Mama Tunu Pinda Awataka Watanzania Kumshukuru Mungu

MKE wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda amesema kila mtu hana budi kumshukuru Mungu kwa kumfikisha salama wakati wa sikukuu ya Noeli kwani kuna wengine ambao walitamani kuiona siku hii lakini wameshindwa.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Desemba 25, 2012) wakati wa ibada ya Krismasi iliyofanyika katika kigango cha Kibaoni kata ya Kibaoni wilayani Mlele, mkoani Katavi.

“Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika sikukuu hii, mpaka leo ni mapenzi yake hakuna binadamu ambaye ana amri na maisha yake. Tutakumbuka hata mwaka jana tulikuwa na Askofu wetu wa Jimbo la Mpanda lakini leo hii hatunaye, hivyo sote tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai,” alisema.

Alisema katika kuadhimisha sikukuu hii watu hawana budi kuwa na kiasi, wasinywe sana hadi kusababisha magomvi. Aliwasihi wazazi wawe karibu na familia zao, na wawajibike kwao.

”Tumuombe Mungu atupe neema, yale tuliyokosea mwaka 2012 tuyaache, tujiandae kuingia mwaka 2013 na yale mazuri tuliyoyaona mwaka 2012,” alisema.

Naye Padre John Giji wa Shirika la Wamisionari wa Mt. Thomas ambaye aliongoza ibada hiyo, aliwataka waumini wa kigango hicho kuwajali wenye shida na siyo kujiingiza katika matendo mabaya wakati wa sikukuu.

“Kuishi kwetu kuanzia leo lazima kuwe na mabadiliko, ni lazima tuwajali wenzetu katika shida zao kwani kwa kufanya hivyo, tutakuwa na mabadiliko ya kiroho na hivyo kuweza kukua kiimani,” alisema Padre John ambaye pia ni Paroko wa Usevya.

“Wako watu wanasherehekea Krismasi kwa matendo mabaya kama vile uzinzi na ujambazi. Huo siyo ukristu tunaotegemewa kuwa nao katika familia takatifu ya Mungu. Tukifanya kazi kwa bidii, hatuwezi kuwa na tamaa ya vitu vya wengine,” alionya.

“Leo ni sikukuu, tufurahi kwa amani bila jazba za kidunia. Tusherehekee kwa upendo na amani, ” alisisitiza.