Mama Tunu Pinda Awaasa Makatibu Muhtasi kuzingatia Maadili Yao

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda


 
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewaasa Makatibu Muhtasi na kuwataka wazingatie maadili ya taaluma yao ya uhazili ili kuongeza ufanisi wa majukumu ya kazi zao. Ametoa wito huo Alhamisi, Mei 16, 2013 wakati akifungua Kongamano la Tatu la Makatibu Muhtasi (Tanzania Personal Secretaries Association – TAPSEA) kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC), Jijini Arusha.
 
Kongamano hilo la siku mbili, limehudhuriwa na Makatibu Muhtasi zaidi ya 1,500 kutoka mikoa yote nchini, na baadhi ya wawezeshaji kutoka Kenya, Uganda na Rwanda.
 
“Umuhimu wa taaluma ya uhazili katika taasisi tunazofanyia kazi unatokana na nafasi  kubwa ya makatibu muhtasi kama wasimamizi wa ofisi na wasaidizi wa watendaji wakuu. Nafasi yenu inawapa fursa ya kuandaa na kutunza nyaraka mbalimbali za kiofisi zinazohusu menejimenti ya taasisi hizo. Niwaombe makatibu muhtasi wote mzingatie maadili ya kazi ya uhazili katika kutekeleza majukumu yenu,” alisisitiza.
 
Aliwataka waongeze jitihada za kukimarisha Chama cheo ili hatimaye TAPSEA iweze kuenea Mikoa yote na kuwa Chombo kitakachosimamia miiko na maadili ya fani ya Uhazili. Alisema majukumu ya makatibu muhtasi siyo kupiga chapa pekee na kuongeza kwamba, kama chama cha kitaaluma, TAPSEA lazima iendeleze jitihada za kubadili mtazamo huo ili jamii iweze kutambua umuhimu wa nafasi ya makatibu muhtasi katika taasisi mbalimbali za umma na za sekta binafsi.
 
“Hata hivyo, napenda ieleweke kwamba kazi ya kuleta mabadiliko ya kimtazamo inaanzia kwa katibu muhtasi mwenyewe. Nawashauri wanachama wote wa TAPSEA wawe mstari wa mbele katika kubadilika kifikra na kujiendeleza kila wakati ili kujijengea uwezo wa kuzikabili ipasavyo changamoto za taaluma ya uhazili katika mazingira ya sasa,” alisema.
 
Mama Tunu Pinda alisema kuwekeza katika teknolojia ni jambo muhimu lakini teknolojia pekee haiwezi kuleta mabadiliko chanya katika kuboresha huduma na kuongeza tija. “Jambo hili ni lazima liende sambamba na uwekezaji katika rasilimali watu kwa watumishi kusoma zaidi na kupatiwa fursa za mafunzo zaidi ndani na nje ya nchi,” alisisitiza. Mama Tunu Pinda pia alizindua TAPSEA SACCOS na kuwataka makatibu muhtasi hao wajiunge kwa wingi ili kutunisha mfuko wa chama chao.
 
Mapema, akimkaribisha kuzungumza na washiriki wa mkutano, Mlezi wa TAPSEA Dk. Mary Nagu ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Uwekezaji na Uwezeshaji aliwataka wawe waaminifu katika kuijenga TAPSEA SACCOS ili hatimaye ifikie hatua ya kuwa benki yao maalum kama ilivyo kwa Chama cha Walimu nchini.
 
Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Angela Kairuki ambaye pia mshauri wa Kisheria wa TAPSEA aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuzingatia maadili kwa kutunza siri za ofisi wanazozitumikia.
 
“Inasikitisha kuona kila mara kunakuwa na taarifa ambazo zinavuja lakini ukifuatilia wapi taarifa hizo zimetokea utabaini kuwa chanzo ni makatibu muhtasi… ninawaomba sana mjitahidi kutunza siri za taasisi zenu,” alisisitiza.