Mambo Muhimu ya Kuzingatia Unapokwenda Kutoa Hotuba…!

Hayati Baba wa Taifa, Julias K. Nyerere

Hayati Baba wa Taifa, Julias K. Nyerere


Ndugu zangu,
MADA kuhusu sanaa ya kuzungumza mbele ya hadhara imevuta wengi. Bila shaka, sababu kuu ni ukweli, wengi tunapata tabu sana kila tunapotakiwa kuongea hadharani. Kwa vile hata waliozaliwa na vipaji vya kuongea hadharani na kuvuta watu wanahitaji kujifunza zaidi, basi, hata asiye na kipaji, anaweza kujifunza na akawa mzungumzaji mzuri mwenye kuvutia hadhira yake.

Leo nitazungumzia kile kilicho muhimu kabisa kwa mtu anayehutubia. Kinaitwa ‘actio’ kwa Kigiriki.
Actio inahusu zaidi kinachoonekana kwa nje na hadhira ama wasikilizaji pale mzungumzaji anapokuwa akihutubia. Ni ile misogeo au mitikisiko mbalimbali ya mzungumzaji kimwili ikiwa ni pamoja na sauti na hata mawasiliano ya mboni za macho ya mzungumzaji na wasikilizaji wake.

Muhimu sana unavyozungumza. Jinsi unavyoitumia sauti yako vile unavyohama kutoka hali tofauti za sauti. Unavyobadilisha ukubwa ama ujazo wa sauti yako. Na ni kwa namna gani, wakati mwingine, kulingana na neno au sentesi unayotaka kuisema unavyobadilisha sauti yako. Mfano mzuri hapa ni Julius Nyerere, aliweza kucheza vizuri na sauti katika hali zote; “.. Ni watu wa ovyo ovyo tu…!” Hapo aliweza kuibana sauti ikasikika kwa namna ya kuvutia kuweka msisitizo wa anachotaka kusema.

Ufundi Ni Upi Kwenye Kuhutubia?
Ili uweze kutoa hotuba ya nguvu ikaweza hata kuwaacha watu wasitamani umalize na kuondoka ni sharti mzungumzaji uwe na uwezo wa kumiliki vitu vitatu;
1. Mimic – inahusu taswira. Hapa ni jinsi unavyocheza na mdomo, macho, na hata kope za macho.
2. Prosodi- Ni neno la Kigiriki hili, ina maana ya namna unavyotumia sauti na hata unapoweka vituo kwenye hotuba.

3. Gestik- Hapa inahusu unavyotumia viungo vya mwili wako ukiwa jukwaani.
Tujikite kwenye Mimic. Eneo hili ni muhimu sana maana ndipo hupelekea wasikilizaji ama wamuamini mzungumzaji au wasimwamini. Kama kinachoonekana kwenye mdomo na macho yako hakifanani na unachosema, kuna wataoguna mioyoni, kuwa unawadanganya. Ndipo hapa tena, Julius Nyerere alipata kusema; :” Mgombea akisema anakemea rushwa, basi, tukimuangalia usoni tuseme , naam, huyu kweli anakemea rushwa!”
Mzungumzaji unaweza ukakochiwa namna ya kuwasiliana kwa mimic. Na tabasamu la kweli huonekana kwa wasikilizaji. Hutokea mzungumzaji akatabasamu lakini macho yamenuna. Hilo ni tabasamu la uongo.

Tabasamu la kweli huonekana machoni. Hapa tena Julius Nyerere ni mfano wa wazungumzaji walioweza kuonyesha tabasamu na macho yakatabasamu pia. Tabasamu ni muhimu sana kwenye hotuba. Ni kama kiungo kwenye chakula. Tabasamu huashiria mzungumzaji ni mtu rafiki, anasogelekeka kwa mazungumzo. Mzungumzaji katika hili tafuta yale ambayo unajua hata wewe ukiyasema hadharani yatakufurahisha. Utatabasamu tu kiuasilia…
Itaendelea…
Kwa mwenye kutaka ushauri wa bure wasiliana nami;
0754 678 252
Maggid.
Dar es Salaam.