Dk. Kigwangala pia amemwamuru Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asilia na Mbadala wa Serikali ndani ya wiki moja kufanya ukaguzi wa kina juu ya tiba inayotolewa na kituo hicho na kuangalia dawa zake kama ni rafiki kwa watumiaji ikiwa ni pamoja na kuvikagua vituo vingine kama hivyo vikiwemo vya Dk. Ndodi, Dk. Rahabu, na wengineo ili kuwabaini wanaowalaghai wananchi juu ya tiba feki.
Awali Naibu Waziri na msafara wake walizuiwa kabla ya kuingia na wahusika kukimbia kwani hakukuta daktari yoyote ndani ya vyumba vyote vya matibabu na badala yake aliwakuta wasaidizi ambao walishindwa kujibu maswali ya Naibu Waziri juu ya huduma wanazozitoa huku kukiwa na foleni za wagonjwa wakisubiri huduma hivyo kuwashauri kwenda hospitalini ili wakapate matibabu fasaha.
Alishangazwa na kitendo cha watoaji wa tiba mbadala kujitokeza kwa kutumia vyombo vya habari na kuuchambua mwili wa mwanadamu kana kwamba wamesomea jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu. Alisema ni kosa kujitangaza kama unatoa tiba za utabibu kwenye vyombo vya habari, kwani sheria hairuhusu mtu wa tiba asilia kutumia maneno ya tiba za kisasa katika shughuli zake.
Hivi karibuni kumeibuka mjadala ukijadili juu ya ukweli wa matibabu ya Dk. Mwaka baada ya mtandao mmoja wa kijamii kuandika ukidai kuwa dawa hizo za asili zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya watumiaji kuwa hazina ukweli, hata hivyo upande uliolalamikiwa haujatoa taarifa ya kukanusha kabla ya serikali kuvamia kituo hicho.
Hata hivyo kumekuwa na ongezeko kubwa la baadhi ya watu na vituo kuibuka na kujitangaza kila uchao kwa vyombo vya habari kuwa wanatoa huduma mbadala na kutibu magonjwa mbalimbali hadi magonjwa ambayo yamekuwa hayatibiki uku vikiwa na gharama kubwa za matibabu jambo ambalo limekuwa likiibua maswali kwa baadhi ya watu.