Man United chali, yapigwa 6-1 kwao

Beki wa Man U, Jonny Evans akiwa aamini kilichotokea alitoka kwa kadi nyekundu

MANCHESTER City imeizaba Manchester United 6-1 kwenye uwanja wa Old Trafford. Kinyume na matarajio ya Wengi, Man United walishindwa kabisa kuhimili vishindo vya majirani zao na mahasimu wao wa jadi.
Hadi mapumziko City walikuwa wakiongoza kwa goli moja lililofungwa na Mario Balotelli.
Man United walicheza karibu kipindi chote cha pili wakiwa na mchezaji mmoja pungufu baada ya beki, Jonny Evans kupewa kadi nyekundu kwa kumzuia Balotelli kwenda kumuona kipa wa United David De Gea.

Baada ya kutolewa kwa Evans, karamu ya magoli ilianza kwa City. Balotelli aliongeza bao la pili katika dakika ya 60. Sergio Aguero akafunga bao la tatu katika dakika ya 69.

Edin Dzeko baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba alifunga bao la nne katika dakika ya 90, David Silva bao la tano na Dzeko tena kupiga msumari wa mwisho katika filimbi ya mwisho ya mchezo. Bao pekee la kufutia machozi la United lilifungwa na Darren Fletcher katika dakika ya 81.
Matokeo haya yanaipa City pointi tatu ambazo zinaifanya kuendelea kuongoza kwa pointi tano zaidi ya United. Katika michezo mingine, Arsenal iliizaba Stoke City 3-1. Gervino aliandika bao la kwanza katika dakika ya 27, ingawa bao hilo lilisawazishwa na Peter Crouch.

Hata hivyo Robin Van Persie ambaye alianza bechi katikika mchezo huo aliingia na kufunga mabao mawili. Everton nayo ikicheza ugenini ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Fulham. Mabao ya Everton yakifungwa na Royston Drenthe, Luis Saha na Jack Rodwell. Bao la Fulham lilifungwa na Bryan Ruiz.

-BBC