Na Dotto Mwaibale
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Philip Mangula amewataka makada wa chama hicho wenye nia ya kugombea ubunge katika maeneo mbalimbali waache kiherehere cha kuanza kujipitisha katika majimbo wakati wabunge wa maenro hayo bado hawajamaliza muda wao.
Mangula alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa wajumbe wa Halmshauri kuu ya CCM, matawi, wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wao na mabalozi wa chama hicho wilaya ya Ilala, uliohusu utekelezaji wa ilani na mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika Dar es Salaam leo asubuhi.
“Nitoe angalizo kwa wale wenzetu wenye nia ubunge kuacha kiherehere cha kuanza kujipitisha majimboni kuanza kampeni kwa waache kufanya hivyo kwani katika majimbo hayo bado kunawabunge waliochaguliwa hawajamaliuza muda wao ” alisema Mangula.
Mangula aliongeza kuwa utaratibu wa chama upo wazi hivyo unapaswa kufuatwa na ukifika tutaona ni nani anapaswa kuendelea na ubunge kutokana na kile alichokifanya kutekeleza ilani ya chama au laa.
Aliwata viongozi wa ccm kuanzia ngazi za matawi kujenga tabia ya kufanya mikutano ya mara kwa mara ambayo itasaidia kujulikana kwa kero za wananchi na kuzifikisha serikali kwa utatuzi.
Mangula aliipongeza wilaya hiyo kwa kupata ushindi wa kuzoa viti vyote 28 katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa akazitaka na wilaya zingine kuiga mfano huo.
Mbunge wa Ilala, Mussa Azan ‘Zungu’ ambaye alikuwa akishangiliwa kila wakati na makada hao wa ccm alisema jimbo hilo limjitahidi kwa kiasi kikubwa kutekeleza ilani ya chama hicho kwa kuzipatia shule madawati, maji na katika michezo kugharamia timu 35 kuzipa vifaa katika kipindi cha miaka 10 pamoja na kutoa mikopo kwa wananchi wake kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali.
Zungu alitaja baadhi ya changamoto katika jimbo hilo kuwa ni kusumbuliwa kwa wamachinga, mama lishe na mgambo na ukamatwaji wa pikipiki zaidi ya 500 zinazotumika kama bodaboda ambazo zipo kituo cha polisi cha Chang’ombe. (Imeandaliwa na mtandao wa www.habarizajamii.com)