Maonesho Kumuenzi Baba wa Taifa Kufanyika Okt. 13

Julias Kambarage Nyerere

Julias Kambarage Nyerere

Na Anna Nkinda – Maelezo

TAASISI ya Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameandaa maonesho na mdahalo wa kukumbuka na kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kujenga, kutetea, kulinda na kudumisha amani Duniani.
 
Maonyesho hayo ya siku tano ambayo yatafunguliwa tarehe 13 na kumalizika terehe 17 mwezi huu yatafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa yaliyopo jijini Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Gallus Abedi ambaye ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ilisema maonyesho hayo yatajikita zaidi kuonyesha picha, nyaraka, vitabu, matukio na kazi mbalimbali zinazohusiana na Baba wa Taifa ambaye ni Rais wa Kwanza na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania.
 
Mada zitakazotolewa katika mdahalo utakaofanyika tarehe 17 ambayo ndiyo siku ya kilele  cha makumbusho hayo ni misingi, utekelezaji na usimamizi wa kujenga, kulinda na kudumisha amani na uchambuzi na mifano halisi ya Sera za utekelezaji wa misingi ya kujenga amani kwenye Sekta mbalimbali za maendeleo.