Maofisa Polisi Kukutana Kuweka Mikakati Kukabili Uhalifu

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya NMB PLC, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akimkabidhi Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Abdulrahman Kaniki (kulia) moja ya mabegi ya msaada yaliyotolewa na Banki ya NMB jana Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam. Mabegi hayo yanatarajia kutumika katika Mkutano Mkuu wa Makamishna na Maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania utakaofanyika kesho kutwa jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Utumishi Jeshi la Polisi, DCP, Gabriel Semiono akishuhudia tukio hilo.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya NMB PLC, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akimkabidhi Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Abdulrahman Kaniki (kulia) moja ya mabegi yaliyotolewa na Banki ya NMB jana Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam. Mabegi hayo yanatarajia kutumika katika Mkutano Mkuu wa maofisa wakuu wa makao mkauu, makamanda wa Polisi wa mikoa yote, vikosi bara na Zanzibar ili kujadili mafanikio na changamoto anuai. Kulia ni Mkuu wa Utumishi Jeshi la Polisi, DCP, Gabriel Semiono akishuhudia tukio hilo. 

 

Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi

MAOFISA wakuu wa Jeshi la Polisi wanatarajia kukutana jijini Dar es Salaam kesho katika kikao kazi cha siku mbili kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu na wahalifu hapa nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Advera Bulimba alisema kikao hicho kitawakutanisha maofisa wakuu wa makao mkauu, makamanda wa Polisi wa mikoa yote, vikosi bara na Zanzibar ili kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utendaji katika kipindi cha mwaka uliopita na kuweka mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa mwaka huu.

Aidha, Bulimba alisema mbali na utaratibu wa mawasiliano ya kila siku katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi pia lina utaratibu wa kukutana kila mwaka kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu na mbinu za wahalifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika hapa nchini.

“Katika kikao hicho Inspekta Jenerali wa Polisi atatoa maelekezo ya kiutendaji ambayo lengo lake ni kuhakikisha kuwa kila ofisa, mkaguzi na askari anawajibika kwa nafasi yake katika kuhakikisha uhalifu unapungua hapa nchini” Alisema Bulimba.

Bulimba alisema kikao kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga ambapo kauli mbiu katika kikao hicho ni “Badilika kifikra, acha kufanya kazi kwa mazoea”.