na mahoteli,mamalishe nk.Katiba mpya itoe wajibu kwa serikali na vyombo vyake vyote kutengeneza mifumo itakayosaidia mwanamke kupata ajira salama.
16. Pendekezo la Kumi na Tano: Usawa mbele ya sheria :
Katiba iweke misingi ya kuwezesha kuweko kwa mazingira ya upatikanaji wa haki sawa ya wanawake na wanaume mbele ya sheria, aidha akiwa mtuhumiwa au mtuhumu. Katiba iwajibishe serikali kutoa huduma za kisheria kwa wanawake. Huduma hii iende sambamba na mikakati ya kubatilisha sheria kandamizi .
17. Pendekezo la Kumi na Sita: Haki ya Wanawake Kupata hifadhi ya jamii :
katiba itambue haki za kila mtanzania wanawake na wanaume, za kupata hifadhi ya jamii wakati wa uzeeni, serikali iwajibishwe kubuni mbinu za kuwezesha wanawake na makundi mengine yaliyoko pemebezoni kufikia na kufaidi huduma za hifadhi wakati wa uzeeni.
18. Pendekezo La Kumi na Saba: Haki za Wanawake wenye Ulemavu:Katiba ikiri kuweko kwa ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu hususani wanawake wenye ulemavu , hivyo iwajbishe serikali kuchukua hatua za kisera na kisheria kulinda haki za msingi za watu wenye ulemavu. Ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kuheshimiwa, kupata taarifa, kufikia huduma, haki ya ajira.
19. Pendekezo la Kumi na Nane: Haki za Wanawake zibainishwe katika Katiba Mpya na ziingizwe kwenye Tamko la Haki za Msingi ( bili of rights)
Katiba mpya ibainishe haki za makundi maalum kama vile haki za wanawake, haki za watoto, wazee na watu wenye ulemavu na haki hizi ziingizwe kwenye Tamko la haki za Msingi ( bill of rights) ili makundi haya yaweze kuzidai na kuzitetea kisheria.
20. Pendekezo la Kumi na Tisa: Kuundwa kwa Chombo cha kusimamia utekelezaji: Katiba mpya iwajibishe serikali kuundwa kwa chombo cha kusimamia utekelezaji wa haki za wanawake na kuwajibisha utoaji wa Taarifa kuhusu hatua mahususi za kuleta usawa wa jinsia kama ilivyoainishwa katika Katiba.

21. Pendekezo la ishirini
Nafasi za Asasi za Kijamii
Katiba mpya itambue mchango na wajibu wa taasisi na asasi za kiraia hususan zinazofanya kazi kuhusu sera . Asasi za kijamii ziachwe huru ili ziweze kutoa sauti mbadala ya kudai haki na usawa pale katika kuleta mabadiliko chanya ya Wananchi walio wengi. Kuwepo na muundo ambao utawezesha Asasi kuwa huru na kufanya kazi kwa maslahi ya taifa na serikali isiingilie mfumo husika.Pia serikali itoe taarifa muhimu kwa asasi husika kwa ajili ya manufaa ya umma .Kwa kuwa suala hili la upatikanaji wa taarifa muhimu ni suala la kikatiba basi katiba iwajibishe serikali pale inaposhindwa kutimiza wajibu huu.
