Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amezindua mradi wa kuhifadhi ya maji kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60 na kutoa wito kwa uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha kuwa mradi huo unatunzwa ili kuufanya uwe endelevu.
Mradi huo ambao umefadhiliwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) una uwezo wa kuhifadhi lita 40,000 za maji na unatarajiwa kutosheleza mahitaji ya watu 150,000 kwa sasa.
Akizungumza na mamia wa wakazi wa Manispaa ya Moshi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo, Jumatatu, Julai 30, 2012 kwenye Hospitali ya Mawenzi, Mama Pinda alisema anatambua changamoto inayoikabili hospitali hiyo ambayo mahitaji yake ya maji kwa siku ni lita 200,000.
“Kuwekwa kwa matenki haya kutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la kuhifadhi maji katika hospitali hii. Hata hivyo, bado changamoto ipo kwa vile pamoja na juhudi hizi bado kutakuwa na mahitaji ya kuhifadhi kiasi cha lita 160,000 ili kutatua tatizo zima la maji hapa hospitali ya Mawenzi,” alisema.
Mama Pinda aliishukuru kampuni ya SBL kwa ufadhili wake na kutumia fursa hiyo kuwaomba wadau wengine ambao wanapenda maendeleo na wanaguswa na tatizo la maji katika hospitali hii wajitokeze na kuchangia ujenzi wa matenki ya ziada.
“Jitihada za wadau wengine zinahitajika kwani hata lile tenki lililokuwepo zamani lenye uwezo wa kuhifadhi lita 20,000 nalo limeanza kuvuja. Na mimi nimelishuhudia. Kwa hiyo, ni wakati muafaka wa kuendelea kutoa mchango wetu katika kusaidia miradi ya maendeleo katika hospitali yetu,” alisisitiza..
Mapema, akisoma taarifa mbele ya mgeni rasmi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mtumwa Mwako alisema upatikanaji wa maji katika hospitali hiyo haukuwa mzuri kwa sababu ya ukame na ongezeko la idadi ya wakazi katika manispaa ya Moshi.
Alisema mahitaji ya maji kwa siku ni lita 200,000 ambazo ni sawa na lita milioni sita kwa mwezi ambayo kwa mwaka yanafikia lita milioni 72. Hata hivyo, Dk. Mwako alisema mahitaji hayo yanakadiriwa kuongezeka pindi majendo ya upasuaji na wodi ya wazazi yatakapokamilika na kuanza kutumika.
“Inakadiriwa kuwa mahitaji ya maji yataongezeka na kufikia lita 300,000 kwa siku na mwezi yatafikia lita milioni tisa,” aliongeza Dk. Mwako.
Alisema hospitali hiyo ambayo ilijengwa mwaka 1920 kama zahanati ya kutibu Waafrika, inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kufungwa kwa jengo la upasuaji katika hospitali hiyo ya mkoa tangu Desemba 27, 2010; uchakavu wa majengo, hospitali kukosa uzio wa kuaminika na msongamano wa wagonjwa katika idara na wodi kadhaa na ukosefu wa watumishi wa afya na hasa madaktari bingwa. Aliishukuru kampuni ya SBL kwa ufadhili wake na kuiomba iwasaidie kukarabati chumba cha upasuaji mdogo.
Naye Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa SBL, Bi. Teddy Mapunda alisema kampuni imejikita kusaidia maeneo manne ambayo ni maji, uhifadhi wa mazingira, elimu na afya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, akimkaribisha Mama Tunu Pinda kuzungumza na hadhira iliyoshuhudia uzinduzi huo aliahidi kuhakikisha kuwa mradi huo unatunzwa ili uendelee kuwasadiai mamia ya wakazi wanaofika kwenye hospitali hiyo ua mkoa.