ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba amestaafu rasmi kulitumikia Jeshi la Polisi Nchini. Manumba amelazimika kuacha kulitumikia jeshi hilo baada ya kufikia umri wa kustaafu kisheria, ambao ni miaka sitini (60) katika utendani wake wa kazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Senso kwa vyombo vya habari Manumba ameacha kulitumikia jeshi hilo baada ya kufikia kikomo kiumri kwa mujibu wa taratibu.
“Jeshi la Polisi nchini linapenda kuutaarifu umma kwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) Robert Manumba amefikia umri wa kustaafu kisheria ambao ni miaka sitini (60) katika utendani wake wa kazi.” Imesema taarifa ya SSP Advera Senso.
Akifafanua zaidi msemaji huyo wa Polisi alisema katika utumishi wake ndani ya Jeshi la Polisi Manumba amefanya kazi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Chumba cha kupokea mashtaka kuanzia mwaka (1976 – 1977), mwendesha mashtaka wilaya ya Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma, 1977 – 1984), Mkufunzi katika chuo cha polisi Dar es salaam, (1984 – 1987), Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Magomeni na Kinondoni na Naibu Mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es salaam (1987 – 1993),
“Pia, amewahi kuwa Mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Arusha, ( 1993 – 1995), Mkufunzi mkuu wa Chuo Cha Polisi Moshi ( 1995 – 1996), Mkuu wa kitengo cha Fraud makao makuu ya upelelezi, (1996 – 1997), Mkuu wa kitengo cha usalama wa nchi, intelijensia na madawa ya kulevya makao makuu ya upelelezi (1997 – 2001) na kuwa msaidizi wa mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini (2001 – 2006). Kuanzia mwaka 2006 hadi anastaafu, alikua Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini.”
Aidha, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, amemshukuru na kumpongeza (DCI) Manumba anayestaafu kwa kulitumikia taifa katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi kwa weledi na uwaminifu mkubwa wakati wote alipokuwa mtumishi ndani ya Jeshi la Polisi.
IGP Mwema amemtaka kuendelea kuwa msaada kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa ushirikiano wa namna yoyote ile unaoweza kusaidia kupunguza uhalifu hapa nchini kwasababu suala la usalama ni taaluma kama zilivyo taaluma zingine, na taaluma hiyo wanayo watu wachache. Hata hivyo, wakati tataratibu wa uteuzi wa mkurugenzi wa upulelezi ukiendelea, mkuu wa ufuatiliaji na tathimini CID makao makuu, kamishina Isaya Mungulu, atakua akikaimu nafasi ya Robert Manumba.