Maoni ya Wanawake Wajasiliamali Dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete na Ijayo (1)
TAREHE 25, Oktoba 2015 Watanzania wenye sifa za kupiga kura wanatarajia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu kuchagua viongozi ambao wataunda Serikali ya awamu ya tano na kuliongoza taifa kwa kipindi cha miaka 5 mfululizo. Yafuatayo ni maoni ya baadhi ya wanawake wajasiliamali walioshiriki Maonesho ya 39 ya Biashara Kimataifa (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam juu ya Serikali inayomaliza muda wake na ijayo.
Bi. Hiraria Aloyce Murisi-Kijiji cha Mwada Tarafa ya Mbugwe Babati Vijijini Mkoa wa Manyara anasema;
“…Serikali inayomaliza muda wake imejitahidi kuwainua akinamama hasa kuboresha huduma za afya kwa akinamama na watoto chini ya miaka mitano, vivile upande wa wajasilimali imejitahidi kuwasaidia akinamama japo bado akinamama wengine hawajatambua fursa hizo…Naomba Serikali ijayo iendeleze kile ambacho kimeanzishwa na Serikali inayomaliza muda wake, hasa kuwaunganisha akinamama na masoko ya nje hasa kwenye upande wa soko la Afrika Mashariki na kuwawezesha pia kielimu. Lakini mama bila afya bora hawezi kufanya vizuri katika shughuli zake hivyo Serikali iendelee kushughulikia changamoto ya wahudumu kwa zahanati za vijijini kwani bado ni kikwazo cha huduma za afya vijijini…”
Naye mjasiliamali Dafrosa Mgimba kutoka Mkoa wa Njombe Wilaya ya Njombe anasema;
“…Kwa serikali mimi siwezi kusemea imetusaidia nini maana sisi tupo pembezoni kule vijijini na mara nyingi watu wa pembezoni vijijini huwa tunasahaulika na hatuonekani, na hatujapata msaada wowote kuona tunasaidiwa, lakini huduma hatuwezi kusema zote zinatufikia maana kuna mambo mengine kwa kweli mpaka sasa hivi ni bado bado kama vile huduma za afya kwenye hospitali zetu zahanati zipo ila dawa hakuna…majengo yapo ila dawa hakuna ukienda unamkuta muhudumu anakuandikia dawa na kukwambia kanunue dawa hizo na unapokwenda kwenye maduka ya dawa huwezi kuwa na hakika na huduma unazopewa maana unakutana na watu wanaotoa huduma kule ambao hujui kama wamesomea au wanababaisha na kazi hiyo. Nashauri Serikali inayokuja ijitahidi kuhudumia watu tunaoishi pembezoni yaani vijijini ili tuweze kupata mahitaji muhimu kama vile huduma za maji, afya, barabara na vitu vingine vingi muhimu…,”
Bi. Stevina Msimbe ambaye ni mjasiliamali kutoka Vijimbambo Shop anasema;
“Namshukuru Mungu kwa upande wangu Serikali hii imetusaidia hasa kwa sisi akinamama wajasiliamali mfano mimi nilikuwa mjasiliamali mdogo na sijulikani lakini sasa najulikana kupitia Serikali…lakini nashauri itusaidie zaidi akinamama hasa wajasiliamali kupata mitaji maana kwenye mabenki ukienda kukopa unaambiwa lete hati ya kiwanja au nyumba kwasababu tuna shida tunaenda lakini kwenye malipo kunaunyanyasaji mkubwa. Tunaomba serikali sasa itutafutie ruzuku ili tuweze kufanya vizuri zaidi…Naiomba Serikali ijayo ijitahidi kupunguza vikwazo kwenye taasisi za viwango kama TBS maana wanatuchaji gharama za juu sana katika kupima bidhaa zako,” alisema.
Maoni hayo yalitolewa na baadhi ya Wanawake wajasiliamali walioshiriki Maonesho ya 39 ya Biashara Kimataifa (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Itaendelea…