MANISPAA ya Kinondoni inahitaji jumla ya Shilingi bilioni 1.3 ili kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete aliyezitaka halmashauri zote kuhakikisha zinajenga maabara katika shule za Sekondari ifikapo Novemba Mwaka huu.
Hayo yamebainishwa jana Jijini Dar es salaam na Naibu Meya wa Manispaa hiyo Songoro Mnyonge wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa shule, watendaji wa mitaa, kata pamoja na wenyeviti wa bodi za shule chenye lengo la kuangali namna ya kupatikana kwa fedha hizo.
Huku akiwaomba wadau mbalimbali yakiwemo mashirika, taasisi, watu binafsi pamoja na wafanyabiashara kujitokeza kuchangia upatikanaji wa fedha hizo, Songoro alisema ushirikiano wao katika suala hilo utaipa faraja manispaa hiyo kutokana na umuhimu wa elimu kwa taifa.
“Tunawaomba mjitokeze kwa wingi ili kuunga mkono juhudi za Rais Kikwete anayetaka kuona shule zote za sekondari zinakuwa na maabara za kudumu ili kusaidia kupanua wigo wa ufundishaji kwa wanafunzi mashuleni, jitihada zetu pekee hazitotuwezesha kufikia malengo hayo kutokana na ufinyu wa bajeti” alisema Mnyonge.
Aidha alisema manispaa hiyo inahitaji maabara za kudumu 114 kukidhi mahitaji katika kata 32 huku sekondari 14 ndizo pekee katika zilizo na maabara hizo kati ya 46 zilizopo katika manispaa hiyo suala alilosema linahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisema kila chumba kimoja cha maabara ya kudumu ujenzi wake unakadiriwa kufikia kiasi cha Sh Milioni 75 na kwa jumla ya vyumba vote 114 inahitajika kiasi hicho cha zaidi ya Sh Bilioni 1, suala alilosema haliwezi kufanikiwa bila nguvu za wadau mbalimbali.
Alisema malengo ya baadae ya manispaa hiyo ni kujenga vyumba vitatu vya maabara ya fikizia, kemia na baiolojia ifikapo mwaka 2016 hatu aliyosema kwa kiasi kikubwa itamaliza tatizo la ugumu wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi sambamba na kuongeza wataalam wa baadae wa Taifa hili.