Maofisa 24 wa Polisi Misri Wauwawa, Mohammed Badie Akamatwa

Kiongozi Mkuu wa Muslim Brotherhood, Mohammed Badie

TAKRIBAN maofisa 24 wa Polisi nchini Misri wameuawa kwenye shambulizi la kushtukiza katika eneo la Rasi la Sinai. Taarifa zinasema polisi hao walikuwa kwenye msafara wa mabasi mawili yaliyoshambuliwa na kundi la watu waliokua na silaha karibu na Mji wa Rafa mpakani na Ukanda wa Gaza.

Polisi watatu walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. Hivi karibuni jeshi la Misri limeimarisha operesheni dhidi ya wanamgambo eneo la Sinai hususan baada ya mashambulizi kuongezeka tangu kuanguka kwa uliokua utawala wa Hosni Mubarak mwaka 2011.

Misri imekua ikishika doria eneo la Sinai chini ya mkataba wa mwaka 1979 kati ya Israel na Misri. Mashirika ya habari yanaripoti kwamba wanaume wanne waliojihami kwa silaha walisimamisha mabasi hayo na kuwaamrisha abiria wote kushuka kabla ya kuwamiminia risasi.

Baadhi ya duru zinasema washambuliaji hao walitumia maroketi kulenga mabasi hayo. Utawala wa mpito umetangaza hali ya hatari kufuatia maandamano ya umma yaliofuatia kuondolewa madarakani kwa kiongozi Muhammed Morsi aliyekuwa Rais wa nchi hiyo.

Zaidi ya watu 800 wakiwemo polisi 70 wameuawa tangu Jumatano ya wiki jana wakati jeshi lilipovunja kambi za wafuasi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood anakotokea Morsi. Na hapo Jumapili mahabusu 36 walikufa wakati wakisafirishwa katika jela moja nje ya mji wa Cairo.Serikali na jeshi wamesema mahabusu hao walikosa hewa kwenye gari walimokua. Hata hivyo Muslim Brotherhood wametaja kitendo hicho kama mauaji ya kinyama.

Wakati huo huo wanachama wa Muslim Brotherhood wamelaani vikali kitendo cha kukamatwa kwa kiongozi wake Mkuu Mohammed Badie, kwa tuhuma za uchochezi wa ghasia na mauaji.

Msemaji wa kundi hilo amesema kukamatwa kwa kiongozi huyo ni njama ya kulipiza kisasi mapinduzi ya umma yaliyomuondoa madarakani Rais wa zamani Hosni Mubarak mwaka wa 2011. Badie alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka makaazi yake karibu na kitovu cha maandamano ya wafuasi wa Brotherhood Mjini Cairo.

Jeshi la Misri lilivunja kambi hizo wiki iliyopita ambapo kulitokea maafa ya raia wengi. Aliyekua Makamu wa Rais Mohamed ElBaradei anakabiliwa na mashtaka ya kusaliti imani ya taifa.

ElBaradei aliondoka nchini Misri baada ya kujiuzulu kufuatia hatua ya jeshi kuvunja kambi za wapinzani na kusababisha maafa ya mamia ya watu. Utawala wa mpito umetangaza hali ya hatari nchini Misri na kumekua na operesheni kali dhidi ya wafuasi wa Rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi.

Muslim Brotherhood wamewaomba wafuasi wao kuendelea na maandamano kushinikiza jeshi limrejeshe madarakani Bw. Morsi. Kwenye mkutano na waandishi wa habari mmoja wa viongozi wa chama cha Justice And Freedom Party, mrengo wa kisiasa wa Brotherhood alisema kukamatwa kwa kiongozi wake hakutadidimiza harakati zao.

Mohammed Badie amekua akiongoza maandamano ya wafuasi wa Bw Morsi. Hata hivyo aliingia mafichoni baada ya serikali kutangaza onyo la kuvunja kambi za waandamanaji. Kiongozi huyo anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia na mauaji ya raia wanane waliopinga Muslim Brotherhood. Mzozo wa kisiasa nchini Misri umepelekea mauaji ya watu 900 na maelfu kujeruhiwa.

-BBC