Mama Tunu Pinda Ataka Elimu Itolewe Bila Ubaguzi wa Kijinsia

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda akizungumza.

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda akizungumza.

Na Mwandishi Wetu

MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewataka wazazi hapa nchini watoe kipaumbele kwenye suala la elimu kwa vijana bila ubaguzi wa kijinsia. Ametoa wito huo Machi 8, 2014 wakati akifungua Kongamano la Wanawake wa Afrika ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
 
Kongamano hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu Wanawake Tanzania (Tanzania Women Teachers’ Association – TAWOTEA) kwa kushirikiana na taasisi ya African Women Charity Organisation ya Oakland, California, Marekani.
 
Akizungumza na washiriki wa kongamano hilo, Mama Tunu Pinda alisema: ”Ninawaomba wazazi wenzangu, wake kwa waume tuungane kwa pamoja kwa kutoa kipaumbele kwenye suala zima la elimu kwa vijana wetu bila ubaguzi wa kijinsia. Kwa kufanya hivyo tutawajenga wavulana na wasichana ili wawe na uwezo wa kiuchumi na uthubutu katika masuala ya uongozi na maisha yao ya baadaye.”
 
Akizindua mfuko wa elimu ulioanzishwa na chama hicho, Mama Pinda  alisema ana imani utakuwa endelevu na utakidhi malengo ya kuazishwa kwake ambayo ni kuwasaidia watoto wenye uhitaji na waishio kwenye mazingira ili wapate elimu ya msingi na ya sekondari.
 
”Mkiwa ni waalimu wanawake na tena ni walezi wa watoto wetu, mmefanya jambo kubwa na la kihistoria kwa kuanzisha mfuko wa elimu mlioamua kuuita Tanzania Education Fund (TEF). Nimedokezwa kwamba malengo ya mfuko huu ni kusaidia gharama za elimu ya msingi na sekondari kwa watoto wa kike na wa kiume na hasa kwa watoto walio kwenye mazingira magumu na wenye uhitaji. Ni matumaini yangu kwamba utakuwa endelevu.”
 
”Ni imani yangu kwamba kupitia mfuko huu unaozinduliwa rasmi leo hii, utaowaongezea vijana wetu wa kike na wa kiume wigo wa kupata elimu ambapo kama mfuko huu usingekuwepo, isingekuwa rahisi kwao kumudu gharama za masomo,” aliongeza.
 
Aliwaomba wadau wote wa elimu na wananchi kwa ujumla, waunge mkono juhudi za walimu hao katika kuikomboa nchi hii, hasa katika sekta ya elimu huku wakiamini elimu ni ufunguo wa maisha.
 
Mapema, akisoma risala yao, Mkurugenzi Mtendaji wa TAWOTEA, Mwl. Neema Kabale alisema asasi hiyo ambayo imesajiliwa tangu mwaka 2008, inajihusisha na utetezi wa haki za msingi za wanawake, wasichana, vijana na watoto katika masuala ya elimu, afya, na upatikanaji wa chakula.

Katika kongamano hilo la siku moja, asasi hiyo iliandaa mada sita zikiwemo za “Ushiriki wa wanaume katika ukombozi wa mwanamke” na “Majukumu ya Vijana katika Muungano wa Afrika”.

Akitoa hitoria fupi ya Kongamano la Wanawake Afrika, Rais wa taasisi ya African Women Charity Organisation ya Oakland, Marekani, Bi. Rwanda Saleem, alisema Tanzania ni nchi ya nane kupata fursa ya kuratibu wa kongamano kama hili.
 
”Barani Afrika tayari nchi saba zimekuwa  waratibu wa kongamano hili ambazo ni Ghana, Guinea, Gambia, Senegal, Kenya, Rwanda, na Msumbiji ambayo ilikuwa mwenyeji mwaka jana. Tanzania imepewa fursa ya kuandaa kongamano hili mwaka huu,” aliongeza.
 
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Kujenga Muungano wa Afrika kwa Kushirikisha Wanawake kwenye Uongozi” (The Unification of Africa Through the Emancipation of Leadership of Women).