‘Mambas’ wa Msumbiji kutua Dar leo

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Msumbiji

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) itawasili nchini kesho (Februari 26 mwaka huu) kwa ndege ya South African Airways. Ndege hiyo yenye mruko namba SA 186 inatarajia kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 7.55 mchana.

Msafara wa Mambas kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano ya Februari 29 mwaka huu saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa na watu 29. Kati ya hao, 19 ni wachezaji wakati waliobaki ni maofisa wa timu hiyo.

Mwamuzi wa mechi hiyo Farouk Mohamed na wasaidizi wake Ayman Degaish, B.T Abo El Sadat na Gihed Greisha kutoka Misri watawasili nchini Februari 26 mwaka huu kwa ndege ya Egypt Air. Kamishna ni Loed Mc Ian kutoka Afrika Kusini.

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa Jumanne ya Februari 28 mwaka huu katika vituo vya vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.