Manchester yafanya mauaji, yaifunga Arsenal 8-2, Man City yaizabua Tottenham 5-1

Mchezaji wa Man U, Wayne Rooney akishangilia goli.

WAYNE Rooney amepachika mabao matatu peke yake wakati Manchester United ikiinyuka Arsenal kwa mabao 8-2. Danny Welbeck ndiye alifungua karamu ya magoli baada ya kuunganisha pasi ya Anderson.

David De Gea aliokoa penati iliyopigwa na Robin Van Persi, na baadaye kidogo Ashely Young kufunga bao la pili. Rooney aliandika bao la tatu na la nne kwa mikwaju miwili ya adhabu, kabla ya kufunga bao moja kwa mkwaju wa penati.

Nani na Park Ji Sung walifunga nao na Ashley Young kuongeza jingine.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Theo Walcott na Robin Van Persie. Wakati huo huo katika mchezo wa awali timu ya Manchester City iliiazibu vibaya timu ya Tottenham Hotspur kwa mabao 5-1.

Edin Dzeko alifunga mabao manne, na Sergio Aguero akifunga moja. Bao pekee la Spurs lilifungwa na Younis Kaboul. Kwingineko Newcastle United imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fulham. Leon Best akifunga mabao yote ya Newcastle na goli la Fulham kufungwa na Clint Dempsey.

West Brom walishindwa kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuchapwa bao 1-0 na Stoke City. Goli hilo pekee lilifungwa na beki Ryan Shotton katika dakika ya 89.