MAONESHO ya wajasiriamali wadogo na wakati katika sekta ya Viwanda yanayoratibiwa na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Kanda ya Kusini kufanyika mkoani Ruvuma mwaka 2011. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Meneja wa SIDO, Mkoa wa Ruvuma Bw. Athur Ndedya.
Bw. Ndedya akizungumza na wanahabari alisema “SIDO imekuwa utaratibu wa kuandaa maonesho ya wajasiriamali kikanda kila mwaka. Maonesho haya hukutanisha wajasiriamali toka mikoa ya kanda husika ambayo ni Lindi,Mtwara, Ruvuma, na mikoa mingine ya Tanzania bara na wakati mwingine hushirikisha hata wajasiriamali toka nchi jirani”.
Maonesho yatafanyika wilayani Mbinga kuanzia tarehe 8 – 12 Septemba 2011. Kauli mbiu ni miaka 50 ya uhuru, tumia mashine na teknolojia ya viwanda vidogo kuongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini.
Maonesho haya yanahusisha wajasiriamali wazalishaji wa viwanda vidogo, ambao wako katika makundi mbalimbali ambayo ni,Bidhaa za uhandisi, Bidhaa za mafundi wadogo, Bidhaa za usindikaji wa vyakula, na matunda, Bidhaa za ushonaji, kazi za mikono pamoja na bidhaa zingine.
Katika maonesho hayo wajasiriamali hushindanishwa katika makundi ili kutoa changamoto ya kuwa na bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko na zenye ubunifu wale wenye bidhaa hutunukiwa zawadi pamoja na vyeti.
Naye Afisa Biashara wa SIDO Ruvuma, Bw. Stephano Ndunguru, alisema, “Lengo la maonesho hayo ni wajasiriamali waweze kutangaza bidhaa zao,waweze kujifunza kwa wenzao,wajijengee mtandao wa mawasiliano,kibiashara miongoni mwao wapate marejesho na maoni toka kwa watejja hatimaye wauze bidhaa hizo”.
Hayo yote yatapelekea kuimarika kwa mnyororo wa thamani kwa mazao na bidhaa mbali mbali zinazo zalishwa hapa mkoani,kanda na maeneo mengine hapa nchini.Wajasiriamali watapata mafunzo na ushauri tokka kwa maafisa wa SIDO na wadau wengine wa maendeleo kama taasisi za fedha,TBS na vyuo vya ufundi n.k
Maonesho hayo yatawakutanisha wajasiriamali na masoko hivyo kupanua wigo wa soko kupitia mafunzo na ushauri unaotolewa na maafisa masoko wa shirika la SIDO katika kipindi cha maonesho hayo.
Naye Afisa Habari wa mradi wa Munganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) Bw. Dunstan Mhilu amewataka wajasiriamali watumie fursa hiyo kujitangaza na kujifunza kwa washiriki wanaotoka sehemu mbali mbali watakao shiriki katika maonesho hayo.
Katika ulimwengu wa ushindani wa kibiashara maonesho yamewajengea wajasiriamali uwezo na ubora wa bidhaa kutokana na changamoto ya ushindani lazima wajasiriamali wazalishe bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya soko.
Mashirika mengine yanayosaidia wajasiriamali kama TBS na taasisi mbalimbali za fedha pia wanashauriwa kusaidia katika kufanikisha maonesho haya ili wayatumie kutoa elimu kwa wajasiriamali juu ya huduma zao. Maonesho hayo yalianzishwa mwaka 2002. Mwaka jana yalifanyika Mkoani Mtwara wilaya ya masasi.
(Picha na Habari kutoka kwa mdau maalum wa TheHabari)