22. Pendekezo la ishirini na moja: Maadili ya Taifa
23. Kumekuwepo na mmomonyoko wa madili ya kitaifa na hasa kwa viongozi ambao kimsingi ni wasimamizi wa rasilimali za nchi ambazo zinapaswa kulindwa na kugawiwa kwa wananchi wote.Pamoja na uwepo wa tume yenye kusimamia maadili ya viongozi kumebainika mapungufu ya usimamizi wa misingi inayolinda maadili ya viongozi pamoja na kuwajibisha viongozi wanaokiuka maadili hayo.Katiba mpya iwe na wajibu wa kuipa nguvu na mamalaka kisheria Tume hiyo ili kusimamia maadili ya viongozi.mali za viongozi zitangazwe wazi kwa wananchi wanaohitaji kupata taarifa hizo.Kwa upande wa wananchi katiba ibainishe maadili ya wananchi wa Tanzania mfano suala la kutoa na kupokea rushwa, ulinzi wa rasilimali za nchi n.k
24. Pendekezo la Ishirini na Mbili : Mfumo wa kiutawala katika serikali za mitaa
25. Serikali za mitaa ziwe huru na zenye mamlaka kamili katika Majiji,Manispaa na halmashauri za Wilaya Miji,Vijiji,mitaa na vitongoji.Serikali kuu isiwe na mamlaka yoyote ya kiuongozi na maamuzi katika ngazi hizo,isipokuwa katika mambo yahusuyo sera na sheria za kitaifa tu.

Hitimisho:
4. Mazingira wezeshi-Itikadi ya pro-people, inclusiveness, democrasia Jumuishi, maadili, katiba inayo elekeza uwajibikaji – unazingatia masuala ya kijinsia.
• Sisi tunaamini kuwa ili haya yote yatekelezeke ni muhimu kuwepo mazingira wezeshi kama:
o Uwepo na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu – baraza la mawaziri, mahakama na bunge na uwajibikaji huu uwe ni pamoja na kuwajibika kwa Watanzania woteo, wanaume na wanawake.
o Katiba itamke bayana kuhusu itikadi inayoongoza nchi yetu. Tunapendekeza itikadi inayozingatia ustawi wa wananchi (pro-poor). Hii itawawezesha wanawake waliyo wengi kutetea na kudai haki zao pamoja na kufikia huduma za msingi
o Rasilimali za wananchi zilindwe na wananchi wenyewe
o Hatua za makusudi za kuongeza ushiriki kwa wanawake (Affirmative Action) isiwe ya ki baguzi. Wawakilishi wa viti maalum waweze kushika nafasi za uongozi k.m. kuwa Waziri Mkuu, wenyeviti wa kamati au mabaraza mbalimbali.
o Mfumo wa kuchagua viongozi unategemea sana vyama vya siasa kuteua viongozi wakati wananchi wengi si wanachama wa vyama vya siasa. Hivyo kutatoa fursa kwa wanawake na wale wasio kuwa na vyama.
o Tutategemea Tume ya Mabadiliko ya Katiba itaendelea kushirikiana na wadau na wataalam wa masuala ya Jinsia /wanawake katika kuhakikisha masuala hayo yanaingizwa kikamilifu katika katiba mpya.
Sisi wanamtandao wapigania haki za wanawake , tunapendekeza kwa tume ya katiba mchakato wa kutayarisha katiba mpya uongozwe kwa kutambua kwamba:
Mfumo ulioko pamoja na sheria, mila na desturi zinaendeleza ubaguzi dhidi ya wanawake
Vilevile mchakato huu uongozwe na ufahamu na uelewa wa kuweko kwa tabia, desturi na mila za ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya watu walemavu, wanawake walemavu wakiadhirika maradufu
Pamoja na kuendelea kuweko ukiukwaji wa haki za msingi za watoto na ubaguzi dhidi ya mtoto wa kike
Changamoto zitokanao na mfumo mpana wa soko huria zinazomlea zaidi mwanamke Mtanzania hususani waishio vijijini, na maskini wa mjini, wanawake wenye ulemavu na watoto wa kike.
Hivyo basi wanawake wa Tanzania wanadai na kuhimiza ushiriki wao katika mchakato wote wa kutayarisha katiba mpya ikiwa ni pamoja na mchakato wa sasa wa kupata maoni ya raia, uundaji wa bunge la katiba, pamoja na kura za maoni. Hii itawezesha kubainisha haki zao za msingi ziweze kuingizwa katika katiba mpya mpya ili kuhakikisha ulinzi wa haki zao kikatiba.
MWISHO